KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 30, 2012

NIZAR KHALFAN AIBEBA YANGA, YAICHARAZA AFRICAN LYON 3-1


YANGA leo imeendelea kuchanja mbuga katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuicharaza African Lyon mabao 3-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Nizar Khalfan ndiye aliyeibeba Yanga baada ya kuifungia mabao mawili katika kipindi cha pili. Nizar aliingia kipindi hicho kuchukua nafasi ya Frank Domayo.
Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao katika kipindi cha kwanza lililofungwa na mshambuliaji Didier Kavumbagu. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Benedicto Mwalangali aliisawazishia African Lyon dakika za mwanzo za kipindi cha pili kabla ya Nizar kufunga la pili na kuongeza la tatu.

Matokeo hayo yameiwezesha Yanga kushika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi saba baada ya kucheza mechi nne.
Simba inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi nne, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 10 na Coastan Union yenye pointi saba, sawa na Yanga.

KUZIONA SIMBA NA YANGA BUKU TANO


Kiingilio cha chini kwenye mechi ya Yanga na Simba itakayochezwa Jumatatu (Oktoba 3 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648 kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000.
Mechi hiyo namba 80 ya Ligi Kuu ya Vodacom itachezwa kwenye uwanja huo kuanzia saa 11 kamili jioni. Watazamaji watakaotaka kuona mechi hiyo wakiwa wameketi kwenye viti vya rangi ya bluu ambavyo ni 17,045 watalipa sh. 7,000 kwa tiketi moja.
Viingilio vingine kwenye mechi hiyo ni sh. 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 wakati VIP C inayochukua watazamaji 4,060 itakuwa sh. 15,000. Kwa upande wa VIP B tiketi ni sh. 20,000 na VIP A yenye watazamaji 748 tu kiingilio kitakuwa sh. 30,000.

VODACOM YAMALIZANA NA KLABU ZA LIGI KUU


Kufuatia kukaa katika kikao cha majadiliano kati ya Mdhamini mkuu wa ligi kuu Vodacom Tanzania, kamati ya ligi, TFF na vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo, Mashabiki na wapenzi wa soka nchini wameondolewa hofu juu ya udhamini wa ligi inayoendelea hivi sasa.

Mdhamini mkuu wa ligi hiyo Vodacom Tanzania, imekubali kuendelea kuunga mkono ligi hiyo na kuwaomba mashabiki wa soka kutegemea msimu mzuri wa ligi mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa, amesema kuwa mvutano ambao umekuwepo baina ya baadhi ya Vilabu vya soka na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na wadhamini sasa yamepatiwa ufumbuzi.
“Kulikuwa na sinto fahamu kati ya Klabu za ligi kuu TFF na sisi kama wadhamini, tulikaa kikao siku ya ijumaa na wadau wote wa ligi na sasa mambo yote yamewekwa katika msitari,” alisema Kelvin na kuongeza kuwa “ Tumedhamiria kuendelea kuiunga mkono Ligi kuu ya Vodacom hatukuwa na matatizo yoyote katika kusaini mkataba na kamati ya ligi ni ufafanuzi tu ndio ulihitajika ili kuwekana sawa,” alisema Twissa.
Kuhusiana na kutolewa kwa fedha za udhamini na uendeshaji wa ligi na udhamini wa kampuni pinzania twissa alisema Vodacom haizuii klabu za ligi kudhaminiwa na kampuni nyingine yoyote tofauti na zile zenye msingi wa kiushindani katika biashara na kampuni hiyo.
“Kufuatia kikao hicho na kuwa katika msitari mmoja tumekwisha toa fedha na vifaa kwa TFF na vilabu ili ligi iweze kwenda kama ilivyo takiwa,Tukiwa kama wadau katika kuunga mkono maendeleo ya soka nchini, tumeruhusu kampuni nyingine ambazo hazina upinzani wa kibiashara na sisi ili kuondoa muingiliano wa kimaslahi,” alisema.
“TFF inadhamana ya kusimamia sheria na masharti kuhusu ligi. Hatuna matatizo yoyote ya kiutendaji na TFF wala klabu yoyote” alihitimisha Twissa.
Ligi kuu ya Vodacom ilianza rasmi tarehe 15 mwezi septemba, na tutashuhudia michezo 182 kwa kushirikisha timu 14 zinazoshiriki katika ligi hiyo, zikiwemo Yanga Afrika, Kagera sugar, na Simba ambaye ndie bingwa mtetezi wa ligi kuu ya Vodacom.
Kampuni ya Vodacom imekuwa mdhamini wa ligi kuu kwa miaka mitano sasa, na imesaini mkataba mpya wa udhamini wa ligi hiyo kwa miaka mitatu na shirikisho la mpira wa miguu TFF, mkataba utakao shuhudia shirikisho hilo likipokea udhamini wa kila msimu kwa miaka mitatu mfululizo

