KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 31, 2013

PINGAMIZI DHIDI YA MANJI, MALINZI, NYAMLANI ZATUPWA



MAAMUZI KUHUSU PINGAMIZI DHIDI YA WAOMBAJI UONGOZI
WA TFF NA TPL BOARD
31 JANUARI 2013

Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(4) katika kikao chake kilichofanyika tarehe 30 Januari 2013, ilijadili pingamizi zilizowekwa dhidi waombaji uongozi wa TFF na TPL Board na kutoa maamuzi kama ifuatavyo:

1. Waombaji uongozi wa TPL Board

(a) Pingamizi dhidi ya Ndg. Said Muhammed Abeid anayeomba kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPL Board): Kamati ilijadili pingamizi iliyowasilishwa na Ndg. Frank M. Mchaki dhidi ya Ndg. Said Muhammed, aliyeoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kumwondoa mwombaji uongozi kugombea nafasi aliyoomba, kwamba Ndg. Said Muhammed:

(i) Si Mwenyekiti wa Klabu ya Azam na hivyo hana sifa za kugombea uongozi wa TPL Board.

(ii) Si mkweli katika maelezo aliyoyatoa kwenye fomu yake ya maombi ya uongozi.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia maelezo ya Mweka pingamizi na ilijiridhisha kuwa pingamizi iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Mchaki haikukidhi matakwa Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) kwa kuwa haikuambatanishwa na vielelezo vyovyote kuthibitisha maelezo ya pingamizi. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa pingamizi hiyo.

(b) Pingamizi dhidi ya Ndg. Yusufali Manji anayeomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPL Board): Kamati ilijadili pingamizi zilizowasilishwa na Ndg. Daniel T. Kamna na Ndg. Juma Ally Magoma walioomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kumwondoa mwombaji uongozi kugombea nafasi aliyoomba, kwamba Ndg. Yusufali Manji :

(i) Hana uzoefu wa uendeshaji wa Mpira wa Miguu uliothibitishwa wa angalau miaka mitano (5) wa uendeshaji wa mpira wa miguu.

(ii) Hana sifa ya kuwa ama mchezaji Mpira wa Miguu, Kocha, Mwamuzi au kushiriki katika uendeshaji wa Mpira wa Miguu katika ngazi ya Mkoa au Ligi daraja la kwanza.

(iii) Hana elimu ya kidato cha nne

(iv) Ameshindwa kusimamia katiba ya Young Africans Sports Club Ibara ya 10(6), 18(1)b, 27 (2) na (5).

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia pingamizi hizo na ilijiridhisha kuwa pingamizi zilizowasilishwa mbele yake na Ndg. Daniel T. Kamna na Ndg. Juma Ally Magoma hazikukidhi matakwa Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) kwa kuwa hazikuambatanishwa na vielelezo vyovyote kuthibitisha maelezo ya pingamizi. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imezitupa pingamizi hizo.

(c) Pingamizi dhidi ya Ndg. Hamad Yahya Juma anayeomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPL Board): Kamati ilijadili pingamizi iliyowasilishwa na Ndg. Frank M. Mchaki dhidi ya Ndg. Hamad Yahya Juma, kwamba Ndg. Hamad Yahya Juma:

(i) Si Mwenyekiti wa Klabu ya Mtibwa na hivyo hana sifa za kugombea uongozi wa TPL Board.

(ii) Si mkweli na mwadilifu na amekuwa akijipachika cheo cha mwenyekiti wa klabu.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa pingamizi ya Ndg. Frank M. Mchaki kwa kuwa pingamizi iliyowasilishwa mbele yake haikukidhi matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) kwa kutoambatanishwa na vielelezo vyovyote kuthibitisha maelezo ya pingamizi.

2. Waombaji uongozi wa TFF

(a) Pingamizi dhidi ya Ndg. Athumani K. Kambi anayeomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 9 (Mtwara na Lindi): Ndg. Kambi aliwekewa pingamizi kwamba amefanya Kampeni kabla ya muda uliopangwa.

Kamati imeitupa pingamizi ya Ndg. Jeremiah John Wambura kwa kuwa mweka pingamizi hakutokea wakati alipotakiwa kufika kwenye Kamati ya Uchaguzi kutoa utetetezi wake kuhusu pingamizi.

(b) Pingamizi dhidi ya Ndg. Eliud P. Mvella anayeomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 7 (Iringa na Mbeya): Ndg. Mvella aliwekewa pingamizi na Ndg. Said Kiponza, Ndg. Abu Changawa na Ndg. Peter Naminga, kwamba Ndg. Mvella:

(i) Akiwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda hiyo ameshindwa kuleta maendeleo ya soka katika ukanda huo.

(j) Ana kesi ya rushwa katika mahakama ya wilaya ya Iringa

Kamati imeitupa pingamizi hiyo kwa kuwa haikukidhi matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) kwa kutoambatanishwa na vielelezo vyovyote kuthibitisha maelezo ya pingamizi.

(c) Pingamizi dhidi ya Ndg. Epaphra Swai anayeomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 3 (Shinyanga na Simiyu): Kamati ilijadili pingamizi zilizowasilishwa na Ndg. Ramadhani Sesso na Ndg. Tsotsie Chalamila, kwamba Ndg. Epaphra Swai:

(i) Alifanya ubadhilifu wa fedha alipokuwa Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA).

(ii) Alitumia madaraka yake vibaya alipokuwa MZFA kujinufaisha kwa kutumia MZFA.

(iii) Alivunja Katiba ya MZFA na FIFA

(iv) Anavuruga shughuli za uendeshaji mpira wa miguu mkoani Simiyu.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia pingamizi hizo na ilijiridhisha kuwa wawekaji pingamizi hawakuwa na sababu za msingi zilizoambatana na vielelezo vinavyothibitisha maelezo ya pingamizi na kuwa pingamizi zilizowasilishwa mbele yake zina chembechembe za wazi za mapatano ya hila na udanganyifu (collusion) dhidi ya Ndg. Epaphra Swai. Kwa kutokidhi matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) na hila/udanganyifu kwa Kamati, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imezitupa pingamizi hizo.

(d) Pingamizi dhidi ya Ndg. Vedastus F.K Lufano na Ndg. Mugisha Galibona wanaoomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 2 (Mwanza na Mara): Ndg. Lufano na Ndg. Galibona waliwekewa pingamizi na Ndg. Paul Mhangwa kwamba hawana uzoefu wa uendeshaji wa Mpira wa Miguu wa miaka mitano (5).

Kamati imeitupa pingamizi hiyo kwa kuwa haikuzingatia Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2).

(e) Pingamizi dhidi ya Ndg. Michael R. Wambura anayeomba kugombea nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF: Pingamizi ziliwasilishwa na Ndg. Said Rubea Tamim na Ndg. Josea Samuel Msengi kwamba Ndg. Wambura:

(i) Alikiuka Katiba ya TFF kwa kuishitaki Klabu yake ya Simba mahakamani kuhusu masuala ya uchaguzi.

(ii) Alikosa uadilifu kwa kutumia kampuni yake binafsi kufanya biashara na Taasisi aliyokuwa aniongoza akiwa Katibu Mkuu wa FAT.

(iii) Amekuwa akijaribu kupotosha umma kwamba vyombo vya TFF havifanyi kazi zake kwa kutumia haki na kuviita ‘Mahakama za Kangaroo (Kangaroo Courts).

(iv) Mwaka 2004 alikiri kwamba alikuwa akiandikwa vizuri na vyombo vya habari kwa kuwa alikuwa akivipa pesa na kwamba vyombo vya habari vilimgeuka kwa sababu aliacha kuwapa waandishi pesa.

(v) Mwaka 2004 alikataa kutekeleza maagizo ya FIFA ya kutaka nafasi ya Katibu Mkuu wa FAT iwe ya kuajiliwa.

(vi) Alikosa uwezo wa kutekeleza wajibu na malengo ya TFF.

Ndg. Josea Samuel Msengi aliondoa pingamizi lake dhidi ya Ndg. Wambura. Kamati imelitupa pingamizi la Ndg. Said Rubea Tamim kwa kuwa halikukidhi matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2).

(f) Pingamizi dhidi ya Ndg. Jamal E. Malinzi anayeomba kugombea nafasi ya Rais wa TFF; Aliwekewa Pingamizi na Ndg. Agape Fue kwamba:

(i) Alivunja Katiba ya TFF kwa kufanya jitihada kubwa za kuhakikisha kuwa wanachama wa TFF kikiwemo Chama chake cha Mkoa wa Kagera haviheshimu wala kutekeleza maagizo ya TFF, CAF, CECAFA na FIFA baada ya Kamati ya Utendaji ya TFF kuwasilisha mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba kwa njia ya Waraka, ambayo yalihusisha pia maagizo ya FIFA na CAF

(ii) Hana sifa ya uzoefu wa miaka mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.

