KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, December 15, 2016

YAHAYA AJIWEKEA MALENGO CAF


MSHAMBULIAJI mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Yahaya Mohammed, ameweka wazi kuwa moja ya malengo yake makubwa ni kuisaidia timu hiyo kuingia kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Azam FC ndio wawakilishi wa Tanzania Bara kwenye michuano hiyo mwakani baada ya kuwa washindi wa pili katika Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) msimu uliopita ikifungwa na Yanga mabao 3-1 katika mchezo wa fainali.

Nyota huyo kwenye mechi yake tu ya kwanza kuichezea Azam FC alifanikiwa kufunga bao, lililokuwa la pili kwa mabingwa hao walipokuwa wakicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi iliyopita, ulioisha kwa sare ya 2-2, bao jingine likiwekwa kimiani na winga Enock Atta Agyei.

Mohammed aliyesajiliwa kwenye usajili huu wa dirisha dogo akitokea Aduana Stars ya Ghana, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa atahakikisha anafunga mabao kwa kushirikiana na wachezaji wenzake ili kuweza kutimiza hilo.

“Kombe la Shirikisho ni lengo langu kubwa, nataka kuisaidia Azam FC kuingia hatua ya makundi na mimi kuwemo kwenye kikosi kitakachoingia katika hatua hiyo, malengo yangu makubwa yapo huko,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachosisimua na kuburudisha koo pamoja na Benki ya NMB, imekuwa na kiu kubwa ya kufika hatua ya makundi ya michuano kwa miaka minne iliyoshiriki michuano hiyo mikubwa barani Afrika (mara moja Ligi ya Mabingwa na mara tatu Kombe la Shirikisho Afrika), ambapo mwaka huu iliishia raundi ya pili baada ya kutolewa na vigogo wa Tunisia kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-2, ikishinda 2-1 nyumbani na kufungwa 3-0 ugenini.

Ujio wa VPL

Kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) unaotarajia kuanza wikiendi hii, kwa Azam FC kuvaana na African Lyon katika Uwanja wa Uhuru Jumapili ijayo saa 10.00 jioni, Mohammed amesema kuwa atajitahidi kwa uwezo wake kama mshambuliaji kuweza kufunga mabao ili kutimiza malengo ya klabu.

“Mimi kama mshambuliaji kazi yangu ni kufunga, nimeanza vizuri kwa kufunga bao katika mechi yangu ya kwanza (Mtibwa Sugar), nimejipanga kuendeleza mazuri niliyoyaanza, japo haitakuwa kila siku lakini nitajitahidi kufanya mazuri kwa ajili ya Azam FC,” alisema.

Kupambana na vikombe

Mohammed aliongeza kuwa: “Nitajitahidi kufanya mazuri kama nilivyosema awali, nahitaji kujitoa kwa ajili ya Azam FC kushinda makombe na kufikia malengo ambayo walipanga kufikia.”

Upinzani VPL

Wakati Azam FC ikicheza na Mtibwa Sugar wikiendi iliyopita, Mohammed amejionea aina ya upinzani anaotarajia kukutana kwenye mechi za ligi, na kusema kuwa ameona viwango vya juu pamoja upinzani mkali.

“Unajua hili ni daraja la Ligi Kuu, hivyo lazima utegemee viwango vya hali ya juu, kwangu mimi nimejipanga vema na upinzani na sitaidharau timu yoyote, kitu cha kwanza kwangu kitakuwa ni kujitahidi kufanya mazuri kwa manufaa ya Azam FC,” alisema.

Alivovutiwa na Bocco

Wakati akisifu ushirikiano anaoonyeshwa na wachezaji wenzake wa Azam FC, nyota huyo wa zamani wa Aduana Stars na Asante Kotoko zote za Ghana, hakusita kumtaja Nahodha wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’, akisema kuwa ni mtu mzuri sana.

“Wachezaji wenzangu wote wako vizuri ni kama kaka zangu tokea niwasili hapa hasa Bocco (John) ni mtu mzuri sana, nawaheshimu wachezaji wenzangu wote wako vizuri sana,” alisema.

Rekodi zake

Mohammed amesajiliwa Azam FC akitoka kuwa mfungaji bora namba mbili wa Ligi Kuu ya Ghana msimu uliopita, akitupia wavuni mabao 15 akizidiwa mawili na staa wa Liberty Proffesional, Latif Blessing, aliyefunga 17.

Staa huyo msimu uliopita aliweka rekodi ya aina yake ya kuwa mchezaji wa kwanza kwenye historia ya klabu ya Aduana kufunga mabao matatu kwenye mechi moja ‘hat-trick’ tokea timu hiyo ipande Ligi Kuu mwaka 2009, alifanya hivyo walipoichapa Sekondi Hasaacas 4-0.

Mbali na kuwahi kuichezea timu ya Taifa ya Ghana, mwaka juzi alikuwa ni miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo waliochaguliwa kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN) zilizofanyika nchini Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment