KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, December 19, 2016

YANGA YAIENGUA SIMBA KILELENI MWA LIGI KUU BARA



YANGA imepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Ruvu jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 36 baada ya kucheza mechi 16 na kuishusha Simba iliyomalizia kileleni mzunguko wa kwanza kwa pointi zake 35. Lakini Simba inaweza kurejea kileleni kesho ikishinda dhidi ya wenyeji, Ndanda FC mjini Mtwara.
Shujaa wa Yanga leo alikuwa ni winga Simon Happygod Msuva aliyefunga mabao mawili kipindi cha pili baada ya kuseti moja kipindi cha kwanza.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Heri Sasii aliyesaidiwa na Hellen Mduma na Kassim Mpanga wote wa Dar es Salaam hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lililokuja baada ya muda mrefu wa timu zote kushambuliana kwa zamu, lilifungwa na beki Michael Aidan Pius aliyejifunga dakika ya 38 katika harakati za kuokoa krosi ya Simon Msuva iliyokuwa inafuatiliwa vizuri na winga Deus Kaseke. 
JKT Ruvu pamoja na kuondoka uwanjani baada ya nusu ya kwanza wakiwa nyuma, lakini walicheza vizuri na kupeleka mashambulizi mawili ya hatari langoni mwa Yanga ambayo yaliokolewa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’.
Yanga nayo ilicheza vizuri pia, lakini wachezaji wake walishindwa kutengeneza nafasi nzuri za kufunga katika kipindi cha kwanza zaidi ya hiyo waliyotumia kupata bao la kwanza.
Dakika 10 baada ya kuanza kipindi cha pili, kocha Mzambia wa Yanga, George Lwandamina alimtoa mshambuliaji Amissi Tambwe na kumuingiza kiungo Said Juma ‘Makapu’.
Mabadiliko hayo yaliifanya Yanga ianze kutawala sehemu ya kiungo na kupika mashambulizi yenye shibe hatimaye kupata mabao mawili zaidi.
Msuva alifunga bao la pili kwa kichwa dakika ya 57 akimalizia krosi ya Kaseke baada ya kazi nzuri ya kiungo mwenzake Haruna Niyonzima. Msuva tena akafunga bao la tatu dakika ya 90 akimalizia pasi ya Niyonzima dakika ya 90.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm alikuwepo jukwaa kuu kufuatilia mchezo, wakati kiungo mpya kutoka Zambia, Justin Zulu alikuwa jukwaani kwa sababu bado hajapatiwa kibali cha kufanya kazi nchini.
Baada ya mchezo, kocha Lwandamina alisema timu haijaanza kucheza kwa kiwango chake kwa kuwa bao anajaribu wachezaji.
Matokeo ya mechi nyingine za Ligi Kuu leo; Mzima. Mwadui imeilaza 1-0 Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Mbeya City imelazimishwa sare ya 0-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Ruvu Shooting imetoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY

No comments:

Post a Comment