(iii) Anakosa uadilifu na haiba ya kuliwakilisha Shirikisho nje na ndani.

Kamati imeitupa pingamizi ya Ndg. Agape Fue kwa kuwa mweka pingamizi hakutokea wakati alipotakiwa kufika kwenye Kamati ya Uchaguzi kutoa utetetezi wake kuhusu pingamizi hilo.

(g) Pingamizi dhidi ya Ndg. Athumani J. Nyamlani anayeomba kugombea nafasi ya Rais wa TFF: Ndg. Nyamlani aliwekewa pingamizi na Ndg. Mintanga Yusuph Gacha na Ndg. Medard Justiniani kwamba:

(i) Ni Hakimu Mkazi katika Mahakama ya Tanzania na kwa maana hiyo ni mtumishi wa umma hivyo alikosa kigezo na sifa ya kugombea nafasi ya urais wa TFF.

(ii) Anakatazwa na Judicial Service Act, Public Service Act 2002 na Code of Conduct for Judicial Officers of Tanzania kugombea nafasi aliyoomba ya Rais wa TFF.

(iii) Kutakuwa na Mgoganao wa kimaslahi endapo Ndg, Nyamlani atachaguliwa kuwa Rais wa TFF.

(iv) Amekosa umakini na uadilifu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake na kusababisha Akanunti za TFF kufungiwa na TRA.

Ndg. Mintanga Yusuph Gacha hakufika kutetea Pingamizi lake ni hivyo halikujadiliwa na Kamati. Kamati imelitupa pingamizi la Ndg. Medard Justiniani kwa kuwa alishindwa kuithibitishia Kamati kuwa alikuwa na ufahamu wa kutosha wa pingamizi lake ikiwa ni pamoja na viambatanisho vyake, hali iliyotanabaisha kuwa pingamizi hilo lilikuwa na chembechembe nyingi za hila na udanganyifu.

Angetile Osiah
KATIBU
KAMATI YA UCHAGUZI

KIM ATANGAZA KIKOSI CHA STARS CHA KUIVAA CAMEROON




Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini Jumapili (Februari 3 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Cameroon (Indomitable Lions).

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo (Januari 31 mwaka huu), Kim amesema mechi dhidi ya Cameroon itakuwa kipimo kizuri kwake kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya kucheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayofanyika Machi mwaka huu.

“Itakuwa mechi ngumu na kipimo sahihi kwetu. Tuko tayari, tutacheza kwa staili yetu kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya mechi dhidi ya Morocco. Ni mechi nzuri kwa sababu wachezaji wameonyesha wako tayari.

“Tumetoka kucheza dhidi ya Zambia na Ethiopia. Lengo ni Taifa Stars kucheza fainali za AFCON 2015, kwa hiyo mechi dhidi ya Cameroon ni sehemu ya mipango yetu kuhakikisha tunafika huko,” amesema Kim ambaye amerejea nchini juzi kutoka Afrika Kusini kuzifuatilia timu za Morocco na Ivory Coast zilizo kundi moja na Tanzania katika mechi za mchujo za Kombe la Dunia.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Stars inashika nafasi ya pili katika kundi lake nyuma ya Ivory Coast inayoongoza. Timu nyingine katika kundi hilo ni Gambia.

Wachezaji aliowaita kwenye kikosi chake ni makipa Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid (Mtibwa Sugar).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Simon Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd (Yanga) na Mwinyi Kazimoto (Simba). Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Tuesday, January 29, 2013

HATIMAYE LULU APATA DHAMANA, ASEMA 'NIOMBEENI, SAFARI NDEFU'


NA FURAHA OMARY WA GAZETI LA UHURU

“WATU waendelee kuniombea, hii ni dhamana tu, lakini kesi bado, safari ni ndefu. Namshukuru Mungu, yeye ndiye kila kitu.”

Hiyo ni kauli ilitolewa na msanii wa maigizo nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, baada ya kuachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, katika kesi inayomkabili ya kuua bila kukusudia.

Lulu, ambaye alikuwa anasota rumande kwa takriban miezi minane katika gereza la Segerea, kuanzia Aprili mwaka jana, anashitakiwa kwa kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Msanii huyo aliachiwa huru kwa dhamana jana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu wa Kanda hiyo, Francis Kabwe baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyotolewa juzi na Jaji Zainabu Mruke wa mahakama hiyo.

Akizunguzumza na waandishi wa habari baada ya kutoka nje ya jengo la Mahakama Kuu, Lulu alisema anawashukuru watu wote na kuwaomba waendelee kumuombea kwa kuwa hiyo ni dhamana tu,kesi bado inaendelea na safari ni ndefu.

Monday, January 28, 2013

LULU ALIPOTINGA MAHAKAMA KUU LEO, DHAMANA YAKE KESHO



MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imetoa masharti ya dhamana kwa msanii wa maigizo nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, ambaye anakabiliwa na kesi ya kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba.


Hata hivyo, Lulu ambaye alikuwa na uso wa furaha jana baada ya kutolewa kwa masharti hayo, alirudishwa rumande kutokana na kutokuwepo kwa Msajili wa Mahakama Kuu wa kanda hiyo, kwa ajili ya kuhakiki iwapo masharti yaliyotolewa na Jaji Zainabu Mruke yametimizwa.

Masharti hayo ya dhamana ni kwamba, muombaji (Lulu) awasilishe hati zake zote za kusafiria kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, asisafiri nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila ya idhini ya msajili, kuripoti kwa msajili kila tarehe moja ya kila mwezi tangu atakapotimiza masharti hadi shauri litakapomalizika.

Masharti mengine ni Lulu awe na wadhamini wawili watakaotia saini bondi ya sh. milioni 20 kila mmoja na wawe wafanyakazi wa serikali na Msajili wa Mahakama Kuu wa Kanda hiyo, atahakiki masharti hayo ya dhamana kama yametimizwa

YANGA, PRISONS ZAINGIZA MIL 101/-



MCHEZO wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na Prisons uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, umeingiza sh. 101,016,000.

Katika mchezo huo, jumla ya watazamaji 17,946 walikata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema jana kuwa, watazamaji 16,158 walikata tiketi za sh. 5,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ni 98 waliokata tiketi za sh. 20,000.

Wambura alisema kutokana na mapato hayo, kila klabu imepata mgawo wa sh. 24,314,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 15,409,220.34.

Alisema asilimia 15 iliyokwenda kwenye uwanja baada ya kuondoa VAT ni sh. 12,363,433.45 na mgawo mwingine wa mapato hayo ni gharama za tiketi sh. 3,183,890.

Alisema gharama za mchezo ni sh. 7,413,060.07, Kamati ya Ligi sh. 7,418,060.07, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,709,030.03 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,884,801.14.

CAPE VERDE YAONYESHA MAAJABU



PORT ELIZABETH, Afrika Kusini

HUWEZI kuamini, lakini ndivyo ilivyokuwa. Cape Verde juzi ilionyesha maajabu baada ya kuichapa Angola mabao 2-1 na kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Katika mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa mjini hapa, Angola ilikuwa ikihitaji ushindi ili iweze kufuzu kucheza hatua hiyo na ilikuwa ya kwanza kupata bao.

Mlinzi Neves wa Cape Verde ndiye aliyeizawadia bao Angola dakika ya 33 baada ya kujifunga wakati akiwa kwenye harakati za kuokoa mpira wa hatari uliopigwa kwenye lango la timu yake. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Cape Verde ilisawazisha dakika tisa kabla ya mchezo kumalizika kwa bao lililofungwa na beki, Fernando Varela kwa shuti la umbali wa mita zipatazo 17.

Wakati mashabiki wakiamini kuwa pambano hilo lingemalizika kwa sare, Heldon aliifungia Cape Verde bao la pili na la ushindi na kuwafanya wachezaji na viongozi wa timu hiyo wapagawe kwa ushindi.

Angola ililianza pambano hilo kwa kasi, kuliko ilivyokuwa katika mechi zake mbili za awali wakati Cape Verde ilifanya mashambulizi ya kushtukiza.

Cape Verde ilipata nafasi mbili nzuri za kufunga mabao katika kipindi cha kwanza, lakini zilipotezwa na Platini na Ryan Mendes.

Mshambuliaji Manucho alikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Cape Verde, ambao walilazimika kumwekea ulinzi mkali ili asilete madhara kwenye lango lao.

Kocha Luis Antunes wa Cape Verde alisema baada ya mchezo huo kuwa, wanawazawadia ushindi huo wananchi wa visiwa vya Cape Verde.

"Lengo letu katika michuano hii limetimia. Tulitaka kufuzu kucheza robo fainali,"alisema.

Kocha Gustavo Ferrin alisema walilazimika kucheza kwa kushambulia kwa lengo la kuongeza mabao na kusahau kujilinda.

BAFANA BAFANA YATINGA ROBO FAINALI




DURBAN, Afrika Kusini

WENYEJI Afrika Kusini, maarufu kwa jina la Bafana Bafana, juzi walifuzu kucheza robo fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Morocco.

Sare hiyo iliiwezesha Bafana Bafana kutwaa uongozi wa kundi A ikiwa na pointi tano baada ya kucheza mechi tatu, sawa na Cape Verde, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Morocco, ambayo ilitakiwa kushinda pambano hilo ili isonge mbele, iliweza kuwa mbele kwa mabao mara mbili, lakini mara zote Bafana Bafana ilisawazisha.

Issam El Adoua aliifungia Morocco bao la kuongoza dakika ya 10 baada ya kioa Itumeleleng Khune wa Bafana Bafana kuokoa vibaya mpira wa kona, ukamkuta mfungaji aliyeunganisha wavuni. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

May Mahlangu aliisawazishia Bafana Bafana dakika ya 71 na kuamsha shamra shamra kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo.

Mehdi Namli aliiongezea Morocco bao la pili dakika ya 81 kabla ya Siyabonga Sangweni kuisawazishia Bafana Bafana dakika ya 87 na kuufanya uwanja ulipuke kwa mayowe ya kushangilia.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bafana Bafana kufuzu kucheza hatua hiyo tangu mwaka 2002 na itabaki mjini Durban kumsubiri mshindi wa pili wa kundi B.

Kutokana na sare hiyo, Morocco imeungana na Angola kufungasha virago kutoka katika kundi hilo, ikiwa ni mara yake ya pili mfululizo kuishia hatua hiyo katika fainali za kombe hilo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Gordon Igesund wa Bafana Bafana alisema wanaona fahari kutimiza lengo lao la kwanza la kufuzu kucheza hatua ya mtoano.

"Morocco ilikuwa timu ngumu. Sitaki kutaja makosa, lakini tuliweza kusawazisha mabao mawili. Sasa imesalia michezo miwili kufuzu kucheza fainali na nina imani na wachezaji wangu,"alisema.

Kocha Rachid Taoussi wa Morocco alisema amekatishwa tamaa na matokeo hayo, lakini wachezaji wake walipambana kadri ya uwezo wao.

Sunday, January 27, 2013

TEGETE AIPAISHA YANGA





MSHAMBULIAJI Jerry Tegete jana aliwadhihirishia mashabiki wa Yanga kwamba amerejesha makali yake baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu ilipomenyana na Prisons ya Mbeya.

Katika pambano hilo la ligi kuu ya Tanzania Bara lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliinyuka Prisons mabao 3-1.

Tegete alianza kuwainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya 10 baada ya kuifungia bao la kwanza, akimalizia krosi maridhawa kutoka kwa Simon Msuva.

Mshambuliaji huyo, aliyeonekana amekwisha wakati wa mechi za mzunguko wa kwanza, aliwainua tena vitini mashabiki wa Yanga dakika ya 66 baada ya kuifungia la tatu. Alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi kutoka kwa Nurdin Bakari.

Bao la pili la Yanga lilifungwa na Mbuyu Twite dakika ya 57 baada ya kumalizia pasi ya Didier Kavumbagu, aliyegongeana vyema na Niyonzima. Twite alishangilia bao hilo kwa kubusu logo ya Yanga.

Prisons ilipata bao la kujifariji dakika ya 17, mfungaji akiwa Elias Maguri baada ya kumzidi maarifa Haruna Niyonzima wa Yanga, aliyedhani ameotea.

Maguri nusura aiongezee bao Prisons dakika ya 20 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Misango Magai, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Ally Mustapha.

Tegete angeweza kufunga bao lingine dakika ya 40 baada ya kutengenezewa pasi safi na Msuva, lakini alichelewa kuupata mpira, kipa David Abdalla wa Prisons alitokea na kuondosha hatari. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Kabla ya Tegete kufunga bao la tatu, mlemavu mmoja alitaka kuingia ndani ya uwanja, lakini polisi walimzuia.

Kutokana na ushindi huo, Yanga inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 14, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 27 na Simba yenye pointi 26.

Yanga: Ally Mustapha 'Barthez', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kevin Yondan, Athumani Iddi 'Chuji', Simon Msuva, Nurdin Bakari, Didier Kavumbagu/Hamisi Kiiza, Jerry Tegete, Haruna Niyonzima.
Prisons: David Abdalla, Aziz Sibo, Henry Mwalugala, Lugano Mwangama, Jumanne Elfadhili, Nurdin Issa, Sino Augustino, Fred Chugu, Elias Maguri,Misango Magai na Jeremiah Juma.

KOCHA SIMBA ALALAMIKIA KIWANGO




LICHA ya Simba kuanza vyema mzunguko wa pili wa michuano ya soka ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa timu hiyo Mfaransa, Patrick Leiwig, amesema hajaridhishwa na kiwango cha timu yake.

Simba ilianza mzunguko huo juzi kwa kuifunga African Lyon mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya pambano hilo, Leiwig alisema licha ya Simba kushinda mchezo huo, kiwango hakikuwa cha kuridhisha.

Kocha huyo alisema anataka kuona kiwango cha Simba kikiwa juu zaidi katika mechi zijazo kwa timu kucheza kwa kujituma zaidi.

Leiwig, ambaye juzi ilikuwa mara yake ya kwanza kuishuhudia Simba ikicheza katika ligi, pia alieleza kutoridhishwa na hali ya hewa ya Dar es Salaam hivi sasa, ambayo alilalamika kuwa joto ni kali mno.

Alisema baridi iliyokuwepo Oman, ambako timu hiyo ilikwenda kuweka kambi ya wiki mbili, imewaathiri wachezaji wake, ambao sasa wanacheza mashindano katika mji wenye joto.

Kocha huyo alisema hali ya hewa ya Oman ilikuwa digrii 22 na kuongeza kuwa, itachukua muda kidogo kwa wachezaji kuzoea kucheza katika mazingira ya joto.

Leiwig aliwataka mashabiki wa Simba wasivunjike nguvu kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake juzi, badala yake wajiandae kuona soka ya kiwango cha juu katika mechi zijazo.

Simba inatarajiwa kushuka tena dimbani Februari 3 mwaka huu kumenyana na JKT Ruvu mjini Dar es Salaam kabla ya kumenyana na JKT Oljoro katika mechi itakayopigwa Februari 9 mjini Arusha.

MALINZI, NYAMLANI, MANJI WAWEKEWA PINGAMIZI TFF



WAGOMBEA wa nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athumani Nyamlani na Jamal Malinzi, wamewekewa pingamizi la kugombea nafasi hiyo.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Nyamlani amewekewa pingamizi mbili na Mtanga Yussuf na Menard Justine wakati Malinzi amewekewa pingamizi moja na Agape Fuwe.

Angetile alisema kamati ya uchaguzi imepokea pingamizi 14 za wagombea wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa TFF unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu.

Aliwataja wagombea wengine waliowekewa pingamizi kuwa ni Michael Wambura, anayewania nafasi ya makamu wa rais, ambaye amewekewa pingamizi mbili na Osiah Samuel na Saidi Rubeya.

Kwa mujibu wa Angetile, wagombea wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji waliowekewa pingamizi ni Epatha Swai, aliyewekewa pingamizi mbili na Ramadhan Sesso na Sos Chalamila, Eliud Mvella amepingwa na Saidi Kiponza, Abdul Changawa na Peter Namengi wakati Athumani Kambi amepingwa na Jeremiah Wambura.

Kwa upande wa Bodi ya Ligi, Angetile alisema wagombea wa nafasi ya mwenyekiti, Yussuf Manji na Ahmad Yahya wamewekewa pingamizi mbili kila mmoja.

Alisema Manji amewekewa pingamizi na mwanachama maarufu wa Simba, Daniel Kamna na mwanachama wa Yanga, Juma Magoma wakati Yahya amewekewa pingamizi na Frank Mchaki na Mohamed Saidi.

Angetile alisema kamati ya uchaguzi ya TFF inatarajiwa kukutana keshokutwa kujadili pingamizi hizo kabla ya kutangaza majina ya wagombea, watakaopitishwa katika uchaguzi huo.

