KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, December 27, 2016

HAJI MANARA AMUOMBEA MSAMAHA JERRY MURO KWA TFF



MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Hajji Sunday Manara amemuomba Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) amsamehe Mkuu wa Idara hiyo wa Yanga, Jerry Muro aliyefungiwa mwaka mmoja Julai mwaka huu.
Muro amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka pamoja na kutozwa faini ya Sh. Milioni 3 Julai mwaka huu baada ya Kamati ya Maadili ya TFF, chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Wilson Ogunde kumtia hatiani kwa mashitaka mawili kati ya matatu.
Makosa yaliyomtia hatiani Muro ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015 alipotakiwa kulipa faini ya Sh. Milioni 5 baada ya kufanya makosa, lakini amekaidi kulipa hadi leo.
Kwa kosa hilo alihukumiwa kutengana na masuala ya soka kwa mwaka mmoja- wakati shitaka lingine lililomtia hatiani ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe ya DRC.
Katika shitaka hilo, Jerry anadaiwa kuwashawishi mashabiki wa Yanga kuwafanyia vurugu mashabiki wa Simba kwenye mchezo huo ambao timu yake ilifungwa 1-0 na Mazembe Juni 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo, Manara amemuomba Rais wa TFF kumsamahe Muro baada ya kutumikia karibu nusu ya adhabu yake.
"Nimekaa nimetafakari sana, nimeamua kumuombea msamaha mtani wangu Jerry Muro ambaye TFF mlimfungia mwaka mmoja kujihusisha na mpira wa miguu, ninafanya hivi nikijua kabisa Jerry alikosea na tayari amekwishatumikia karibia nusu ya kifungo chake,"alisema Manara.
"Nnajua kwa kufanya hivyo atakuwa amekwishajifunza lugha za kutumia na pia itakuwa fundisho kwetu sisi wasemaji na viongozi wa vilabu kwa ujumla. Nafahamu pia Jerry aliwahi kunitolea lugha zisizostahili mimi binafsi, lakini yale yalikwishapita na binafsi amenihakikishia hatorudia tena, na ninaamini viongozi na washabiki wa Simba watanielewa dhamira yangu hii njema, ambayo inathibitisha uungwana tulio nao wana Simba,"aliongeza Manara.
Aidha, Manara amemuomba Rais Malinzi kutumia mamlaka yake kumfungulia Muro, au kuziomba kamati zilizomfungia kumuachia huru, hususan ikizingatiwa Muro si mzoefu sana wa utamaduni wa siasa za mchezo huu murua zaidi duniani.

IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

No comments:

Post a Comment