CHEKA AMDUNDA NYILAWILA

Bondia Fransic Cheka akinyooshwa mkono juu na mmoja wa mashabiki wa Kigeni waliokuja kuangalia mpambano wake dhidi ya Karama Nyilawila Cheka alishinda katika raundi ya sita baada ya karama kusalimu amri kushoto ni Rais wa PST Emanuel Mlundwa na wa pili kulia ni mgeni rasmi Kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu Mkoa wa Dar es salaam Suleiman Kova.Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com

Saturday, September 29, 2012

SIMBA YACHANJA MBUGA, YAIUA PRISONS



SIMBA leo imezidi kuchanja mbuga katika michuano ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Prisons mabao 2-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, timu hizo zilimaliza kipindi cha kwanza zikiwa sare ya bao 1-1.
Simba ililazimika kumaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji 10 baada ya beki wake wa kushoto, Amir Maftah kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Khalid Fupi wa Prisons.
Prisons ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 10 lililofungwa na Elias Maguri kwa shuti lililombabatiza beki Juma Nyoso na kumpoteza maboya kipa Juma Kaseja.
Sunzu aliisawazishia Simba dakika ya 45 kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Mrisho Ngasa, ambaye tangu alipojiunga na klabu hiyo msimu huu, amekuwa tegemeo kubwa la timu hiyo.
Ngasa aliifungia Simba bao la pili dakika ya 55 kwa shuti dhaifu, ambalo kipa David Abdalla wa Prisons alilidaka, lakini mpira ulimpokonya na kutinga wavuni.
Kutokana na kuonyeshwa kadi nyekundu, Maftah hataichezea Simba katika mechi ijayo dhidi ya Yanga, itakayochezwa Jumatano ijayo. Nafasi yake inatarajiwa kuchukuliwa na Paul Ngelema.
Mbali na Maftah, mchezaji mwingine atakayeikosa mechi hiyo ni mshambuliaji, Emmanuel Okwi ambaye alionyeshwa kadi nyekundu wakati Simba ilipomenyana na JKT Ruvu. Okwi amefungiwa mechi tatu.
Simba imeendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi nne, ikifuatiwa na Azam yenye pointi tisa.

MHOLANZI ARITHI MIKOBA YA SAINTFIET YANGA



Makamu mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga (kushoto) akiwa na kocha mkuu mpya wa timu hiyo, Ernstud Brandts.

