'
Wednesday, January 16, 2013
WAMBURA AJITOSA TFF
KATIBU Mkuu wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT), Michael Wambura amechukua fomu kwa ajili ya kuwania uongozi katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Wambura amechukua fomu ya kuwania nafasi ya makamu wa rais wa shirikisho hilo.
Wambura alisema wagombea wengine watano walichukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika shirikisho hilo na kufanya jumla ya wagombea waliojitokeza hadi sasa kuwa 26.
Aliwataja wagombea hao, ambao wote wanawania nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji kuwa ni Mbasha Matutu, Muhsin Balhabou, Salum Chama, Titus Osoro na Zafarani Damoder.
Uchaguzi mkuu wa TFF umepangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu, ambapo nafasi zinazogombewa ni ya rais, makamu wa rais na wajumbe 13 wa kamati ya utendaji.
Idadi kamili ya waliochukua fomu, nafasi wanazogombea zikiwa kwenye mabano ni Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia (makamu wa rais).
Wanaogombea ujumbe, kanda zikiwa kwenye mabano ni Salum Chama (Kagera na Geita), Mugisha Galibona, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mungodo, Elly Mbise na Twahili Njoki (Arusha na Manyara).
Wengine ni Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa), James Mhagama (Njombe na Ruvuma), Athuman Kambi (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Shaffih Dauda na Zafarani Damoder (Dar es Salaam).
Wakati huo huo, Said Mohamed amechukua fomu ya kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment