KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, August 31, 2012

MBUYU TWITE KUTAMBULISHWA LEO U/TAIFA DAR

Beki mpya wa Yanga, Mbuyu Twite akipewa maelekezo na Kocha Tom Saintfiet wakati wa mazoezi yaliyofanyika jana kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola mjini Dar es Salaam.

Mbuyu Twite akiwa katika mazoezi ya Yanga yaliyofanyika jana kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola.


BEKI mpya wa klabu ya Yanga, Mbuyu Twite anatarajiwa kutambulishwa rasmi leo kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Kocha Tom Saintfiet wa Yanga amepanga kumtambulisha beki huyu wakati wa mechi ya kirafiki ya soka dhidi ya Coastal Union itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Twite aliwasili nchini juzi akitokea Rwanda na kumaliza wasiwasi uliokuwa umetanda kwamba huenda angeshindwa kujiunga na timu hiyo baada ya kudaiwa kuwa aliitapeli Simba.

Hata hivyo, hakuna uhakika iwapo Twite atacheza mechi hiyo kutokana na kutofanya mazoezi na wenzake kwa muda mrefu.

SIMBA, AZAM KUWANIA NGAO YA HISANI SEPT 11

Kikosi cha Simba kitakachocheza na Azam kuwania Ngao ya Jamii


Kikosi cha Azam kitakachocheza na Simba kuwania Ngao ya Jamii


Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria ufunguzi rasmi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 kati ya bingwa mtetezi Simba na makamu bingwa Azam itachezwa Septemba 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
MCHEZAJI WA MTIBWA SUGAR NAYE APATA ITC

Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) limetuma Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Ayoub Hassan Isiko aliyejiunga na Mtibwa Sugar akitokea timu ya Bull FC ya nchini humo.

ITC hiyo ilitumwa jana (Agosti 30 mwaka huu), hivyo kufanya wachezaji ambao ITC hazijapatikana hadi sasa kubaki wawili tu. Dirisha la usajili wa wachezaji litafungwa rasmi Septemba 4 mwaka huu.

Wachezaji ambao ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng kutoka AFC Leopards ya Kenya waliojiunga na Simba.

ITC hizo zinatarajiwa kupatikana wakati wowote kwani tayari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeshaziomba kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) baada ya nyaraka zote zilizokuwa zikitakiwa kupatikana.

SERENGETI BOYS KUJIPIMA NA ASHANTI

Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyokuwa kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Kenya itavunja rasmi kambi yake kesho (Jumamosi) kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Ashanti United.
Mechi hiyo dhidi ya Ashanti United iliyoko daraja la kwanza itachezwa kuanzia saa 10 jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa kiingilio cha sh. 2,000.
Serengeti Boys ilikuwa Septemba 9 mwaka huu icheze na Kenya kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, lakini Kenya ikajitoa ambapo sasa itacheza na Misri katika raundi ya pili.
Mechi ya kwanza itachezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Mwishoni mwa Septemba, Serengeti Boys itarejea tena kambini kujiandaa kuikabili Misri ambapo kabla inatarajia kupata mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu itakayotangazwa baadaye.

MTIHANI WA MAWAKALA WA WACHEZAJI SEPT 17

Mtihani kwa ajili ya watu wanaotaka kuwa mawakala wa wachezaji wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Septemba 27 mwaka huu saa 4 kamili asubuhi ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa wanaotaka uwakala huo wanatakiwa kujisajili ambapo watapewa kanuni mbalimbali za FIFA na TFF ili waweze kujiandaa kikamilifu kwa mtihani huo utakaokuwa na sehemu mbili.

Sehemu ya kwanza ni maswali kutoka FIFA wakati nyingine ni kutoka TFF. Ada ya mtihani ni dola 50 za Marekani.

Pia Damas Ndumbaro na Ally Mleh wa Manyara Sports Management ambao tayari ni mawakala wanaotambuliwa na FIFA wanatakiwa kufanya mtihani huo kama wanataka kuendelea na uwakala kwa vile muda wa leseni zao za awali umemalizika.

Mawakala wengine ambao ni John Ndumbalo, Mehdi Remtulla, Ally Saleh, Yusuf Bakhresa na Said Tully leseni zao bado ziko hai.

WACHEZAJI 17 WAWEKEWA PINGAMIZI LIGI KUU

Klabu mbalimbali zimewasilisha pingamizi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupinga usajili wa wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu.
Toto Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.
Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.
Super Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.
Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.
Azam inapinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani. Nayo Simba inapinga Kelvin Yondani kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.
Vilevile Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo alilipwa dola 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.
Nayo Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu) kupitia pingamizi hizo pamoja na usajili wa wachezaji kwa ujumla kwa 2012/2013.

SIMBA, YANGA KUKIPIGA OKTOBA 3, 2012, KURUDIANA MEI 18, 2013

Michuano ya Ligi Kuu kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kwa msimu wa 2012/2013 itaanza Septemba 15 mwaka huu kwa timu zote 14 kujitupa kwenye viwanja tofauti.
Mechi za ufunguzi zitakuwa kati ya Simba vs African Lyon (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Polisi Morogoro vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro), Tanzania Prisons vs Yanga (Sokoine, Mbeya), Mgambo JKT vs Coastal Union (Mkwakwani, Tanga), JKT Ruvu vs Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), Kagera Sugar vs Azam (Kaitaba, Bukoba) na Toto Africans vs Oljoro JKT (Kirumba, Mwanza).
Mzunguko wa kwanza (first round) utamalizika Novemba 11 mwaka huu ambapo kwenye mzunguko huo mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba itachezwa Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ligi hiyo itamalizika Mei 18 mwakani kwa mechi kati ya Toto Africans vs Ruvu Shooting (Kirumba), Mgambo JKT vs African Lyon (Mkwakwani), JKT Ruvu vs Mtibwa Sugar (Azam Complex), Tanzania Prisons vs Kagera Sugar (Sokoine), Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Azam (Sheikh Amri Abeid Kaluta) na Polisi Morogoro vs Coastal Union (Jamhuri).
Endapo Simba na Azam hazitafanikiwa kuvuka hatua mojawapo ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, ratiba hiyo itafanyiwa marekebisho.

Thursday, August 30, 2012

DIWANI ILALA ATEMBELEA KAMBI ZA MISS UTALII ZA KINONDONI NA ILALA



DIWANI wa kata ya mchikichini na Mwenyekiti wa Madiwani wa
kata tano (Ilala, Mchikichini, Kariakoo, Gerezani na Jangwani),
Ghalib Riyami ametembelea kambi ya washiriki wa
Miss Utalii wilaya ya Ilala na Kinondoni 2012.

Kambi hiyo ya pamoja kati ya warembo wanao
wania taji la Miss Utalii Ilala 2012 na wale wanao wania taji la Miss
Utalii Kinondoni 2012 ipo katika hoteli ya kitalii ya nyota tatu ya
Lamada Hotel.
Diwani huyo ameelezea kufurahishwa kwake kwa wilaya ya
Ilala kupewa heshima ya kuwa wenyeji wa shindano hilo la
kihistoria ambapo wilaya mbili kwa pamoja zinashindana kuwania
mataji ya wilaya zao katika ukumbi na steji moja tena siku moja.
“Najua waandaaji wangeweza kuamua shindano hili lifanyikie
kinondoni,lakini mmeamua kutupa heshima hiyo sisi wa wilaya ya
ilala,hakika tumefarijika sana,” alisema.

Katika kuonyesha furaha yake na kupokea heshima hiyo aliyoiita

kubwa, diwani huyo aliahidi kuwa yeye binafsi pamoja na

madiwani wa wilaya ya ilala watahakikisha wanasaidia na kuunga

mkono kwa hali na mali kufanikisha kufanyika kwa shindano hilo

kama lilivyopangwa yaani tarehe 14/09/2012 katika hotel ya Lamada.
Aliwataka warembo wanaoshiriki shindano hilo kutambua kuwa
shindano hili tofauti na mashindano mengine ni alama ya urithi wa
Taifa na kielelezo cha utamaduni wa mtanzania,hivyo wanapaswa
kutambua kuwa na nidhamu na kuvaa uhalisia wa mtanzania siku
zote na wakati wote mashindanoni nan je ya mashindano.
Amewakumbusha na kuwaomba kutumia shindano hili kutangaza
utalii wa wilaya ya Ilala na mkoa kwa ujumla ikiwemo uwanja wa

ndege wa Juliasi Nyerere, soko la Kariakoo, Makumbusho ya
Taifa, soko la kimataifa la samaki la Magogoni, shule ya Pugu
ambayo Mwalimu Nyerere alifundisha, na ufukwe wa bahari ya
hindi.
Diwani huyo aliwashukuru na kuwapongeza wadhamini
mbali mbali ambao wamethibitisha kudhamini shindano
hili,wakiwemo Lamada Hotel,105 Times FM Radio,Kahama Gold
Mine,Traventine Hotel,Mzee Yusuph Enterprises,Easy Media,Daja
Saloon,Zizu Fashion,Tambaza Cort Brocker and Action Mart,Dagaa
Finance na Aucland Travel and Tours,Hameed Designer.

Ametoa wito kwa kampuni na watu mbali mbali
kudhamini na kuchangia shindano hili ambalo gharama za kuandaa
ni kubwa hivyo kuhitaji mchango wa hali na mali.
Jumla ya warembo ishirini na nne(24), kumi na mbili kutoka wilaya ya
Kinondoni na kumi na mbili kutoka wilaya ya Ilala kwa pamoja
watachuana ili kupata taji la Miss Utalii wa wilaya ya Ilala na Miss
Utalii wilaya ya Kinondoni.

Wilaya ya Ilala washiriki ni Zourha Malisa, Nancy Musheruzi,

Princess Lemi, caroline Yust, Eunice George, Naomi Michael, Lucy Julius,

Nurina Mikindo, Rose James, Salome Kiula, Marry Wambura na Judith Frank.

Washiriki wa wilaya ya Kinondoni ni Mwasiti Thabit, Irene Richard,

Hellen Herman, Fatma Hussein, Rachel Magai, Neema Mbeju,
Neema Ngowi, Duda Tumbo, Zahra Waziri, Janeth Nelson,

Teddy Paul na Ruby Kivunjo.
Akizungumza na warembo hao muheshimiwa diwani alisisita
umuhimu wa warembo hawa kulitumikia taifa kwa kutangaza
vivutio vya kitalii kitaifa na kimataifa ili kusaidia kuinua uchumi na
kuongezeka kwa pato la taifa wakati huu ambapo sekta ya utalii
inachangia asilimia zaidi ya kumi na saba(17%) ya pato la taifa.
Alisisitiza umuhimu wa kuelimisha vijana mashuleni ili kukuza na
kuhamasisha utalii wa ndani pia alisisitiza haja ya kutangaza kwa
nguvu zote vivutio vya utalii vya nchi yetu ya Tanzania ili kuongeza
idadai ya watalii wanaotembelea, ikiwa hadi leo kulingana na
takwimu Tanzania hutembelewa na watalii laki nane(800,000) kwa
mwaka na hii ni idadi ndogo ukilinganisha na nchi jirani
zinazotuzunguka.
Pia alitoa wito kwa wazazi kuondokana na dhana potofu juu ya
mashindano ya urembo na aliwaasa mabinti kuwa na heshima,
adabu na haiba nzuri ili kuifanya jamii kubadili mtazamo juu ya
mashindano haya yenye tija kwa taifa letu kwa kuwa linatangaza
utalii wa taifa hili la Tanzania.
Mwisho aliahidi ushirikiano wa hali na mali katika kufanikisha
shindano hili ambalo limepangwa kufanyika katika ukumbi wa
lamada hotel ambao upo katika umoja wa kata tano
anazoziongoza.

MAKUNDI LIGI YA MABINGWA ULAYA YATAJWA


Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) limetangaza makundi manane ya michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya. Makundi hayo ni kama ifuatavyo:

KUNDI A: Porto, Dynamo Kiev, Paris St Germain, Dinamo Zagreb
KUNDI B: Arsenal, Schalke, Olympiakos, Montpellier
KUNDI C: AC Milan, Zenit St Petersburg, Anderlecht, Malaga
KUNDI D: Real Madrid, Manchester City, Ajax, Borussia Dortmund,
KUNDI E: Chelsea, Shakhtar Donetsk, Juventus, FC Nordsjaelland,
KUNDI F: Bayern Munich, Valencia, Lille, Bate Borisov,
KUNDI G: Barcelona, Benfica, Spartak Moscow, Celtic,
KUNDI H: Manchester United, Braga, Galatasaray, CFR Cluj

MBUYU TWITE AFUNIKA DAR



Hatimaye mshambuliaji mpya wa klabu ya Yanga, Mbuyu Twite amewasili nchini leo alasiri na kujiunga na kambi ya timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Twite alitua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam saa tisa alasiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda na kupokewa na viongozi wa Yanga pamoja na mashabiki wa klabu hiyo.

Aliyeongoza mapokezi ya beki huyo wa zamani wa APR ya Rwanda ni makamu mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Seif Ahmed Magari na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa.

Awali, ujio wa beki huyo mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ulionekana kama sinema, kwani licha ya ndege kutua uwanjani mapema huku mashabiki wakimsubiri kwamba hamu kubwa, alichelewa kutoka nje ya uwanja huo.

Na pale alipotoka nje, alikuwa ameongozana na Mwesigwa pamoja na Seif huku wakiwa wamezungukwa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo maarufu kwa jina la makomandoo.


Beki huyo alikuwa amevalia kaptura ya khaki na fulana ya njano, lakini mara baada ya kutoka nje, baadhi ya mashabiki walimvisha jezi nyingine yenye rangi ya njano na kijani, ikiwa na namba nne na jina la Rage mgongoni.

Jezi hiyo ilikuwa na jina la Rage, kufuatia msuguano mkali kati ya klabu hiyo na Simba kuhusu usajili wa beki huyo, ambapo awali ilidaiwa kuwa, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alishafanya naye mazungumzo na kumsajili kwa kitita cha dola 30,000 za Marekani, zaidi ya sh. milioni 35.
Lakini baadaye kukawa na taarifa kwamba, beki huyo alighairi kujiunga na Simba, badala yake akaingia mkataba na Yanga baada ya kulipwa kitita cha sh. milioni 75.

Tayari Twite ameshakamilisha taratibu zote za kujiunga na Yanga ikiwa ni pamoja na kupatiwa hati ya uhamisho ya kimataifa (ITC) kutoka APR.

Akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo, Twite alisema amekuja Tanzania kucheza soka na aliwataka mashabiki wa Yanga watarajie mambo makubwa kutoka kwake.

BREAKING NEWS! HATIMAYE MBUYU TWITE ATUA DAR

HATIMAYE MSHAMBULIAJI MBUYU TWITE ALIYESAJILIWA NA KLABU YA YANGA KUTOKA APR YA RWANDA AMETUA NCHINI ALASILI HII NA KUPATA MAPOKEZI MAKUBWA KUTOKA KWA MASHABIKI WA TIMU HIYO.

TWITE ALITUA UWANJA WA NDEGE WA MWALIMU JULIUS NYERERE SAA TISA ALASILI KWA NDEGE YA SHIRIKA LA NDEGE LA RWANDA NA KUSABABISHA VURUGU KUBWA UWANJANI HAPO.

BEKI HUYO MWENYE ASILI YA JAMHURI YA KIDEMOKRASI YA CONGO, AMEPOKEWA NA VIONGOZI TAKRIBAN WOTE WA YANGA, WAKIWEMO WAJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI.

BAADHI YA WANACHAMA MAARUFU WA KLABU HIYO KWA JINA LA MAKOMANDOO WALIMWEKEA ULINZI MKALI BEKI HUYO ILI KUHAKIKISHA HAPATI MADHARA YOYOTE KUTOKA KWA MAHASIMU WAO SIMBA.

HABARI ZAIDI KUHUSU MAPOKEZI HAYO PAMOJA NA PICHA UTAZIPATA MUDA MFUPI UJAO KUTOKA KWA WAPIGANAJI WA BLOGU YA LIWAZO ZITO WALIOPO UWANJANI HAPO MUDA HUU.

REAL MADRID BINGWA KOMBE LA MFALME HISPANIA

Hiki ndicho kikosi cha Real Madrid kilichotwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Mfalme la Hispania jana usiku baada ya kuichapa Barcelona mabao 2-1 na kuibuka na ushindi wa jumla kwa faida ya bao la ugenini baada ya kuchapwa mabao 3-2 katika mechi ya awali wiki iliyopita.


LULU KUBURUTWA TENA KORTI YA RUFANI SEPT 17

NA FURAHA OMARY
MAHAKAMA ya Rufani Tanzania, imepanga kusikiliza shauri la umri wa msanii wa filamu Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, Septemba 17 mwaka huu.
Rufani hiyo iliyokatwa na upande wa Jamhuri kupinga uamuzi wa Jaji Dk. Fauz Twaib kukubali kusikiliza maombi ya kufanyia uchunguzi umri wa Lulu, itasikilizwa na jopo la Majaji watatu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika Mahakama ya Rufani, Majaji waliopangwa kusikiliza shauri hilo ni Jaji Bernard Luanda, Jaji January Msoffe na Jaji Katherine Oriyo.
Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Msanii huyo anadaiwa kutenda kosa hilo, Aprili 7, mwaka huu, nyumbani Kanumba Sinza.
Umri wa msanii huyo umezua utata baada ya mawakili wanaomtetea kudai ana miaka 17 na si 18 kama ilivyodaiwa katika hati ya mashitaka na hivyo kuiomba kesi hiyo isikilizwe katika Mahakama ya Watoto.

Hata hivyo, Mahakama ya Kisutu iliyakataa maombi hayo kwa madai haina uwezo wa kusikiliza shauri hiyo na ndipo mawakili wa Lulu wakawasilisha maombi hayo Mahakama Kuu ambayo katika uamuzi wake ilikubali kufanya uchunguzi wa umri halali wa mshitakiwa huyo.

Hata hivyo siku ambayo Mahakama Kuu ilitarajia kuanza kusikiliza maombi hayo, upande wa Jamhuri uliitarifu kuwa umewasilisha Mahakama ya Rufani maombi ya marejeo ya uamuzi huo.
Kutokana na hilo, Mahakama Kuu aliamua kuahirisha kusikiliza maombi hayo kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani.

SIMBA KURUDIANA NA NAIROBI CITY JPILI ARUSHA

TIMU ya Simba inatarajia kucheza mechi dhidi ya timu ya soka ya Nairobi City Stars siku ya Jumapili ijayo katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta jijini Arusha.
Timu hiyo kutoka Kenya ndiyo iliyocheza na Simba jijini Dar es Salaam katika tamasha la Simba Day na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Awali Simba ilikuwa imepanga kucheza mjini Tanga wikiendi hii, lakini kutokana na mabadiliko ya programu ya mazoezi ya benchi la Ufundi, Wekundu wa Msimbazi sasa watabaki Arusha hadi Septemba nne mwaka huu ili kukamilisha programu yote bila ya usumbufu.
Hali ya kikosi cha Simba ni ya utulivu kabisa na mazoezi yanafanyika kwa mchanganyiko wa mazoezi ya uwanjani na GYM.
Hakuna majeruhi yoyote hadi sasa na wachezaji wote wanafanya mazoezi kama kawaida.
Kwenye mechi mbili za kirafiki zilizopita jijini Arusha, mlinda mlango namba moja wa Simba, Juma Kaseja, hakudaka na badala yake waliodaka ni Wilbert Mweta na Waziri Hamadi Mwinyiamani.
Kudaka kwa makipa hao ni mipango tu ya mwalimu na Kaseja hana maumivu yoyote na anafanya mazoezi kwa nguvu sana kujiandaa na msimu ujao.
Kama ilivyo ada, Kaseja atadaka siku ambayo mwalimu ataamua akae langoni.
Kuna baadhi ya vyombo vya habari vimeanza kuandika vichwa vya habari vyenye lengo la kuuza magazeti kutokana na kufiwa kwa mchezaji wetu huyu.
Simba SC inapenda kutumia nafasi hii kuviomba vyombo vya habari na wadau wengine kumuacha mchezaji huyu aomboleze msiba huu na siku yake ya kurudi itakapofika, klabu itatangaza.
Simba SC inafahamu kiu ya vyombo vya habari kuhusiana na kutaka kujua masuala ya usajili wa wachezaji wake wa kigeni.

Ukweli ni kwamba taarifa yoyote itakayotoka leo au kesho itakuwa haijaiva bado na klabu isingependa kutoa taarifa ambazo hazijaiva bado.
Tutatoa taarifa rasmi na kamili wakati mchakato mzima utakapokuwa umekamilika.

Kwa hiyo, Simba haitatoa tamko lolote kwa sasa kuhusu usajili wa wachezaji wake wa kigeni hadi kila kitu kikamilike.
Tunaahidi kwamba hilo litafanyika haraka iwezekanavyo ili kiu yenu itimizwe.

EZEKIEL KAMWAGA

MSEMAJI,

SIMBA SC

DIAMOND AIBUKA MSHINDI WA NANI MKALI, PROFESA J ASHIKA NAFASI YA PILI

Naseeb Abdul 'Diamond' aibuka mshindi wa nani mkali


Profesa J ashika nafasi ya pili


Ali Kiba ameshika nafasi ya tatu


Ambwene Yesaya AY ameshika nafasi ya tatu kwa kufungana na Kiba


Khamis Mwinjuma 'Mwana FA' ameshika nafasi ya tano


Khaleed Mohamed TID ameshika mkia




MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipywa, Naseeb Abdul
'Diamond' ameibuka mshindi wa shindano na msanii yupi mkali wa
kiume wa muziki huo.Diamond ameibuka mshindi wa shindano hilo baada ya
kuwabwaga washiriki wenzake watano.Shindano hilo liliandaliwa na blogu ya liwazo zito na iliendeshwa
kwa muda wa mwezi mmoja kwa wasomaji kuwapigia kura
washiriki.Diamond aliibuka mshindi baada ya kupata kura 21, ambazo ni
sawa na asilimia 45 ya kura zilizopigwa.Mkongwe Joseph Haule, maarufu kwa jina la Profesa J aliibuka
mshindi wa pili baada ya kupara kura nane, sawa na asilimia 17.Nafasi ya tatu ilichukuliwa kwa pamoja na Ali Kiba na Ambwene
Yesaya waliopata kura sita kila mmoja, sawa na asilimia 13. Khamisi Mwinjuma 'Mwana FA' alishika nafasi ya nne baada ya
kupata kura nne, sawa na asilimia nane wakati Khaleed Mohamed
TID alishika mkia baada ya kuambulia kura moja, sawa na asimilia
mbili.Hii ni mara ya sita kwa blogu ya liwazo zito kuendesha shindano la
kuchagua wasanii na wanamichezo bora wa fani mbali mbali ili
kuwawezesha wajitambue mahali walipo na wajue nini la kufanya.Blogu hii inawashukuru wasomaji wake wote walioshiriki kupiga
kura kwa wasanii walioshiriki kwenye shindano hili na kuwaomba
waendeleze ushirikiano huo katika mashindano yajayo.

PATA NAKALA YAKO YA BURUDANI LEO




Wednesday, August 29, 2012

MALINZI AZINDUA ROCK CITY MARATHON

MWENYEKITI wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi, amezindua rasmi michezo ya nne ya mbio za Rock City Marathon, zitakazofanyika kuanzia Oktoba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika mjini Dar es Salaam jana, Malinzi alisema huu ni wakati wa kukufua vipaji vya mchezo wa riadha nchini.
“Kwanza nawashukuru Kampuni ya Capital Plus Internationa kwa kuendelea kuandaa mbio hizi kwa miaka mine sasa. Sio siri michezo Tanzania imedorora, kwani tumechukua dhamana ya michezo, lakini baadhi ya watu wamekuwa walafi, wanajenga majumba Mbezi Beach na kuendesha magari ya kifahari.
“Hii yote imechangiwa na dhamana ya uongozi wa michezo kuwapa walafi ambao wametufikisha hapa. Nawaomba Capital Plus International msiishie hapa, tunataka sasa tufufue vipaji vya riadha na mwaka huu tumeamua tuwe na mashindano ya taifa ya riadha,” alisema Malinzi.
Mashindano hayo yamevutia wadau wengi waliojitokeza kudhamini mbio hizo, ambao ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), African Barrick Gold, Nyanza Bottlers, Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), Geita Gold Mine, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Sahara Communications, Shirika la Ndege Tanzania (ATC), New Mwanza Hotel, Airtel na New Africa Hotel.
Mbio za mwaka huu zitahusisha mashindano mbali mbali kama vile mbio za nyika za kilomita tano (ambazo sio za ushindani) , mbio za nusu marathon za kilomita 21 na mbio za kujifurahisha maarufu kama 'fun race'.
Mbio zingine ni za walemavu za kilomita tatu, mbio za watu wazima za kilomita tatu na mbio za watoto kuanzia miaka saba hadi 10 zenye urefu wa kilomita mbili.
Msemaji wa Capital Plus International, Dk. Ellen Otaru, alisema mbio hizo zinakwenda sambamba na kuhamasisha utalii wa ndani kupitia sekta ya michezo, ambapo washiriki watatoka Ziwa Victoria na nchi jirani za Kenya, Uganda, Afrika Kusini na baadhi ya mataifa ya Ulaya.
“Ningependa kutoa shukrani kwa wafadhili mbali mbali waliofanikisha mashindano haya, nasi Capital Plus International tunataka kuwahakikishia kuwa tunakuza riadha nchini na kuleta medali za dhahabu,” alisema.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Riadha Tanzania (RT), William Kalage, alisema wameridhia uwezo wa Capital Plus International kuandaa mbio hizo kwa mara ya nne kwa ufanisi.
“Sote tunatambua mchezo wa riadha ndio ulioipa sifa nchi yetu, lakini kwa sasa umedorora. Safari ya kuiletea medali nchi yetu imeanza na lazima tuwekeze kwenye riadha ili tupate medali,” alisema Kalage

TWITE AIKOROGA YANGA

UJIO wa beki wa kimataifa wa Rwanda, Mbuyu Twite umeendelea kuwa kitendawili baada ya kushindwa kuwasili nchini jana kujiunga na Yanga.
Badala yake, uongozi wa klabu ya Yanga umesema beki huyo wa zamani wa APR ya Rwanda sasa anatarajiwa kutua nchini leo saa tisa alasiri.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, taratibu zote za kumwezesha Twite kuja nchini leo zimekamilika.
Awali, Twite ilikuwa awasili na kikosi cha Yanga mwanzoni mwa wiki hii, lakini alishindwa kufanya hivyo kwa madai kuwa, alikwenda kwao Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuchukua familia yake.
Baadaye kulikuwepo na taarifa kwamba beki huyo angetua juzi au jana, lakini mara zote ameshindwa kufanya hivyo na kumweka kwenye wakati mgumu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Tom Saintfiet.
“Twite atatua nchini kesho (leo). Alibaki Rwanda kwa sababu za msingi, nawaomba mashabiki wa Yanga wajitokeze kwa wingi kwenda kumpokea kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam,”alisema.
Sendeu aliponda tishio lililotolewa na viongozi wa klabu ya Simba kwamba, watahakikisha wanamkamata mchezaji huyo mara atakapotua nchini kwa tuhuma za kuwatapeli.
“Hao wanaodai kwamba wana RB ya kumkamata Twite kutoka polisi Interpool wanajisumbua kwa sababu wanachokifanya ni kichekesho,”alisema Sendeu.
Ofisa Habari huyo wa Yanga alisema Twite anatarajiwa kujiunga moja kwa moja na Yanga kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza Septemba 15 mwaka huu.
Yanga imekuwa ikifanya mazoezi yake kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Dar es Salaam na inatarajiwa kucheza mechi nyingine ya kirafiki Jumamosi kwa kumenyana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa.
Kwa mujibu wa Sendeu, iwapo mambo yatakwenda vizuri, Twite huenda akashuka dimbani kucheza mechi hiyo na kutambulishwa rasmi kwa mashabiki wa Yanga.
Katika hatua nyingine, habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, kuchelewa kuwasili nchini kwa mchezaji Mbuyu Twite kumemkera Kocha Tom Saintfiet.
Kwa mujibu wa habari hizo, kocha huyo kutoka Bulgaria amewataka viongozi wa Yanga wahakikishe mchezaji huyo anatua nchini haraka iwezekanavyo, vinginevyo atagoma kumpokea.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, kuchelewa kuwasili kwa mchezaji huyo kumevuruga programu ya Saintfiet, ambaye hadi sasa ameshindwa kupata kikosi cha kwanza cha kudumu.
Imeelezwa kuwa, awali kocha huyo aliwataka viongozi wa Yanga wahakikishe kuwa, Twite anakuja nchini pamoja na timu hiyo Jumatatu iliyopita, lakini mipango hiyo ilikwama baada ya mchezaji huyo kuomba ruhusa ya kwenda kuichukua familia yake Congo.
Kocha huyo pia ameulalamikia uongozi wa Yanga kwa kushindwa kumpatia usafiri wa uhakika na kumwacha aendelee kutumia basi dogo la klabu, ambalo anadai kuwa halifai kwa usalama wake.

SUMA MNAZARETI :SIJAFUKUZWA MTANASHATI

SIKU chache baada ya kutangazwa kuwa ametimuliwa katika kundi la Mtanashati, msanii Suma Mnazareli ameibuka na kukanusha vikali taarifa hizo.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Suma alisema hakutimuliwa kwenye kundi hilo bali aliamua kujiondoa mwenyewe.
“Nimeamua kujitoa Mtanashati sababu kubwa ikiwa ni kukosa kile nilichokuwa nikikitarajia,”alisema msanii huyo.
“Nilikwenda Mtanashati kufanyakazi, sikufuata pesa zake. Nilichokuwa nadhani ningekipata, hakipo. Bosi anatafuta zaidi sifa na umaarufu Tanzania na mimi muziki ni kazi yangu,”aliongeza.
Suma alidai kuwa, kiongozi wa kundi hilo, Ustaadh Juma Namusoma anaweza kugawa mamilioni kwa wasanii ili atajwe kwenye nyimbo zao, lakini anashindwa kulipa pesa za kutengeneza video ya msanii wake.
Alidai kuwa, kuna wakati kiongozi huyo alimpatia sh. 300,000 kwa ajili ya kurekodi video, ambazo alisema hazitoshi na zinadhihirisha wazi kuwa, hana dhamira ya dhati ya kuwainua wasanii wake.
“Unadhani tutaweza kushindana na video za wasanii kama AY za milioni 30? Nimeuza hadi simu yangu ya Blackberry ili kuongeza pesa kwa ajili ya kukamilisha video yangu,”alisema msanii huyo akionekana kuwa na masikitiko makubwa.
“Hii ndiyo sababu iliyonifanya nijiondoe Mtanashati kwa sababu sioni faida yoyote ya kuendelea kuwepo kwenye kundi na mimi muziki kwangu ni maisha na nataka nifike mbali zaidi,”alisisitiza.
Wiki iliyopita, Ustaadhi Namusoma alitangaza kuwa, amewatimua Suma na meneja wake, aliyemtaja kwa jina moja la Maneno kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Kundi la Mtanashati linaundwa na wasanii wengi maarufu nchini akiwemo Dogo Janja, Amazon na PNC.

SHARO MILIONEA AMPA SHAVU ALI KIBA

MSANII nyota wa vichekesho na muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Mkieti ‘Sharo Milionea’ amerekodi wimbo mpya kwa kushirikiana na Ali Kiba.
Sharo alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, bado hajaamua kuupa jina wimbo huo.
Alisema awali, walikuwa wameupa jina wimbo huo, lakini baada ya kugundua kwamba limeshatumiwa na wasanii wengine kwenye nyimbo zao, waliamua kulifuta.
“Kwa sasa nasubiri kikao na viongozi wangu ili wanisaidie kupendekeza jina la wimbo huo,”alisema msanii huyo.
Kwa mujibu wa Sharo, iwapo atapendekeza jina la wimbo huo peke yake, huenda lisiwe na mvuto kwa mashabiki na kusababisha apoteze mwelekeo.
Msanii huyo alisema ameamua kumshirikisha Kiba katika wimbo huo kutokana na ukali wake katika fani ya muziki na pia kukubalika na mashabiki.
Alisema kiba ni mmoja wa wasanii nyota nchini katika muziki wa kizazi kipya, hivyo anaamini kwa kushirikiana naye kuimba wimbo huo, utakuwa na mvuto zaidi kwa mashabiki.
Kwa sasa, Sharo anatamba na kibao chake cha ‘Chuki ni Bure’ ambacho amemshirikisha nyota mwingine wa muziki huo nchini, Dully Sykes.
Sharo amewaomba mashabiki wake waendelee kumuunga mkono katika kazi zake ili naye aweze kupata morari ya kufanya vizuri zaidi kwenye gemu.

GENEVIEVE AVISHWA PETE YA UCHUMBA

LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nigeria, Genevieve Nnaji amevishwa pete ya uchumba na anatarajia kufunga ndoa hivi karibuni.
Habari za kimtandao zimeeleza kuwa, tayari Genevieve ameshavishwa pete ya uchumba na mumewe mtarajiwa hivi karibuni.
Hata hivyo, Genevieve hayupo tayari kumtaja mchumba wake huyo kwa madai kuwa, anataka kuwashangaza mashabiki wake.
Genevieve amekaririwa kupitia akaunti yake ya twitter wiki hii akisema kuwa, baada ya muda si mrefu anatarajia kuitwa ‘mke wa mtu’.
“Natarajia kuitwa mke hivi karibuni,” alisema msanii huyo kupitia kwenye mtandao huo.
Genevieve, ambaye ni mama wa mtoto mmoja pia aliandika kwenye mtandao huo maneno yasemayo: “busu maalumu kwa ajili yako.”
Mwanadada huyo mwenye sura yenye mvuto pia aliweka picha yake kwenye mtandao huo, ikimuonyesha akiwa amevaa pete ya uchumba.
Msanii huyo amekuwa akitajwa kuwa na uhusiano wa mapenzi na mwanamuziki maarufu wa Nigeria, D’Banj.
Hata hivyo, wote wawili wamekuwa wakikanusha mara kwa mara taarifa hizo na kudai kuwa, uhusiano wao ni wa kawaida, kama ule wa kaka na dada.

KALALA: NIMERUDI NYUMBANI

MWIMBAJI nyota wa zamani wa bendi ya Mapacha Watatu, Kalala Junior amesema ameamua kurejea Twanga Pepeta kwa vile bendi hiyo ni kama nyumbani kwake.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Kalala alisema amefurahi kuona kuwa amepokelewa vyema na wanamuziki wa bendi hiyo na kumpa ushirikiano mkubwa.
Kalala amejiunga na Twanga Pepeta, akitokea kundi la Mapacha Watatu, ambalo alishiriki kulianzisha mwaka jana akiwa na Jose Mara na Khalid Chokoraa.
Wakati alipotangaza kujitoa Mapacha Watatu miezi miwili iliyopita, mwanamuziki huyo alisema anataka kumpumzika kwa muda, hali iliyosababisha kuwepo na hisia kwamba, huenda alitaka kujiunga na bendi ya Mashujaa.
Kalala anatarajiwa kutambulishwa rasmi kesho wakati Twanga Pepeta itakapofanya onyesho kwenye ukumbi wa Mango Garden uliopo Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika onyesho hilo, Kalala anatarajiwa kutambulisha kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la Nyumbani ni nyumbani.
Kalala amejigamba kuwa, amepania kuwapa mashabiki wa bendi hiyo vitu vipya, ambavyo walikuwa wakivikosa kwa muda mrefu.
“Nimerudi Twanga Pepeta nikiwa na vitu vipya, ambavyo nitaanza kuvionyesha siku ya utambulisho,”alisema mwimbaji huyo, ambaye ni mtoto wa mkongwe wa muziki nchini, Hamza Kalala.
Kalala alitambulishwa rasmi na uongozi wa Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET) katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika wiki iliyopita.
Wakati wa utambulisho huo, Kalala aliwaambia waandishi wa habari: “Koti lilikuwa linanibana nilipokuwa Mapacha Watatu, nimeamua kulivua na kuacha kuendelea kulivaa.”
Kalala alisema amefurahi kujiunga tena na Twanga Pepeta na kuongeza kuwa, amekuja na zawadi ya nyimbo mbili, wa kwanza ukiwa Nyumbani ni Nyumbani, ambao unaelezea mambo aliyokutana nayo katika maisha yake kimuziki.
Mwimbaji huyo mwenye makeke alisema uamuzi wake wa kurejea Twanga Pepeta haukutokana na kulazimishwa, bali mapenzi yake mwenyewe, hasa akikumbuka fadhila alizopata kutoka ASET.
“Nawaomba wadau wa Twanga Pepeta wakae mkao wa kula kwani nimerejea kivingine na watarajie kupata mambo mengi mazuri,” alisema Kalala.
“Nitafanya zaidi ya yale niliyoyafanya zamani, lengo ni kuendelea kushika hatamu katika muziki wa dansi,” aliongeza mwimbaji huyo, ambaye vionjo vyake vimewashika mashabiki wengi wa muziki wa dansi nchini.
Ofisa Habari wa ASET, Mohamed Pizaro alisema ujio wa Kalala katika bendi hiyo umetokana na mpango wao waliouanzisha unaojulikana kwa jina la ‘Amsha Amsha Twanga Pepeta Nyumbani ni Nyumbani’.
Pizaro alisema wamempokea Kalala kwa roho moja na kwamba Twanga Pepeta ni chimbuko la watu na hivyo akitoka mtu ni lazima arudi, kutokana na raha na burudani za bendi hiyo.
Alisema Kalala amepokelewa kwa mikono miwili na wana imani kubwa kwamba watashirikiana naye ipasavyo kuifanya bendi hiyo izidi kunoga.

WOLPER SASA KUTENGENEZA FILAMU ZAKE



BAADA ya kucheza filamu za wasanii wenzake kwa muda mrefu, hatimaye mwanadada Jacqueline Wolper ameamua kuanzia sasa kuandaa filamu zake mwenyewe.
Mtandao wa filamucentral ulimkariri Wolper akisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, ataandaa filamu hizo kupitia kampuni ya JB Production.
Msanii huyo mwenye umbo na sura jamali alisema, atafanyakazi hiyo kwa kushirikiana na meneja wake, Leah Mwendamseke ‘Lamata’.
Wolper alisema tayari ameshaanza kuandaa filamu yake ya kwanza itakayojulikana kwa jina la Malipo.
Mwanadada huyo alisema ameamua kujitosa kwenye fani hiyo kwa lengo la kuongeza ujuzi na kipato.
Alisema ana hakika filamu yake hiyo mpya itawasisimua mashabiki kutokana na mvuto wa hadithi na waigizaji, ambao alisema wameigiza kwa kiwango cha juu.
“Mara nyingi ninapopanga kufanya kitu fulani, lazima nihakikishe nakimaliza kwa asilimia mia moja,” alisema msanii huyo mwenye mvuto.
Aliongeza:” Kwa vile nimeingia mzigoni kwa dhamira moja, nawaomba mashabiki wajiandae kushuhudia maajabu kutoka katika kampuni yangu mpya ya kutengeneza filamu.”
Aliwataja baadhi ya wasanii walioshiriki kucheza filamu yake hiyo mpya kuwa ni Blandina Chagula ‘Johari’, Stanley Msungu ‘Seneta’, Hashim Kambi ‘Ramsey’, Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’, Ahmed Ulotu ‘Mzee Chilo’.
Wolper alisema tangu alipojitosa kwenye fani hiyo, watayarishaji na waongozaji wa filamu wamekuwa wakimkubali kutokana na uwezo wake mkubwa katika uigizaji.
Msanii huyo aliendelea kutetea msimamo wake kuhusu mavazi wanayotumia wasanii wa kike kwenye filamu kwamba hayana matatizo.
Alisema mara nyingi mavazi yanategemea sehemu husika hata kama mtu akiwa nyota, huwezi kwenda kanisani na kimini.
“Sehemu ambazo hazistahili kwa mavazi yaliyo tofauti, unatakiwa kuvaa vazi linalostahili na inafikia mahali lawama inawaangukia sana wasanii wakionekana kama ndivyo wavaavyo,”alisema.
Wolper alisema ni vigumu kwa mtu kwenda katika maonyesho ya muziki wa disco akiwa amevaa mavazi yasiyoendana na sehemu hiyo.
Hivi karibuni, Wolper alibadili dini na kuitwa Ilham baada ya kupata mchumba muislam aliyemtaja kwa jina la Dulla ‘Dallas’, ambaye alimnunulia gari sambamba na kumboreshea maisha.
Wolper ni mmoja wa wasanii wanaomiliki magari ya kifahari. Anamiliki magari mawili, Toyota Harrier Lexus lenye thamani ya sh. milioni 25 na Toyota Noah lenye thamani ya sh. milioni 18, ambalo analitumia kwenye kazi za filamu.

BANDARI KENYA YAIBANDUA COASTAL UNION

Na Sophia Wakati, Tanga

KIBARUA cha makocha Juma Mgunda na Habibu Kondo leo kimezidi kuwa hatarini baada ya timu yao ya Coastal Union kuchapwa mabao 2-0 na Bandari ya Tanga katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini hapa.

Wachezaji wa Tanzania wanaocheza soka ya kulipwa Bandari ndio walioifungia mabao hayo mawili, la kwanza likiwa limefungwa na David Naftali na la pili na Thomas Maurice.

Mechi hiyo ilikuwa ya pili mfululizo kwa Coastal Union mbele ya mashabiki wake, ambao walionekana kuwa na hasira wakati wa mchezo huo kutokana na timu yao kuonyesha kiwango duni cha soka.

Katika mechi yake nyingine ya kirafiki iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, Coastal Union ilichapwa mabao 2-1 na Polisi Morogoro kabla ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro.

Coastal Union inatarajiwa kushuka tena dimbani Jumamosi kumenyana na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

NGASA, AKUFFOR WAIBEBA SIMBA

Na Shaaban Mdoe, Arusha
MABINGWA wa soka nchini Simba leo wameendelea kudhihirisha jinsi kikosi chao kilivyo moto baada ya kuichapa JKT Oljoro mabao 2-1 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Arusha.

Ushindi huo ulikuwa wa pili mfululizo kwa Simba katika kipindi cha siku nne. Mwishoni mwa wiki iliyopita, Simba iliilaza Mathare United mabao 2-1 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye uwanja huo.
Mshambuliaji Mrisho Ngasa alikuwa miongoni mwa wachezaji walioifungia Simba mabao hayo mawili, likiwa bao lake la kwanza tangu aliposajiliwa na mabingwa hao msimu huu akitokea Azam FC.

Bao la pili la Simba lilifungwa na mshambuliaji mpya kutoka Ghana, Daniel Akuffor, likiwa bao lake la pili tangu alipoanza kuichezea timu hiyo.

Akuffor aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 25 baada ya kuunganisha wavuni pasi ya Ngasa kabla ya Ngasa kuongeza la pili dakika ya 76 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Abdalla Juma.

Oljoro JKT ilipata bao la kujifariji dakika ya 89 lililofungwa kwa njia ya penalti na Markus Mpangala baada ya beki Paschal Ochieng wa Simba kumuangusha mchezaji huyo ndani ya eneo la hatari.

SERIKALI YABWAGWA KESI YA MINTANGA, MAHAKAMA KUU YAFUNGA USHAHIDI

Na Furaha Omary
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeamua kufunga ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Rais wa zamani wa Shirikisho la Ngumi za Radhaa Tanzania (BFT), Alhaji Shaaban Mintanga, baada ya kushindwa kuleta mashahidi watano kutoka nchini Mauritius kwa muda mrefu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Dk. Fauz Twaib anayesikiliza kesi hiyo, baada ya kukubaliana na ombi la jopo la mawakili waomtetea Alhaji Mintanga la kuiomba kufanya hivyo kwa mamlaka iliyokuwa nayo kwa mujibu wa sheria.
Alhaji Mintanga jana aliwakilishwa na mawakili Berious Nyasebwa, Aliko Mwamanenge na Jerome Msemwa huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila na Wakili wa Serikali, Hamidu Mwanga.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Dk. Twaib alisema kwa muda wa vipindi vinne vya mahakama, upande wa Jamhuri umeshindwa kuleta mashahidi na kila mara umekuwa ukitoa hoja za kuomba kuahirishwa, ukosefu wa fedha, unafanya mawasiliano na kutumwa ofisa Mauritius na pia kwa vipindi hivyo umekuwa ukileta mawakili tofauti.
Jaji Dk. Twaib alisema alichobaini katika kesi hiyo ni ucheleweshwaji wa muda wa mahakama na kwamba Jamhuri walikuwa na muda mwingi wa kufanya yale waliyotaka kuyafanya.
Pia alisema kuna uzembe kwani upande wa Jamhuri kwa kupitia ofisi ya DPP ilikuwa inajua ilipaswa kumshauri Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kufuata taratibu za kumhoji mtu ambaye yupo nje.
"Kutokana na mazingira hayo, nimejiuliza mimi kama Jaji nitafanya nini, hivyo kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu namba 264 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ambayo inaongoza mwenendo wa mashauri ya jinai, ninaona ni vema kukubaliana na hoja za upande wa utetezi na kuamua kufunga ushahidi wa upande wa Jamhuri kwa kutoleta mashahidi kwa muda uliopangwa," alisema na kuutaka upande wa utetezi kuendelea na kesi kwa upande wao.
Awali, akianza kusoma uamuzi huo, Jaji Dk. Twaib alisema mshitakiwa Alhaji Mintanga anakabiliwa na mashitaka mawili ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya, ambayo amekana na upande wa Jamhuri ulitoa orodha ya mashahidi 29 ambao watano kati yao wapo nchini Mauritius.
Jaji huyo alisema Wakili wa Serikali Stella Machaku alifika mahakamani hapo na kueleza kuwa watatoa mashahidi tisa tu na kwamba wakati wa usikilizwaji, walitoa wanne na kubaki watano, ambao wapo nchini Mauritius.
Alisema kesi hiyo ilipangwa Februari, 2012 hata hivyo upande wa Jamhuri uliomba kuahirisha tena shauri hilo kwa kuwa hawana mashahidi na hivyo kupangwa Juni, 2011, ambapo tena waliomba ahirisho kwa madai Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) amewasiliana na maofisa wa serikali Mauritius kuona uwezekano wa kuwaleta mashahidi hao.
Pia alisema upande wa Jamhuri ulidai Mahakama Kuu haina fedha za kuwaleta mashahidi nao na kwamba ikishindikana watatoa ushahidi kwa njia ya video wakiwa Mauritius.
Jaji Dk. Twaib alisema shauri hilo lilipangwa Julai, mwaka huu, ambapo halikuendelea kwa kuwa alikuwa na majukumu mengine na hivyo kuahirishwa kwa takriban miezi miwili na nusu hadi Agosti 28, mwaka huu.
Alisema kesi hiyo ilipotajwa Agosti 28, mwaka huu, Wakili wa Serikali Mkuu, Arafa Msafiri akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila waliomba kuahirishwa kwa shauri hilo kwa madai Agosti 23, mwaka huu, DPP alimtuma ofisa wake kwenda Mauritius.
Hata hivyo, mawakili wa utetezi walipinga ombi hilo kwa madai kama upande wa Jamhuri umeshindwa kuleta mashahidi hao, ambao watatu ni Watanzania (mabondia wanaodaiwa kukutwa na dawa hizo) na wawili ni raia wa Mauritius, basi ufunge ushahidi wao na pia mahakama itumie mamlaka iliyonayo kufunga ushahidi ili waendelee na kesi kwa upande wao.
Pia mawakili hao walidai sheria ipo wazi kwamba mahakama haiwezi kutoa uamuzi bila ya kuwepo kwa vielelezo vya nakala ya barua iliyopelekwa Mauritius na tiketi ya ofisa huyo aliyetumwa.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Wakili wa utetezi Msemwa aliiomba mahakama wawasilishe hoja zao za kisheria iwapo wanaona mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la.
Jaji Dk. Twaib aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 7, mwaka huu, ambapo upande wa Jamhuri na wa utetezi utawasilisha hoja hizo kabla ya mahakama kutoa uamuzi iwapo inaona Alhaji Mintanga ana kesi ya kujibu au la.
Mintanga anakabiliwa na mashitaka mawili ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 4.8 kutoka nchini Tanzania kwenda nchini Mauritius. Dawa hizo zinadaiwa kuwa na thamani ya sh. milioni 120.

MTANZANIA AOMBEWA ITC UJERUMANI

CHAMA cha Soka cha Ujerumani (DFB) kimetuma maombi ya kupatiwa hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Robert Makanja. DFB imetuma maombi hayo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kumwezesha mchezaji huyo kuichezea timu ya TUS Ahausen, Hessischer FuBall-Verband ya Ujerumani.
Hata hivyo, DFB haikueleza timu hiyo inashiriki ligi ya daraja gani nchini humo. Wambura alimkariri Mkuu wa Mashindano wa DFB, Markus Stenger akisema kuwa, Mtanzania huyo ameombewa hati hiyo kama mchezaji wa ridhaa kwa maelezo kuwa hakuwahi kusajiliwa na klabu yoyote nchini.

Alisema TFF inayafanyia kazi maombi hayo na hati hiyo itatolewa mara baada ya taratibu husika kukamilika, ikiwemo kubaini kama kweli mchezaji huyo hakuwahi kusajiliwa na klabu yoyote hapa nchini.

SERENGETI BOYS SASA KUIVAA MISRI

TIMU ya soka ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) sasa itaivaa Misri katika raundi ya pili ya michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika.
Awali, Serengeti Boys ilipangwa kumenyana na Kenya katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo iliyotarajiwa kuchezwa Septemba 9 mwaka huu kabla ya nchi hiyo kutangaza kujitoa.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), limetuma taarifa ya kujitoa kwa Kenya.
Kwa mujibu wa Wambura, pambano la awali kati ya Serengeti Boys na Misri litachezwa Oktoba 14 mwaka huu mjini Dar es Salaam na la marudiano kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu nchini Misri.
Mshindi wa mechi hizo mbili atafuzu kucheza raundi ya tatu, ambayo itakuwa ya mwisho kabla ya kwenda Morocco katika fainali zitakazochezwa mwakani.
Katika raundi ya tatu, ambayo mechi zake zitachezwa katikati ya Novemba na za marudiano mwishoni mwa mwezi huo, mshindi kati ya Tanzania na Misri atacheza na mshindi wa mechi kati ya Congo Brazzaville na Msumbiji.

Wachezaji wanaounda kikosi cha Serengeti Boys chini ya Kocha Jakob Michelsen ni makipa Abdallah Bakar (Mjini Magharibi), Hamad Juma (Azam) na Peter Manyika (JKT Ruvu).

Mabeki ni Abdallah Salum (Mjini Magharibi), Basil Seif (Morogoro), Hassan Mganga (Morogoro), Ismail Gambo (Azam), Mgaya Abdul (Azam), Miraji Selemani (Polisi Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni), Mohamed Hussein (Azam), Pascal Matagi (Dodoma) na Paul James (Kinondoni).

Viungo ni Farid Musa (Kilimanjaro), Hussein Twaha (Coastal Union), James Mganda (Kipingu Academy), Mbwana Ilyasa (Simba), Mohamed Haroub (Zanzibar), Mohamed Kapeta (Kinondoni), Mudathiri Yahya (Azam), Mzamiru Said (Morogoro) na Selemani Bofu (JKT Ruvu).

Washambuliaji ni Abdallah Kisimba (Mwanza), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Joseph Lubasha (Azam), Kelvin Friday (Azam) na Salvatory Nkulula (Kipindu Academy).

TUSKER KUDHAMINI KOMBE LA CHALENJI KWA MIL 700

Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye akipokea kombe la ubingwa wa michuano ya Tusker Chalenji, Mkurugenzi wa Masoko wa Uganda Breweries, Lemmy Mutahi.


Meneja Masoko wa Uganda Breweries, Lemmy Mutahi (katikati) akimkabidhi mfano wa hundi ya pesa kwa Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye. Kulia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA), Livingstone Kyambadde.


Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye akitaniana na mwasisi wa baraza hilo, Kezekia Ssegwanga Musisi wa Uganda kabla ya makabidhiano ya mkataba wa michuano ya Kombe la CECAFA- Tusker Chalenji Cup 2012 kwenye hoteli ya Serena mjini Kampala, Uganda juzi.


Tuesday, August 28, 2012

KESI YA LULU YAENDELEA KUPIGWA KALENDA

KESI ya tuhuma za mauaji inayomkabili msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael au ‘Lulu’ imeendelea kupigwa kalenda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Msanii huyo anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba, alipandishwa kizimbani jana mahakamani hapo, kesi hiyo ilipotajwa.
Wakili wa Serikali Leonard Chalo alidai mbele ya Hakimu Mkazi Augustino Mbando, kuwa shauri hilo limekuja kwa kutajwa.
Hata hivyo, Hakimu huyo alisema jalada la kesi hiyo lipo mahakama ya juu ambapo alitaka kujua hatua iliyofikiwa kuhusu suala la mshitakiwa huyo kutotakiwa kupandishwa kizimbani mahakamani hapo.
Wakili wa utetezi Peter Kibatala alidai ameshawasiliana na Hakimu Mkazi Mfawidhi Ilvin Mugeta ambaye alimweleza kwamba ataandika barua kwenda Mahakama Kuu kuelezea sababu za Lulu kufikishwa Kisutu.
Hakimu huyo aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 10, mwaka huu kwa kutajwa.
Baada ya Lulu kupandishwa kizimbani Mahakama ya Kisutu, mawakili wake waliwasilisha maombi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kuomba kufanya uchunguzi wa umri wa mshitakiwa huyo.
Jaji Dk. Fauz Twaib aliyepangiwa kusikiliza maombi hayo alikubali mahakama hiyo kufanyia uchunguzi umri wa Lulu na kuamuru mshitakiwa huyo kutopelekwa Kisutu bali awe anafikishwa Mahakamani hapo.

SIMBA KUJIPIMA NA JKT OLJORO KESHO

Simba itacheza mechi ya kirafiki na timu ya soka ya Oljoro JKT katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta jijini Arusha kesho.

Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Ligi Kuu ya Tanzania inayotarajiwa kuanza baadaye mwezi ujao.

Hii itakuwa mechi ya pili ya kirafiki ya Simba kucheza jijini Arusha baada ya ile ya juzi dhidi ya Mathare United ya Kenya.

Oljoro JKT imetoka kwenye michuano ya timu za majeshi hapa nchini ambapo ilichukua nafasi ya kwanza pamoja na Ruvu JKT.

Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema atatoa nafasi kwa wachezaji wengi kwa kadri itakavyowezekana kwenye pambano hilo.

Viingilio vitakuwa ni Sh 5,000 kwa VIP A, Sh 3,000 kwa VIP B na Sh 2000 kwa VIP C. Kiingilio kwa watoto kitakuwa sh 1000.

SUNZU AFIWA NA DADA YAKE

Mshambuliaji Felix Mumba Sunzu ameondoka nchini leo kwenda Lubumbashi, DRC kuhudhuria msiba wa dada yake, ambaye alifariki dunia juzi jioni nchini humo.

Dada huyo alikuwa amekwenda kumtembelea mdogo wa Sunzu, Stopila, ambaye anachezea klabu ya soka ya TP Mazembe siku sita zilizopita, lakini akakumbwa na umauti kutokana na ugonjwa wa malaria iliyopanda kichwani (Cerebral Malaria).

Uongozi wa Simba umetoa pole kwa familia ya Sunzu pamoja na kufanikisha kuondoka kwa haraka kwa mchezaji huyo ili akaungane na familia yake.

Sunzu atarejea nchini baada ya kumaliza maziko na klabu ya Simba inaomba vyombo vya habari na wadau wengine kumpa nafasi ya kuomboleza msiba huu mzito kwake binafsi, kwa familia yake na Simba.

Mola na aiweke roho ya marehemu mahali pema. Amen

HATMA YA YONDANI, MBUYU J'PILI

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu) kupitia usajili wa wachezaji kwa msimu wa 2012/2013.

Usajili utakaopitiwa ni wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Lidi Daraja la Kwanza (FDL) ambapo Kamati itapitia pingamizi zilizowasilishwa na klabu mbalimbali dhidi ya wachezaji waliosajiliwa na klabu zingine.

SERENGETI BOYS, KENYA KUCHEZA AZAM COMPLEX

Mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania tiketi ya kucheza Fainali za 10 za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwakani nchini Morocco kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Kenya itachezwa Septemba 9 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.

Tayari Serengeti Boys chini ya Kocha Jakob Michelsen na Msaidizi wake Jamhuri Kihwelo ikiwa na wachezaji 28 iko kambini jijini Dar es Salaam tangu jana (Agosti 27 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoanza saa 10 kamili jioni.

Wachezaji waliko kambini ni makipa Abdallah Bakar (Mjini Magharibi), Hamad Juma (Azam) na Peter Manyika (JKT Ruvu). Mabeki ni Abdallah Salum (Mjini Magharibi), Basil Seif (Morogoro), Hassan Mganga (Morogoro), Ismail Gambo (Azam), Mgaya Abdul (Azam), Miraji Selemani (Polisi Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni), Mohamed Hussein (Azam), Pascal Matagi (Dodoma) na Paul James (Kinondoni).

Viungo ni Farid Musa (Kilimanjaro), Hussein Twaha (Coastal Union), James Mganda (Kipingu Academy), Mbwana Ilyasa (Simba), Mohamed Haroub (Zanzibar), Mohamed Kapeta (Kinondoni), Mudathiri Yahya (Azam), Mzamiru Said (Morogoro) na Selemani Bofu (JKT Ruvu).

Washambuliaji ni Abdallah Kisimba (Mwanza), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Joseph Lubasha (Azam), Kelvin Friday (Azam) na Salvatory Nkulula (Kipindu Academy).