KLABU ya Yanga leo imeingia mkataba na kocha mpya, Ernstud Brandts kutoka Uholanzi, ambaye amechukua nafasi ya kocha wa zamani, Tom Saintfiet kutoka Ubelgiji.
Brandts ameingia mkataba wa kuinoa Yanga kwa mwaka mmoja na kibarua chake cha kwanza kinatarajiwa kuanza kesho wakati timu hiyo itakapomenyana na African Lyon.
Mechi hiyo ya ligi kuu ya Tanzania Bara, inatarajiwa kuanza saa 11 jioni na itaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini.
Brandts ametia saini mkataba huo mbele ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, Kaimu Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako na meneja mpya wa timu hiyo, Majid Saleh 'Kaburu'.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutia saini mkataba huo, Brandts alisema anafahamu wazi kuwa, jukumu alilokabidhiwa ni zito, lakini atajitahidi kadri ya uwezo wake kufanyakazi kwa bidii ili kuhakikisha Yanga inapata mafanikio.
Brandts alisema anaushukuru uongozi kwa kumuamini na kumpa kazi hiyo na kuongeza kuwa, cha muhimu ni kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi, wanachama na wachezaji.
Kabla ya kujiunga na Yanga, Brandts alikuwa kocha mkuu wa APR ya Rwanda, ambayo alikuja nayo nchini mwaka huu wakati wa michuano ya Kombe la Kagame.
Kwa upande wake, Sanga alisema wamepata kocha mjuzi na mwenye uzoefu mkubwa wa soka ya Afrika, hivyo wanaamini atawaletea mafanikio makubwa.

WANNE WAOMBEWA ITC TFF


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wanne waliokuwa wakichezea timu mbalimbali nchini.
Wachezaji hao ni Tony Ndolo aliyejiunga na KCC ya Uganda kutoka Toto Africans, Felix Amech Stanley aliyekwenda Bahla ya Oman kutoka Coastal Union, Ernest Boakye kutoka Yanga aliyejiunga na Tripoli Athletics Club ya Lebanon na Derrick Walulya aliyerejea URA ya Uganda kutoka Simba.
MKUTANO VODACOM, KLABU ZA LIGI KUU
Klabu za Ligi Kuu na mdhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom zimekutana jana (Septemba 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yalilenga kipengele ya upekee (exclusivity) kilichopo kwenye mkataba wa udhamini ambacho kitaendelea kuwepo. Klabu zilikuwa zimeomba kwa mdhamini kuangalia uwezekano wa kukiondoa.
Pande hizo zimekubaliana kuunda kamati ya pamoja kwa ajili ya kuitafutia kila klabu mdhamini binafsi kwa lengo la kuhakikisha zinashiriki kikamilifu katika ligi hiyo.
Klabu zote zimeshapata vifaa kutoka kwa Vodacom ukiondoa African Lyon ambayo ilitarajia kuchukua vifaa hivyo leo kutoka kwa mdhamini wa ligi hiyo.
MCHAKATO WA UCHAGUZI WA VIONGOZI TAFCA
Mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) unaanza rasmi Septemba 30 mwaka huu kwa uchukuaji fomu kwa wagombea.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, fomu kwa waombaji uongozi zitaanza kutolewa Septemba 30 mwaka huu, na mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu hizo ni Oktoba 4 mwaka huu.
Fomu hizo zinapatikana ofisi za TAFCA zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 alasiri. Ada ya fomu kwa waombaji wa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Katibu Msaidizi ni sh. 200,000.
Nafasi zilizobaki za Mhazini, mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ada ya fomu ni sh. 100,000. Uchaguzi wa TAFCA umepangwa kufanyika Novemba 10 mwaka huu.

15 WAJITOKEZA KUWANIA UONGOZI TWFA



Wanamichezo 15 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) utakaofanyika mwanzoni mwa mwezi ujao.
Waliochukua fomu za kuwania uenyekiti ni Lina Kessy, Isabellah Kapera na Joan Minja. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti imeombwa na Roseleen Kisiwa pekee wakati Katibu Mkuu ni Amina Karuma na Cecilia Makafu. Macky Mhango pia ni mwombaji pekee aliyeomba nafasi ya Katibu Msaidizi.
Waombaji watatu wa nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni Furaha Francis, Juliet Mndeme na Zena Chande. Nafasi ya Mhazini nayo ina mwombaji mmoja tu ambaye ni Rose Msamila.
Sophia Charles, Rahim Maguza, Telephonia Temba na Jasmin Badar Soud wao wanaomba nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho kwenye uchaguzi huo ambao utaendeshwa na Kamati ya Uchaguzi ya TWFA chini ya Ombeni Zavalla.

LEO NI SIMBA NA PRISONS LIVE DAR


MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Simba leo wanaendelea na kampeni za kuwania tena taji hilo kwa kumenyana na Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano hilo linatarajiwa kuanza saa 11 jioni na litaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini.
SuperSport imeingia mkataba na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) wa kuonyesha moja kwa moja mechi tano za ligi hiyo zitakazochezwa kwenye Uwanja wa Taifa na Chamazi, Dar es Salaam.
Kituo hicho kilianza kazi hiyo jana kwa  kuonyesha moja kwa moja mechi kati ya Azam na JKT Ruvu iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa. Katika mechi hiyo, Azam iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho wakati Yanga itakapomenyana na African Lyon kwenye uwanja huo huo. Pambano hilo pia limepangwa kuanza saa 11 jioni.
Oktoba Mosi mwaka huu, Mtibwa Sugar itashuka dimbani kwenye uwanja wa Chamazi kumenyana na Ruvu Shooting kuanza saa 10.30 jioni.
Mahasibu wa soka nchini, Simba na Yanga watashuka dimbani Oktoba 3 mwaka huu, katika pambano linalosubiriwa kwa hamu kubwa litakalofanyika kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia saa moja usiku.

Wednesday, September 26, 2012

MANJI AWACHIMBIA MKWARA MASTAA YANGA


MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji amewaonya wachezaji wasioitakia mema timu hiyo na kuwataka wafungashe virago mapema kabla ya kusubiri kutimuliwa.
Manji alitoa onyo hilo juzi alipokutana na wachezaji wa timu hiyo katika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Alisema wapo baadhi ya wachezaji, ambao kwa makusudi hawataki kujituma na hivyo kuidhoofisha Yanga, hivyo ni bora wajiondoe mapema badala ya kusubiri kuondolewa.
Manji alisema yupo tayari kumlipa mchezaji yoyote, ambaye hapendi kuendelea kuitumikia timu hiyo na atafanya hivyo bila ya kuwa na kinyongo naye.
Mwenyekiti huyo wa Yanga alisema ni bora kuwa na wachezaji wachache wenye mapenzi na moyo wa kuitumikia timu hiyo kuliko kuwa na mamluki.
Aliwataka wachezaji wa timu hiyo kubadilika kwa kujituma zaidi uwanjani ili timu hiyo iweze kufanya vizuri zaidi katika mechi zake zijazo za michuano ya ligi kuu ya Tanania Bara.
"Kama hamtaki kujituma, ama timu itafungwa kutokana na uzembe, aliyesababisha hali hiyo lazima aondoke,"alisema Manji wakati wa kikao hicho.
Kwa sasa, Yanga inashika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi nne baada ya kucheza mechi tatu. Ilianza ligi hiyo kwa kulazimishwa kutoka suluhu na Prisons mjini Mbeya, ikapigwa mweleka wa mabao 3-0 na Mtibwa mjini Morogoro kabla ya kuicharaza JKT Ruvu mabao 4-1 mjini Dar es Salaam.
Matokeo hayo yalisababisha uongozi wa klabu hiyo kusitisha mkataba wa kocha wake, Tom Saintfiet kutoka Bulgaria. Nafasi yake inashikiliwa kwa muda na aliyekuwa msaidizi wake, Fred Felix Minziro.
Yanga inatarajiwa kushuka tena dimbani Jumapili kumenyana na African Lyon kabla ya kuvaana na watani wao wa jadi Simba, Oktoba 3 mwaka huu katika mechi itakayopigwa usiku kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

YANGA YASALIMU AMRI KWA FIFA


KLABU ya Yanga imeahidi kuyafanyia kazi malalamiko ya mchezaji wake wa zamani, John Njoroge na Kocha Kostadin Papic yaliyowasilishwa kwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamepokea taarifa ya malalamiko hayo kutoka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
"Haya mambo hatukuwa tukiyajua, tumeyakuta kwa uongozi uliopita, lakini baada ya kupokea taarifa hizi, hatuna budi kuyashughulikia,"alisema.
Sanga alisema watahakikisha suala hilo linashughulikiwa kikamilifu ili kuiepusha klabu hiyo na hatari ya kufungiwa ama kushushwa daraja.
Papic amefungua mashitaka FIFA dhidi ya Yanga, akidai malimbikizo yake ya mishahara, inayokadiriwa kufika dola 12,300 za Marekani (sh. milioni 17) wakati Njoroge anatakiwa kulipwa sh. milioni 17 kutokana na klabu hiyo kukatisha mkataba wake kienyeji miaka mitatu iliyopita.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alikaririwa juzi akisema kuwa, walijaribu kuwasiliana na viongozi wa Yanga ili Papic asiwasilishe malalamiko hayo, lakini juhudi zao hizo hazikuweza kufanikiwa.
Yanga imetakiwa kuwasilisha vielelezo vyake FIFA kuhusu malalamiko hayo ya Papic, vinginevyo huenda ikakumbana na adhabu ya kushushwa daraja ama kuzuiwa kuajiri makocha wa kigeni.
Njoroge aliishtaki Yanga kwa FIFA na kushinda kesi yake iliyoamuliwa Januari mwaka huu na Kitengo cha Usuluhishi wa Migogoro cha shirikisho hilo.
Ushindi wa Njoroge unamaanisha kwamba, iwapo Yanga itashindwa kumlipa mchezaji huyo, itapokonywa pointi katika mechi zake za ligi na kushushwa daraja.

JANGWANI KUWA KITEGA UCHUMI CHA YANGA



UONGOZI wa klabu ya Yanga umepanga kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la makao makuu ya klabu hiyo lililopo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam kwa lengo la kuligeuza kuwa kitega uchumi.
Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, ukarabati wa jengo hilo utakwenda sambamba na ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa wa soka utakaokuwa na uwezo wa kuingiza watu 5,000 kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa habari hizo, tayari Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji ameshafanya mazungumzo na kundi la wazee na vijana wa klabu hiyo kwa ajili ya kupata baraka zao.
Kikao hicho kati ya Manji na wazee pamoja na vijana wa klabu hiyo kilifanyika juzi makao makuu ya klabu hiyo kabla ya mwenyekiti huyo kuzungumza na wachezaji.
Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, lengo la Manji kutaka kuligeuza jengo la Yanga kuwa kitega uchumi ni kuiongezea mapato klabu hiyo badala ya kutegemea mechi za ligi na michuano ya kimataifa.
Manji aliwaeleza wanachama hao wa Yanga kuwa, baada ya ukarabati huo kukamilika, jengo hilo litakuwa na hoteli kubwa na ya kisasa na itakuwa ikikodishwa kwa timu zingine na watu mbali mbali kwa ajili ya kuongeza mapato.
Mwenyekiti huyo alisema, hata timu yaYanga itakapokuwa ikiingia kambini kwenye hoteli, italazimika kulipia huduma za malazi na chakula, badala ya kukaa bure.
Kuna habari kuwa, tayari mkandarasi ameshapatikana na kufikia makubaliano na uongozi kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo, ambao unatarajiwa kuanza wakati wowote.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, timu ya Yanga haitakaa tena kambini kwenye jengo hilo hadi ukarabati utakapomalizika.
Habari zaidi zinasema kuwa, eneo la jengo hilo la kitega uchumi litakuwa na maegesho ya magari yasiyopungua 1,000 na kazi ya ukarabati inatarajiwa kuanza mwezi ujao.
"Manji ametuambia kwamba, baada ya ukarabati wa jengo la kitega uchumi kumalizika, mtu yeyote atakuwa na uwezo wa kupanga hoteli na kutumia fursa zingine zitakazopatikana kwa malipo,"kilisema chanzo cha habari.