VITUKO VYA MASHABIKI AFCON 2013



ADEBAYOR AIBEBA TOGO



RUSTENBURG, Afrika Kusini

MSHAMBULIAJI Emmanuel Adebayor juzi aliifungia Togo bao moja kati ya mawili, ilipoichapa Algeria mabao 2-0 katika mechi ya kundi D ya michuano ya soka ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika iliyochezwa mjini hapa.

Matokeo hayo yamefufua matumaini ya Togo kufuzu kucheza robo fainali baada ya kuwa na pointi tatu katika mechi mbili ilizocheza, sawa na Tunisia. Algeria inashika mkia katika kundi hilo.

Togo sasa itacheza mechi yake ya mwisho Januari 31 kwa kupambana na Tunisia na timu yoyote itakayoshinda, itafuzu kucheza robo fainali.

Adebayor aliifungia Togo bao la kuongoza dakika ya 32 kwa shuti la mguu wa kulia lililotinga moja kwa moja wavuni.

Dove Wome aliiongezea Togo bao la pili dakika za majeruhi baada ya kupokea pasi kutoka pembeni ya uwanja, akaingia na mpira ndani ya 18 kabla ya kufumua shuti lililotinga wavuni..

Mechi hiyo ililazimika kusimama kwa dakika 15 ilipotimia dakika ya 86 baada ya mwamba wa goli kupata mushkeli. Maofisa 10 walilazimika kuingia ndani ya uwanja kusimamia utegenezaji wa goli hilo.

"Ilikuwa moja ya mechi ngumu tulizocheza hadi sasa, tulipambana na timu nzuri ya Algeria,"alisema Kocha Didier Six wa Togo.

"Tulikuwa tumedhamiria kushinda na tulistahili kupata ushindi,"aliongeza kocha huyo.

Naye Adebayor alisema amefurahishwa na ushindi huo na kuongeza kuwa, ilikuwa lazima washinde ili kufufua matumaini.

IVORY COAST YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA



RUSTENBURG, Afrika Kusini

IVORY Coast juzi ilifuzu kucheza robo fainali ya michuano ya soka ya fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kuicharaza Tunisia mabao 3-0 katika mechi ya kundi D iliyochezwa mjini hapa.

Ushindi huo umeiwezesha Ivory Coast kuwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili, ikifuatiwa na Tunisia na Togo zenye pointi tatu kila moja. Algeria inashika mkia kwa kutoambulia pointi.

Ivory Coast itahitimisha mechi zake Januari 30 kwa kumenyana na Algeria wakati Togo itakipiga na Tunisia.

Iliwachukua Ivory Coast dakika 21 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Gervinho baada ya gonga safi kati yake na Lacina. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Bao la pili la Ivory Coast lilifungwa na Yaya Toure dakika ya 87 kwa shuti kali la mbali lililotinga moja kwa moja wavuni.

Didier Ya Konan, aliyeingia kipindi cha pili, aliihakikishia ushindi Ivory Coast dakika ya 90 baada ya kuifungia bao la tatu.

Mshambuliaji Didier Drogba, ambaye alionyesha kiwango duni katika mechi ya ufunguzi, aliingia uwanjani dakika ya 67, lakini alishindwa kuonyesha cheche zake.

Katika mechi hiyo, Ivory Coast ilitawala sehemu kubwa ya mchezo na kuonyesha kiwango tofauti na ilivyocheza na Togo.

Tunisia ilifanya shambulizi kubwa dakika ya 84 wakati Saber Khalifa alipoingia na mpira ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Boubacar Barry wa Ivory Coast.

Ivory Coast haijawahi kutwaa kombe la Mataifa ya Afrika tangu 1992. Mwaka jana ilishika nafasi ya pili baada ya kufungwa na Zambia kwa penalti katika mechi ya fainali.

VICTORIA ATWAA TAJI LA AUSTRALIA OPEN



MELBOURNE, Australia

VICTORIA Azarenka wa Belarus jana alifanikiwa kutetea taji lake la ubingwa wa michuano ya wazi ya tennis ya Australia kwa wanawake baada ya kumbwaga Li Na wa China.

Katika mechi hiyo ya fainali, iliyokuwa na msisimko wa aina yake, Victoria alimshinda Li Na kwa seti 2-1.

Li Na aliianza seti ya kwanza kwa kishindo na kumbwaga Victoria kwa 6-4. Lakini mwanadada huyo wa Belarus alichachamaa katika seti mbili zilizofuata na kushinda kwa 6-4, 6-3.

Kabla ya mchezo huo, Victoria alikuwa hapewi nafasi kubwa ya kutwaa tena taji hilo.

Baadhi ya magazeti ya Australia na hata wasomaji wake, walikuwa wakitoa nafasi kubwa kwa Li Na kuibuka mshindi kutokana na uwezo aliouonyesha katika mechi za hatua ya awali.

Mara baada ya pambano hilo kumalizika, Victoria alijikuta akikaa kwenye kiti uwanjani na kuanza kuangua kilio. Alilazimika kutumia taulo kufuta machozi yake.

Victoria ndiye mchezaji namba moja duniani kwa sasa katika mchezo huo kwa wanawake.

"Nilikuwa na wakati mgumu na sasa najisikia ahueni na mwenye furaha kubwa,"alisema Victoria.

MUUMIN, SONYO, GEORGE GAMA WAIBUKIA VICTORIA SOUND



NA RASHID MUSSA, MTWARA

UNAPOWAZUNGUMZIA wanamuziki wenye tabia ya kuhamahama kutoka bendi moja hadi nyingine hapa nchini, bila shaka jina la Muumin Mwinjuma haliwezi kukosekana. Kama ni orodha ya wanamuziki 10 wanaoongoza kwa tabia hiyo, jina la Mwinjuma lazima liwemo.

Ni mwanamuziki aliyepitia bendi nyingi hapa nchini na hata katika nchi jirani ya Kenya. Aliwahi kupiga muziki katika bendi za Mchinga Sound, Double M Sound na Bwagamoyo Sound, ambazo alikuwa akiziongoza na Twanga Pepeta International.

Na sasa ameanzisha bendi nyingine mpya inayojulikana kwa jina la Victoria Sound, ambayo imeweka kambi mkoani Mtwara, ikiandaa nyimbo mpya. Lengo la Muumin ni kuifanya bendi hiyo itishe.

Katika maisha yake kimuziki, Muumin amewahi kutunga nyimbo nyingi zilizompatia sifa na umaarufu mkubwa. Lakini vibao vya Mgumba namba moja na namba mbili na Kilio cha Yatima ndivyo alivyoviimba akiwa Double M Sound ndivyo vitakavyobaki kwenye kumbukumbu ya mashabiki wa muziki kwa muda mrefu ujao.

Sifa kubwa ya Muumin katika muziki ni sauti yake maridhawa. Wapo baadhi ya waimbaji wenye sifa na uwezo wa kuiga sauti za wanamuziki mbalimbali maarufu, lakini kuiga sauti ya Muumin kunahitaji sifa ya ziada.

Ndio sababu siku alipoondoka Mchinga Sound, wanamuziki wa bendi hiyo pamoja na mmiliki wake waliona wazi kuwa, ulikuwa mwisho wao. Walipatwa na hisia hiyo kwa sababu Muumin aliimba karibu nyimbo zote za bendi hiyo na hakukuwa na mwenye uwezo wa kuiga sauti yake.

Je, ni kwa nini Muumin ameamua kujiengua katika bendi ya Twanga Pepeta International na kuanzisha bendi mpya ya Victoria Sound? Je, bendi hii itaweza kudumu kwa muda mrefu? Mbona aliwahi kuanzisha Bwagamoyo Sound lakini ikafa?

Maswali hayo na mengineyo kadhaa ndiyo yaliyonishawishi nimtafute Muumin baada ya kupata taarifa kwamba yupo Mtwara, akiwa amejichimbia na bendi yake hiyo ya Victoria Sound.

Akizungumza na Uhuru mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa, Muumin alisema kuhama kutoka bendi moja hadi nyingine ni jambo, ambalo haliwezi kuzuilika kwa mwanamuziki, lengo likiwa ni kutafuta malisho mazuri.

Muumin alisema inawezekana wapo baadhi ya wanamuziki wanaohama bendi kwa malengo mengine, lakini kwake siku zote amekuwa akitafuta malisho mazuri na pia kuinua vipaji vya wengine.

Hata hivyo, mwimbaji huyo mkongwe hakutaka kuzungumzia kiundani kuhusu suala hilo la kuhamahama kutoka bendi moja hadi nyingine kwa madai kuwa, majibu aliyoyatoa yanatosha.

Lakini alitamba kuwa, ana hakika bendi hiyo itadumu kwa muda mrefu kutokana na kujiimarisha katika kila idara na pia kuundwa na wanamuziki wengi wenye vipaji vya muziki.

Alisema uamuzi wao wa kuweka kambi Mtwara ulilenga kuwapa muda wa kutosha wa kutunga nyimbo mpya na kuzifanyia mazoezi kabla ya kuanza rasmi maonyesho yao kwenye kumbi mbalimbali za burudani.

Muumin alisema bendi ya Victoria Sound sio mpya kwa sababu ilianzishwa miaka sita iliyopita. Alisema kilichofanyika ni kuisuka upya.

"Tumekuja hapa Mtwara tangu mwishoni mwa mwaka jana na lengo letu kubwa la kuweka kambi hapa ni kutafuta utulivu, utakaotuwezesha kufanyakazi yetu kwa umakini mkubwa,"alisema mwimbaji huyo.

Alisema kambi yao imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kupata ushirikiano mzuri na huduma nzuri kutoka kwa wenyeji wao. Alisema tangu walipoanza kambi, wamekuwa wakifanya mazoezi saa nane kwa siku.

Muumin alisema tayari wameshatunga vibao vipya vinne na walianza kuwaonjesha uhondo wake wakazi wa Mtwara mwishoni mwa wiki iliyopita katika onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa klabu ya Bandari.

Alivitaja vibao hivyo vipya kuwa ni Shamba la Bibi na Utafiti wa mapenzi, alivyovitunga yeye mwenyewe. Aliviita vibao hivyo kuwa ni moto wa kuotea mbali.

Vibao vingine ni Mama Bahati, kilichotungwa na mpiga gita la rythm, Yohana Mbatizaji na Mwisho wa siku, kilichotungwa na Waziri Sonyo.

"Kwa watakaovisikia vibao hivyo kwa mara ya kwanza, wataelewa ni kwa nini tuliamua kuja kuweka kambi Bagamoyo kwa sababu si vya mchezo,"alisema Muumin.

Baada ya onyesho hilo la Mtwara, bendi hiyo ilitarajia kuwapa burudani wakazi wa mkoa wa Lindi kabla ya kurejea Dar es Salaam. Makao makuu ya bendi hiyo yapo Mbagala-Kiburugwa.

Kwa mujibu wa Muumin, mara baada ya bendi hiyo kurejea Dar es Salaam, itakwenda moja kwa moja studio kwa ajili ya kurekodi nyimbo hizo nne. Alisema wanataka kurekodi albamu, itakayokuwa na nyimbo saba.

Muumin amewataka mashabiki wa muziki nchini kujiandaa kupata burudani ya aina yake kutoka katika bendi hiyo, ambayo alijigamba kuwa, wapinzani wao wakubwa watakuwa Twanga Pepeta na FM Academia.

Mbali na Muumin, Sonyo na Yohana, wanamuziki wengine wanaounda bendi hiyo ni Selemani Mumba, anayepiga gita la solo na Moshi Hamisi, anayepiga kinanda.

Wengine ni George Gama, anayepiga magita yote matatu, Januari Joseph, Ciana Jordan, Ramso Bushoke, Jonas Mlembuka na Mussa Kalenga, ambao ni waimbaji.

Wanamuziki wengine wanaounda bendi hiyo ni Kassim Mumba, anayepiga gita la besi, Abdalla Hussein anayepiga kinanda na Vaninga Swalehe,anayepiga tumba.

Bendi hiyo inakamilishwa na wacheza shoo, Omari Mussa 'Bokilo', Joha Juma, Mariam Othaman, Farida Omari, Lilian Wayanga, Nadia Benjamin na Sophia Ramadhani.

SIMBA, LYON ZAINGIZA MIL 53/-



MCHEZO wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, uliozikutanisha timu za Simba na African Lyon umeingiza sh. 53,756,000.

Katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, jumla ya watazamaji 9,408 walikata tiketi na kushuhudia mchezo huo, ambapo Simba ilishinda mabao 3-1.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema jana kuwa, kutokana na mapato hayo kila klabu ilipata mgawo wa sh. 12,499,752.45.

Wambura alisema mgawo mwingine ulikuwa wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), iliyolipwa sh. 8,200,067.80, wakati asilimia 15 ya uwanja ni sh.6,355,806.33.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni gharama za tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 3,813,483.80, Kamati ya Ligi sh. 3,813,483.80, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF), sh. 1,906,741.90 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,483,021.48.

Viingilio katika mchezo huo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Saturday, January 26, 2013

SIMBA, AZAM, COASTAL UNION ZAUA



MABINGWA watetezi Simba leo wameuanza vyema mzunguko wa pili wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuichapa African Lyon mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika pambano hilo, Simba ingeweza kutoka uwanjani na ushindi mkubwa wa mabao iwapo mshambuliaji wake, Mrisho Ngasa angekuwa makini kila alipolifikia lango la African Lyon.

Ngasa pia alipoteza penalti katika kipindi cha pili baada ya shuti lake kumlenga kipa Abdul Seif. Hadi mapumziko, Simba ilikuwa mbele kwa mabao 3-0.

Mabao ya Simba katika kipindi hicho cha kwanza yalifungwa na Mrisho Ngasa, aliyefunga mawili na Ramadhani Chombo 'Redondo'.

Redondo, aliyerejea Simba akitokea Azam, alifunga bao la kwanza dakika ya tatu baada ya kuunganisha wavuni mpira wa krosi uliopigwa na Ngasa kutoka pembeni ya uwanja na kuamsha shangwe kutoka kwa mashabiki wa Simba.

Bao la pili lilifungwa na Ngasa baada ya gonga safi kati yake na Mwinyi Kazimoto kabla ya kufumua shuti lililompita kipa Seif wa African Lyon.

Lyon ingeweza kupunguza tofauti ya mabao dakika ya 31 wakati ilipopata adhabu ya penalti baada ya beki Paul Ngelema wa Simba kumwangusha Fred Lewis ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, shuti la kwanza la Shamte Ally liliokolewa na kipa Juma Kaseja wa Simba, lakini mwamuzi Israel Mujuni aliamuru penalti hiyo irudiwe. Na iliporudiwa, shuti la Shamte lilitoka pembeni ya lango.

Ngasa aliifungia Simba bao la tatu baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Haruna Chanongo, aliyepandishwa kutoka kikosi cha pili, ambaye alionyesha kila dalili za kuweza kuziba vyema pengo la Emmanuel Okwi, aliyeuzwa kwa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.

Lyon ilibadili sura ya mchezo katika kipindi cha pili, ambapo ilicheza gonga safi na kutoa usumbufu mkubwa kwa mabeki na viungo wa Simba, ambao walikuwa wakiutafuta mpira kwa toshi.

Mashambulizi hayo ya Lyon yalizaa matunda dakika ya 59 baada ya kupata bao la kujifariki kupitia kwa Bright Ike baada ya kupokea pasi kutoka kwa Fred.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa leo, Mtibwa Sugar ilichapwa bao 1-0 na ndugu zao wa Polisi kwenye uwanja wa Manungu. Bao pekee na la ushindi la Polisi lilifungwa na Muzamil Saidi.

Katika mechi zingine, Coastal Union iliwacharaza ndugu zao wa Mgambo JKT mabao 3-1, Ruvu Shooting waliwalaza ndugu zao wa JKT Ruvu bao 1-0, Azam iliinyuka Kagera Sugar mabao 3-1 wakati JKT Oljoro iliibamiza Toto Africans mabao 3-1.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo wakati Yanga itakapomenyana na Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Friday, January 25, 2013

SERIKALI YAPUNGUZA MAKATO U/TAIFA, TRA KUREJESHA FEDHA ZA TFF



SERIKALI imekubali kupunguza makato mbalimbali yanayotolewa wakati wa mechi za michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara na Kimataifa.


Uamuzi huo umetangazwa leo na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla alipokuzungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam.

Makalla alisema kuanzia sasa, serikali itakuwa ikichukua asilimia 15 ya mapato yanayopatikana katika mechi hizo, hasa zinazochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ili kuzipunguzia gharama klabu.

Alisema baada ya serikali kupata asilimia hiyo ya mapato, hakutakuwa na asilimia zingine zitakazokatwa zaidi ya gharama za tiketi.

Aliwashuru viongozi wa klabu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na waandishi wa habari kwa kusimama kidete kulisimamia jambo hilo kwa vile ni kweli klabu zilikuwa zikiachiwa mzigo mkubwa wa gharama.

Makalla alisema pia kuwa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekubali kurejesha fedha ilizochokua kutoka kwenye akaunti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya nauli za klabu.

Fedha hizo, sh. milioni 150 zilitolewa na wadhamini wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kwa ajili ya nauli kwa timu zinazoshiriki mzunguko wa pili wa ligi hiyo.

Awali, klabu za ligi hiyo pamoja na kamati ya ligi, zilitishia kususia kucheza mechi za mzunguko huo iwapo TRA isingerejesha fedha hizo.

Hata hivyo, Makalla amezitaka klabu kuwa na subira kwa vile utaratibu wa kurejesha fedha hizo hauwezi kufanyika kwa siku moja. Alisema utaratibu huo unaweza kuchukua muda kidogo, lakini lazima fedha hizo zirejeshwe.

ZFA YAMKATALIA MAKUNGU KUJIUZULU



Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kimeikataa barua ya maombi ya kujiuzulu iliyowasilishwa na Rais wa chama hicho, Amani Makungu.

Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya ZFA kilichofanyika juzi mjini hapa.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa, wajumbe wa kamati ya utendaji ya ZFA wamemkatalia Makungu kujiuzulu kwa vile sababu alizozitoa hazijitoshelezi.

Katika barua yake ya kutaka kujiuzulu, Makungu amedai kuwa, amefikia uamuzi huo kutokana na kushindwa kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wa chama hicho wa kanda ya Unguja.

Rais huyo wa ZFA amedai kuwa, alipokuwa ziarani Pemba hivi karibuni, hakupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa makamu wake wa Pemba, badala yake alipokewa na viongozi wa chama cha wilaya ya Chakechake.

Aliitaja sababu nyingine iliyomfanya afikie uamuzi wa kujiuzulu kuwa ni viongozi wa ZFA kanda ya Unguja kufanya mambo yao bila kuushirikisha uongozi wa kitaifa na wakati mwingine kuanzisha ligi ya kanda hiyo wanavyotaka wao.

Hata hivyo, wakati wa kikao hicho, wajumbe waliamua kuwa, uamuzi wa Makungu kujiuzulu si sahihi kwa sababu badala ya kutatua matatizo ameamua kuyakimbia.

Katika kikao hicho, wajumbe pia waliona kuwa, Makungu amefanya mambo mengi mazuri tangu alipoingia madarakani ZFA na hivyo yanapaswa kuendelezwa.

Wajumbe waliitaja sababu nyingine ya kupinga uamuzi huo wa Makungu kuwa, usimamizi wa timu ya Zanzibar kwa michuano ya kimataifa kwa sasa umekuwa mzuri na wa kiwango cha juu tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

"Katika mazingira haya, wajumbe wameona kuwa si busara kwa Makungu kuamua kujiuzulu wakati huu, badala yake ashirikiane na wajumbe wenzake kuyatatua matatizo hayo na baada ya hapo ndipo anaweza kujiuzulu," alisema mjumbe mmoja aliyehudhuria kikao hicho.

Thursday, January 24, 2013

MAOMBI YA DHAMANA YA LULU J'TATU



MAOMBI ya dhamana ya msanii wa maigizo nchini, Elizabeth Michael 'Lulu', anayesota rumande kutokana na kukabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia, yamepangwa kusikilizwa Jumatatu ijayo.

Lulu anakabiliwa na kosa la kumuua bila kukusudia msanii mwenzake Steven Kanumba.

Taarifa zilizopatika jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, zilieleza kuwa, maombi hayo hayataweza kusikilizwa leo kwa sababu ni sikukuu ya Maulid.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maombi hayo sasa yatasikilizwa Jumatatu
mbele ya Jaji Zainabu Mruke.

Lulu kupitia jopo la mawakili, Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Masawe wanaomtetea, aliwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu kwa kuwa kosa linalomkabili linadhaminika.

Mawakili hao waliwasilisha maombi hayo chini ya hati ya dharura wakiomba yasikilizwe na kuamriwa mapema kwa madai kuwa, Lulu amekaa rumande kwa muda wa miezi saba na kosa lake linadhaminika.

Kwa mujibu wa hati ya maombi iliyoambatanishwa na hati ya kiapo, ambacho muapaji ni wakili Kibatala kwa niaba ya mshtakiwa huyo, wanaiomba Mahakama iamuru mshitakiwa apewe dhamana, akiwa au bila kuwa na wadhamini, au kwa amri na masharti mengineyo ambayo itaona yanafaa.

"Tunaomba Mahakama hii tukufu impe dhamana mshitakiwa akiwa na au bila kuwa na wadhamini, wakati akisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi yake ya msingi, shauri la jinai namba 125 la 2012, lililopo katika mahakama hii tukufu,” ilisema sehemu ya hati ya maombi.

Lulu anadaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, April 7, 2012, nyumbani kwake (Kanumba), Sinza Vatican, Dar es Salaam. Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, umedai kuwa utaita mashahidi tisa wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo.

JK ATETA NA BLATTER



NA MWANDISHI MAALUM, ZURICH

RAIS Jakaya Kikwete amelishukuru Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) kwa kuipatia Tanzania misaada mbalimbali ya kifedha na ufundi.

Kikwete amesema misaada hiyo si tu kwamba imekuwa ikisaidia kuinua kiwango cha soka nchini, bali pia barani Afrika.

Rais Kikwete alitoa shukurani hizo jana baada ya kutembelea makao makuu ya FIFA mjini hapa na kukutana na Rais wa shirikisho hilo, Sepp Blatter.

Kikwete aliwasili Zurich akitokea Ufaransa, ambako alifanya ziara ya kiserikali ya siku tatu.

Rais Kikwete ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu, ambapo anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa dunia kuhusu uchumi, utakaofanyika katika mji wa Davos.

Tanzania ni mwanachama wa FIFA kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

FIFA imekuwa ikitoa dola 250,000 za Marekani kila mwaka kwa nchi wanachama kwa ajili ya kuendeleza soka na dola zingine milioni 2.5 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Shirikisho hilo pia limekuwa likitoa dola 400,000 kila baada ya miaka minne kwa kila mwanachama kwa ajili ya malengo ya muda mrefu ya kuendeleza soka.

MALINZI, NYAMLANI WANDALIWA MDAHALO

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeandaa mdahalo kwa ajili ya wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mdahalo huo umepangwa kufanyika Februari 15 mwaka huu.

Mhando alisema uamuzi wa kuendesha mdahalo huo ulifikiwa wakati wa kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kilichofanyika jana, ambapo pamoja na mambo mengine, kilijadili masuala mbalimbali.

"Kikao kimeiagiza sekreterieti ya TASWA ifanye maandalizi ya mdahalo huo kwa kuzungumza na vituo vya televisheni ili uweze kuonyeshwa moja kwa moja kwenye vituo hivyo ili wananchi waweze kuwasikiliza wagombea,"alisema.

Mhando alisema mazungumzo ya awali na wadhamini mbalimbali yameanza kwa ajili ya kufanikisha tukio hilo la kuendesha mdahalo huo laivu kwenye televisheni. Alisema nafasi ambazo wahusika watafanyiwa mdahalo ni ya rais na makamu wa rais.

TASWA ilianza kufanya midahalo kwa wagombea wa nafasi za juu katika uchaguzi wa TFF kuanzia 2001 na 2004. Mdahalo wa kwanza kuonyeshwa laivu ulikuwa wa 2008.

Kwa mujibu wa Mhando, chama chake kitawasiliana na uongozi wa juu wa TFF ili kiweze kutoa msaada wa kufanikisha mdahalo huo.

"Tunaamini ushirikiano uliopo kati ya TFF na TASWA utasaidia kwa namna fulani kufanikisha jambo hilo na mdahalo huo utahusisha waandishi wa habari waandamizi wa michezo, wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari vya michezo na wadau wachache wa soka,"alisema.

Mhando alisema tayari Kamati ya Utendaji ya TASWA imemteua mwandishi wa habari mkongwe, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Redio ABM, Abdallah Majura kuwa mwendeshaji wa mdahalo huo kutokana na uzoefu wake katika masuala ya habari na mambo ya michezo.

Katibu Mkuu huyo alisema chama chake hakiungi mkono mgombea yeyote na haina mpango wa kumuunga mkono mgombea yeyote.

"TASWA inaonya kuwa, kama kuna baadhi ya wagombea wenye ndoto za kutaka kutumia mgongo wa TASWA ili wapate mteremko kufikia malengo yao, hazitatimia,"alisema Mhando.

Amewataka waandishi wa habari za michezo nchini kuzidisha umakini katika kipindi hiki cha uchaguzi wa TFF na kujiepusha na makundi ya aina yoyote, ambayo yatatia doa taaluma ya habari.

KAMATI YA RUFANI TFF YAAHIDI KUTENDA HAKI



KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imewaahidi wadau wa mchezo huo kuwa, itafanyakazi zake kwa misingi ya haki.

Mwenyekiti wa kamati hiyo yenye wajumbe watano, Idd Mtiginjola amesema wapo kwa ajili ya kutenda haki kwa watu wote.

Mtiginjola alisema hayo juzi baada ya uzinduzi wa kamati hiyo, uliofanywa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kwa niaba ya rais wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga.

Mwenyekiti huyo alisema, kamati yao inaundwa na watu waadilifu, hivyo watafanya kazi kwa kuzingatia kanuni zilizopo na sheria nyingine za mpira wa miguu, ikiwemo Katiba husika.

“Niwakikishie kuwa, hatutafanya uamuzi kutokana na mawazo yetu, tufanya uamuzi kwa kuzingatia kanuni na sheria. Kamati hii ni chombo cha haki, hivyo itafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria. Sheria na haki ni vitu viwili tofauti. Sheria zipo kwa ajili ya kuitafuta haki,” alisema Mtiginjola, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, akiwa Wakili wa Kujitegemea.

Baada ya uzinduzi huo, Osiah aliwakabidhi wajumbe wa kamati hiyo vitendea kazi (instruments) mbalimbali, zikiwemo kanuni za uchaguzi za TFF na wanachama wake, katiba ya TFF na katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Mbali ya Mtiginjola, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Makamu Mwenyekiti, Francis Kabwe, ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mohamed Mpinga, ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria.

Wajumbe wengine ni mshambuliaji wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo, ambaye kwa sasa ni Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini Morogoro, na mdau wa soka Murtaza Mangungu, ambaye ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini.

TBL YAMWAGA VIFAA VYA MICHEZO KWA SIMBA NA YANGA



KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) imezipatia klabu za Simba na Yanga vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. milioni 70.

Vifaa hivyo vyenye nembo ya bia ya Kilimanjaro, ni kwa ajili ya mzunguko wa pili wa michuano ya soka ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika mjini Dar es Salaam jana kuwa, kila klabu imepata vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 35.

Kavishe alisema kampuni yake imekuwa ikizipatia klabu hizo vifaa vipya vya michezo kila zinapokabiliwa na michuano mbalimbali na kwamba wanafurahi kuona zinautumia vizuri udhamini wao.

Alivitaja vifaa vilivyotolewa kwa klabu hizo kuwa ni mipira, viatu vya mazoezi na vya kuchezea mechi, vikinga ugoko, jezi za mazoezi na za kuchezea mechi.

Mzunguko wa pili wa ligi hiyo unatarajiwa kuanza kesho katika viwanja saba tofauti, ambapo Simba itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na African Lyon.

Yanga itaanza mzunguko huo keshokutwa kwa kucheza na Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akipokea vifaa hivyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema, wanaishukuru TBL kwa kuendelea kuifadhili timu yao.

Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga aliishukuru kampuni hiyo na kusema kuwa, ufadhili huo unasaidia kuifanya timu yao kushiriki vyema katika ligi hiyo.

FLAVIANA AWA MWANAMITINDO BORA AFRIKA 2012



MREMBO na mwanamitindo nyota wa Tanzania, Flaviana Matata ameendelea kung’ara kimataifa baada ya kushinda tuzo ya 'Nigeria’s Next Super Model'.

Flaviana alishinda tuzo hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Lagos, Nigeria na kuwa mwanamitindo bora wa Afrika 2012 (Africa’s Most Outstanding Model 2012).

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Compass Communication Tanzania Limited, Maria Sarungi Tsehai alisema jana kuwa, ushindi huo wa Flaviana ni sifa na changamoto kwa wanamitindo wa Tanzania wanaochipukia.

Maria alisema amejisikia faraja kubwa kutokana na mafanikio hayo ya Flaviana kwa sababu yeye ndiye aliyemvumbua mwanamitindo huyo, ambaye kwa sasa anashika chati ya juu nje ya nchi.

Aliongeza kuwa, Flaviana amedhihirisha ubora wake na mpaka sasa kiwango chake cha kuitangaza Tanzania kimataifa ni ndoto aliyokuwa nayo kwa muda mrefu.

Tuzo aliyopata mwanamitindo huyo hutolewa kwa wanamitindo, ambao bado wanailetea sifa Afrika kimataifa. Flaviana amekuwa katika chati ya juu, ambapo Desemba mwaka jana, alishinda tuzo ya mwanamitindo bora kutoka kwa diaspora ya Waafrika.

Flaviana kwa sasa anaishi na kufanya kazi ya uanamitindo mjini New York nchini Marekani kupitia shirika la Wilhelmina Models.

Mwanamitindo huyo pia anaendesha taasisi yake, inayojulikana kwa jina la Flaviana Matata Foundation, ambayo inasomesha watoto yatima wa kike 16 nchini.

LEIWIG-LIGI ITAKUWA NGUMU



KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Leiwig kutoka Ufaransa amekiri kuwa, mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara utakuwa mgumu kwa vile timu nyingi zimefanya maandalizi mazuri.

Leiwig amesema itakuwa vigumu kwake kutabiri timu ipi itakayoibuka na ubingwa na kusisitiza kuwa, timu yoyote itakayocheza vizuri na kushinda ndiyo inayostahili kuwa bingwa.

“Ligi itakuwa ngumu, siwezi kusema kwa sasa iwapo itakuwa rahisi kwa Simba kutetea taji lake,” alisema.

Kocha huyo alisema hayo jana baada ya kikosi cha Simba kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kikitokea Oman.

Msafara wa timu hiyo uliwasili kwenye uwanja huo saa 11 jioni kwa ndege la Shirika la Oman na kupokewa na baadhi ya viongozi wa timu hiyo, akiwemo Katibu Mkuu, Evodius Mtawala na Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange 'Kaburu'.

Wachezaji wa timu hiyo walitoka nje ya uwanja kwa mafungu, na kukwepa kupigwa picha na waandishi wa habari. Baadhi ya wakati walitoka nje mmoja mmoja na wakati mwingine wawili wawili.

Leiwig alisema ziara yao ya mazoezi nchini Oman imetoa nafasi nzuri kwake na wachezaji kufahamiana na pia kuwafundisha mfumo anaotumia katika kucheza soka.

Kocha huyo alisema mechi tatu walizocheza dhidi ya timu ya Olimpiki, timu ya Taifa ya Jeshi na Ahli Nasab zilimwezesha kujua uwezo wa kila mchezaji na uimara wa timu yake.

Simba ilikwenda moja kwa moja kwenye hoteli ya Sapphire iliyoko Kigamboni, Dar ee Salaam, ambako itaendelea na maandalizi yake kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara uliopangwa kuanza Jumamosi

SIMBA, YANGA DIMBANI MEI 18



WATANI wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga wanatarajiwa kurudiana Mei 18 mwaka huu katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano hilo la watani ni miongoni mwa mechi saba za mwisho za ligi hiyo zitakazochezwa siku hiyo kwenye viwanja tofauti, likiwepo pambano kati ya Azam na JKT Oljoro zitakazomenyana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Simba na Yanga zilipambana kwa mara ya kwanza Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Ratiba ya mechi za mzunguko wa pili wa ligi hiyo, iliyotolewa juzi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inaonyesha kuwa, katika mechi zingine za kufunga pazia, Toto African itamenyana na Ruvu Shooting mjini Mwanza, Mgambo JKT itavaana na African Lyon mjini Tanga, JKT Ruvu itamenyana na Mtibwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, Prisons itavaana na Kagera Sugar mjini Mbeya wakati Polisi Morogoro watakuwa wenyeji wa Coastal Union mjini Morogoro.

Kwa mujibu wa ratiba, mzunguko wa pili wa ligi hiyo unatarajiwa kuanza Jumamosi kwa mechi sita. Katika moja ya mechi hizo, Simba itamenyana na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mechi zingine zitakazochezwa siku hiyo, Mtibwa Sugar itamenyana na ndugu zao wa Polisi Moro kwenye uwanja wa Manungu uliopo Turiani, Morogoro, Coastal Union itawakaribisha ndugu zao wa Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwa, Tanga, Ruvu Shooting itapambana na ndugu zao wa JKT Ruvu kwenye uwanja wa Mabatini uliopo Ruvu mkoani Pwani, Azam itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati JKT Oljoro itacheza na Toto Africans kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Ratiba inaonyesha kuwa, Yanga itaanza mzunguko wa pili wa ligi hiyo Jumapili kwa kumenyana na Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi zingine zinazotarajiwa kuwa na ushindani mkali ni kati ya Yanga na Mtibwa Sugar zitakazomenyana Februari 2 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kati ya Yanga na Azam zitakazomenyana Februari 23 kwenye uwanja huo.