Mechi ya marudiano itachezwa jijini Nairobi, Kenya kati ya Septemba 21, 22 na 23 mwaka huu. Timu itakayofanikiwa kusonga mbele itacheza raundi ya pili dhidi ya Misri. Mechi ya kwanza itachezwa nyumbani kati ya Oktoba 12, 13 na 14 mwaka huu wakati ya marudiano itakuwa kati ya Oktoba 26, 27 na 28 mwaka huu.

Misri ni kati ya timu 17 zilizoingia moja kwa moja raundi ya pili. Nyingine ni Afrika Kusini, Algeria, Burkina Faso, Cameroon, Congo Brazzaville, Cote d’Ivoire, Gabon, Gambia, Ghana, Guinea, Mali, Rwanda, Senegal, Sierra Leone, Tunisia na Zambia.

Monday, August 27, 2012

YANGA YAREJEA DAR KUTOKA RWANDA

Baadhi ya wachezaji wa timu ya soka ya Yanga wakiwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam mara baada ya kurejea nchini kutoka Rwanda walikokwenda kwa ziara ya mechi mbili za kirafiki kwa mwaliko wa Rais Paul Kagame wa nchi hiyo. (Picha na Emmanuel Ndege wa blogu ya liwazozito na rusha roho)

ATONG, MREMBO WA SUDAN KUSINI ALIYETWAA TAJI LA MREMBO WA AFRIKA

MREMBO Atong Demach wa Sudan Kusini mwishoni mwa wiki iliyopita aliushangaza ulimwengu baada ya kutawazwa kuwa mrembo wa Afrika katika shindano la dunia lililofanyika katika mji wa Ordos uliopo kaskazini mashariki mwa China.
Atong alitwaa taji hilo ikiwa ni mara ya kwanza kwa Sudan Kusini kushiriki katika shindano hilo baada ya kujitenga na Sudan mwaka jana na kuwa nchi huru.
Katika shindano hilo lililowashirikisha warembo zaidi ya 100 kutoka katika nchi mbali mbali duniani, Wenxia Yu wa China alitawazwa kuwa mrembo mpya wa dunia 2012.
Wenxia alivishwa taji hilo na mrembo wa dunia wa mwaka 2011, Ivian Sarcos wa Venezuela. Lilikuwa taji la 62 tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 1951.
Akiwa anaiwakilisha nchi yake kwa mara ya kwanza, Atong aliwashangaza mashabiki wa fani ya urembo duniani kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha katika mashindano ya hatua za awali.
Mbali na kutwaa taji la Afrika, mrembo huyo, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 24 pia alitwaa taji la mwanamitindo bora, ambalo ni miongoni mwa mataji madogo yanayoshindaniwa katika shindano hilo.
Atong aliteka hisia za watamazaji wakati wa shindano la mwanamitindo bora lililofanyika kwenye uwanja wa Dongsheng, ambapo alipendeza mno kwa mavazi, miondoko yake, mwonekano wake na pozi zake za picha.
Atong alikuwa miongoni mwa warembo 15 waliotinga hatua ya nusu fainali, akiwa na washiriki wenzake kutoka katika nchi za Kenya, Indonesia, Netherlands, USA, Philippines, Spain, Brazil, England, Wales, China, Jamaica, Australia, Mexico na India. Baadaye alitinga hatua ya fainali, akiwa na washiriki wenzake saba.
Mbali na Atong, warembo wengine waliotinga nusu fainali ya shindano hilo walitoka nchi za Jamaica, India, Australia, Brazil, China PR na Wales.
Kutinga hatua ya fainali kwa mrembo huyo ndiko kulikovuta hisia za watazamaji wengi wa shindano hilo, ambao walianza kufuatilia nchi anayoiwakilisha.
Sudan Kusini imeungana na nchi zingine kadhaa kutwaa taji la mrembo wa Afrika katika shindano hilo, ambapo Afrika Kusini inaongoza kwa kulitwaa mara 11.
Mwaka jana, taji hilo lilinyakuliwa na Bokang Montjane wa Afrika Kusini, ambapo pia alitinga fainali ya shindano la dunia. Mwaka 2010, taji hilo lilinyakuliwa na Emma Wareus wa Botswana.
Atong ni mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika Chuo Kikuu cha Juba, kilichopo mjini Juba. Moja ya malengo yake ya baadaye ni kuwasaidia watu wenye matatizo, hasa watoto na pia kuwa mtetezi wa uhifadhi wa mazingira.
Binti huyo kutoka mji wa Bor uliopo kando kando ya Mto Nile alisema kabla ya shindano hilo: “Naona fahari kuiwakilisha nchi yangu kwa mara ya kwanza katika shindano la dunia na najivunia urembo wenye malengo.”
Sudan Kusini inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni nane. Uamuzi wake wa kujitenga na Sudan ulitokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka kadhaa na kusababisha vifo vya maelfu ya watu wasiokuwa na hatia.
Ushindi wa taji la urembo la Afrika uliotwaliwa na Atong ni miongoni mwa mafanikio kadhaa, ambayo nchi hiyo inayatarajia katika miaka michache ijayo.
Shindano la kumsaka mrembo wa dunia liliasisiwa na Eric Morley mwaka 1951, likiwashirikisha wasichana 26 wa Uingereza.
Kwa sasa, shindano hilo linaendeshwa na Julia Morley, mke wa Eric, ambaye alifariki dunia mwaka 2000. Nchi 130 hushiriki katika shindano hilo kila mwaka.
Mwaka 2001, mrembo wa Nigeria, Agbani Darego alifanikiwa kutwaa taji la mrembo wa dunia na mwaka uliofuata, shindano hilo lilifanyika katika mji wa Abuja nchini humo.

MASHABIKI RWANDA WAGOMBEA JEZI ZA YANGA





Baadhi ya mashabiki wa soka wa Rwanda mwishoni mwa wiki iliyopita walijikuta wakigombea jezi zenye nembo ya klabu ya Yanga zilizokuwa zikigawiwa kwenye uwanja wa Amahoro wakati wa mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Yanga na Polisi. Katika pambano hilo, Yanga iliichapa Polisi mabao 2-1. Picha hizi zimepigwa na Saleh Ally, Mhariri kiongozi wa gazeti la Champion.

KOMBAINI COPA COCA COLA YAENDA AFRIKA KUSINI

Kombaini ya Copa Coca-Cola Tanzania (Dream Team) yenye wachezaji 16 inatarajia kuondoka kesho (Agosti 28 mwaka huu) asubuhi kwenda Afrika Kusini kwenye kambi itakayokuwa chini ya makocha wa Chelsea.

Makocha watano kutoka timu ya Chelsea ya Uingereza ndiyo watakaoongoza kambi maalumu ya kimataifa ya Copa Coca-Cola yenye wachezaji 140 kutoka nchini 15 itakayofanyika jijini Pretoria kuanzia Agosti 28 hadi Septemba 8 mwaka huu.

Robert Luke Udberg, Russel William Banyard, Oliver Staurt Woodall, Shane Jason Hughes na Dean Aaron Steninger kutoka Chelsea FC Foundation ndiyo wanaounda jopo hilo la makocha litakalowanoa vijana hao wenye umri chini ya miaka 17.

Wachezaji wanaounda Dream Team iliyotokana na michuano ya Copa Coca-Cola iliyofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 24 hadi Julai 15 mwaka huu ni Abrahman Said Mohamed (Zanzibar), Ayubu Alfan (Dodoma), Baker Hamad (Tanga), Edward Joseph (Ruvuma), Hassan Kabunda (Temeke) na Joseph Chidyalo (Dodoma).

Wengine ni Mtalemwa Katunzi (Morogoro), Mwarami Maundu (Lindi), Nankoveka Mohamed (Ilala), Nelson Peter (Morogoro), Rajab Rashid (Mwanza), Said Ramadhan (Kagera), Shiza Kichuya (Morogoro), Shukuru Msuvi (Temeke), Tanganyika Suleiman (Kigoma) na Tumaini Baraka (Kilimanjaro).

Nchi nyingine zitakazokuwa na washiriki katika kambi hiyo ni wenyeji Afrika Kusini, Burundi, Cameroon, Congo Brazzaville, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Swaziland, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Hii ni mara ya sita mfululizo kwa kampuni ya Coca-Cola kupeleka Dream Team kwenye kambi za kimataifa. Mwaka 2007 na 2008, timu hiyo ilikwenda Brazil wakati mwaka 2009, 2010 na 2011 ilikuwa Afrika Kusini.