Mechi zingine ni kati ya Simba na Mtibwa Sugar zitakazomenyana Februari 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa na kati ya Simba na Azam zitakazomenyana Aprili 13 kwenye uwanja huo.

YANGA MWENDO MDUNDO

]


YANGA jana iliendeleza ubabe kwa Black Leopards ya Afrika Kusini baada ya kuichapa mabao 2-1 katika mechi ya kirafikiya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Ushindi huo ulikuwa wa pili mfululizo kwa Yanga dhidi ya Black Leopards. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilishinda mabao 3-2.

Iliwachukua Yanga dakika tatu kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Saidi Bahanuzi, kufuatia shuti la Simon Msuva, aliyepigiwa kona ndogo na David Luhende.

Baada ya kupata bao hilo, Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la Leopards, lakini ilipoteza nafasi nzuri za kufunga mabao dakika ya nne, sita na nane.

Leopards ilisawazisha dakika ya 13 kupitia kwa mshambuliaji wake, David Zulu kwa shuti kali lililomshinda kipa Ally Mustapha 'Bathez'. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Yanga ilikianza kipindi cha pili kwa kasi na kupata nafasi nyingine nzuri za kufunga mabao dakika ya 48, 50 na 52, lakini zilipotezwa na washambuliaji wake kutokana na kukosa umakini.

Katika kipindi hicho, Yanga iliwaingiza Tegete, Athumani Iddi 'Chuji', Haruna Niyonzima, Frank Dumayo na Didier Kavumbagu kuchukua nafasi za Cannavaro, Kabange Twite, Hamisi Kiiza, Bahanuzi na Luhende.

Bao la pili la Yanga lilifungwa na Jerry Tegete kwa njia ya penalti dakika ya 54 baada ya Didier Kavumbagu kuangushwa na beki mmoja wa Leopards ndani ya eneo la hatari. Leopards ilifanya mashambulizi makali kwenye lango la Yanga dakika ya 86 na 87, lakini washambuliaji wake, Mandli Miya na David Zulu walipoteza nafasi hizo za kufunga mabao.

Yanga: Ally Mustapha, Mbuyu Twite,Oscar Joshua, Nadir Haroub/Athumani Iddi, Kevin Yondan, Nurdin Bakari/Haruna Niyonzima, Simon Msuva/Nizar Khalfan, Kabange Twite/Frank Dumayo, Hamis Kiiza/Didier Kavumbagu na David Luhende.

Black Leopards: Posnef Omony, Moses Kwena, Thulani Ntshineela, Vicent Mabusela, Victor Kamhuka, Bafana Sibeko, Tuyane Mabunda/Siguve Sibia, Michael Nkambule/ Raymon Monama, Mxolis Gumende, Mandli Miya na David Zulu.

Tuesday, January 22, 2013

NI YANGA NA PRISONS, SIMBA NA LYON J'PILI

TIMU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga zimepangwa kuanza mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwa kumenyana na African Lyon na Prisons.

Wakati Simba itashuka dimbani Jumamosi kumenyana na Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga itashuka dimbani siku inayofuata kwenye uwanja huo kuvaana na Prisons.

Ratiba ya mzunguko huo iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inaonyesha kuwa, mechi zingine zitakazochezwa Jumamosi ni kati ya Mtibwa na Polisi (Manungu), Coastal Union na Mgambo Shooting (Mkwakwani), Ruvu Shooting na JKT Ruvu (Mlandizi), Azam na Kagera Sugar (Chamazi) na Oljoro JKT na Toto African (Sheikh Amri Abeid).

TFF imetangaza ratiba hiyo baada ya timu zote zinazoshiriki ligi hiyo kufuta mgomo wa kususia mechi za mzunguko wa pili kutokana na kutolipwa fedha za nauli na wadhamini, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, klabu zote 14 zimekubali kuendelea na mzunguko huo baada kufanyika kwa kikao cha pamoja na Kamati ya Ligi ya TFF.

Wambura alisema kikao hicho kilifanyika Januari 21 mwaka huu na kamati iliweka masharti kadhaa kabla ya kuendelea na ligi hiyo.

Alisema masharti hayo yanatokana na fedha za nauli kwa ajili ya klabu zilizotolewa na Vodacom kuchukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Fedha hizo ni sh. milioni 157.

Wambura alisema masharti hayo yatawasilishwa na Kamati ya Ligi kwa maandishi kwa Katibu Mkuu wa TFF na nakala kupelekwa kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Awali, klabu zilitishia kutoshiriki mzunguko wa pili wa ligi hadi fedha hizo zitakaporejeshwa na TRA.

Katika hatua nyingine, mzunguko wa pili wa michuano ya ligi daraja la kwanza unatarajiwa kuanza kutimua vumbi Februali 2, huku timu ya Small Kids ya Rukwa ikiondolewa na kushushwa daraja.

Wambura alisema timu hiyo imeshushwa daraja kwa mujibu wa kanuni baada ya kushindwa kucheza mechi mbili katika mzunguko wa kwanza na matokeo yote ya mechi, ambazo ilicheza katika mzunguko huo wa kwanza yamefutwa.

75 WAPITISHWA USAJILI WA DIRISHA DOGO

WACHEZAJI 75 wameidhinishwa kuzichezea timu mbalimbali katika mzunguko wa pili wa michuano ya soka ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara utakaoanza kutimua vumbi Jumamosi.

Katika usajili huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemuidhinisha kipa Shaaban Kado, aliyekuwa akichezea Mtibwa Sugar ya Morogoro kujiunga na Coastal Union ya Tanga.

Ofisa Habari wa (TFF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliyokutana Januari 19 mwaka huu, ilipitia maombi ya usajili wa dirisha dogo kwa klabu zote za za Ligi Kuu.

Wambura alisema licha ya kuwaidhinisha wachezaji hao, kamati hiyo imekataa kumuidhinisha Martin Mlolere, aliyeombewa usajili na Mgambo Shooting kutoka Majimaji baada ya taratibu za uhamisho wake kutokamilika, hivyo ataendelea kuichezea Majimaji.

Aliwataja wachezaji walioidhinishwa katika usajili huo, klabu zao zikiwa kwenye mabano kuwa ni Humphrey Mieno, Brian Umony, Jockins Atudo, David Mwantika, Abdallah Seif, Malika Ndeule na Uhuru Selemani -kwa mkopo(Azam).

Wengine ni Juma Mdindi, Njaidi Mohamed na Mahmoud Mbulu (Ruvu Shooting), Mohamed Kayi na Emmanuel Gabriel (Tanzania Prisons), Nurdin Selemani, Shaibu Nayopa, Hamidu Hassan, Paul Malipesa, Josephat Moses, Muharami Mnyangamala, Majaliwa Mbaga na Alphonce Peter (Oljoro JKT).

Wachezaji wengine ni Shukuru Kassim, Chacha Marwa, Salum Machaku, Mzamiru Said, Victor Bundala, Delta Thomas, Edward Mzeru na Tizzo Chomba (Polisi Morogoro), Edmund Kashamila na Julius Mrope (Kagera Sugar). Pia wamo Rajab Mohamed, Zakayo Joseph, Baraka Anthony na Mussa Chambo (Mtibwa Sugar), Zahoro Pazi (kwa mkopo), Emmanuel Linjechele, Kisimba Luambano na Nashon Naftali (JKT Ruvu), Moaka Shabani, Ismail Mkaima na Damas Milanzi (Mgambo Shooting), Donald Obimma, Exavery Muhollery, Mohamed Hussein na Ulugbe Odia (Toto Africans).

Wengine ni Obadi Mungusa, Juma Seif, Yusuf Mgwao, Ibrahim Job- kwa mkopo, Shamte Ally- kwa mkopo, Buya Jamwaka, Takang Valentine, Nurdin Mussa, Salvatory Jackson, Mohamed Athuman, Athuman Kajembe na Jarufu Kizombi (African Lyon), Mussa Mudde na Abel Dhaila (Simba), Rashid Simba, Zuberi Hamisi, Shaongwe Ramadhan, Castory Mumbara, Tinashe Machemedze na Shabani Kado (Coastal Union).