OKWI AFUNGIWA MECHI TATU, ATOZWA FAINI 500,000/-


KAMATI ya ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia mshambuliaji Emmanuel Okwi wa klabu ya Simba kucheza mechi tatu za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Mbali na kufungiwa, kamati hiyo imemtoza faini ya sh. 500,000 mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, maamuzi hayo yalifikiwa katika kikao cha kamati ya ligi kilichofanyika juzi chini ya mwenyekiti wake, Wallace Karia.
Wambura alisema Okwi amefungiwa kwa mujibu wa kanuni ya 25 (1) ya ligi kwa kosa la kumpiga kiwiko beki Kessy Mapande wa timu ya JKT Ruvu ya mkoa wa Pwani.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Okwi alitolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani. Simba iliibwaga JKT Ruvu kwa mabao 2-0.
Kufuatia kupewa adhabu hiyo, Okwi sasa atakosa mechi zingine mbili za ligi kuu dhidi ya Prisons na Yanga. Tayari mchezaji huyo ameshakosa mechi moja dhidi ya Ruvu Shooting.
Simba inatarajiwa kumenyana na Prisons keshokutwa katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kuvaana na watani wao Yanga kwenye uwanja huo Oktoba 3 mwaka huu.
Wakati huo huo, kamati ya ligi imemwondoa George Komba kwenye orodha ya makamishna wanaosimamia mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara.
Wambura alisema jana kuwa, Komba ameondolewa kwenye orodha hiyo kutokana na upungufu uliojitokeza kwenye ripoti yake ya mechi kati ya Simba na JKT Ruvu.
Kwa mujibu wa Wambura, kamati hiyo pia imeziandikia barua za onyo klabu za Africal Lyon, Mtibwa Sugar, Simba na mwamuzi Ronald Swai kwa makosa mbali mbali.
African Lyon imepewa onyo kwa kwenda uwanjani na jezi tofauti na ilizozionyesha kwenye mkutano wa maandalizi katika mechi yake dhidi ya Simba, Mtibwa imeonywa kwa kuchelewa kuwasilisha leseni za wachezaji wake katika mechi kati yao na Ruvu Shooting wakati Simba imeonywa kwa kosa la mashabiki wake kushangilia kupita kiasi.
Swai ameonywa kutokana na upungufu aliouonyesha katika mechi kati ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Wambura, mchezaji Faustine Lukoo wa Polisi Morogoro na Katibu wa Oljoro JKT aliyemwagiwa maji na wachezaji wa Polisil, masuala yao ni ya kinidhamu hivyo yamepelekwa mbele ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi kwa ajili ya hatua zaidi.
Wakati huo huo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga leo anatarajiwa kukutana na waandishi wa habari katika kikao kitakachofanyika saa sita mchana katika makao makuu ya shirikisho hilo yaliyopo Ilala, Dar es Salaam.

SAINTFIET-ALIAJIRIWA KWA BASHASHA KAONDOKA KICHWA CHINI


JAPOKUWA huenda usiku wa Ijumaa iliyopita haukuwa mzuri kwa watu wengi, lakini kocha Tom Saintfiet kwake ulikuwa mbaya zaidi.
Kocha huyo hakutegemea kama mazungumzo yaliyochanganyika na malumbano kati yake na viongozi wa Yanga mbele ya wachezaji wakati alipofuatwa kwenye hoteli ya Protea Masaki, Dar es Salaam ili aeleze sababu za timu kuvurunda katika ligi kuu, kama yangefuta kibali chake cha kuishi Tanzania, nchi inayosifika kuwa kisiwa cha amani.
Hawezi kuendelea kuishi kwenye ardhi ya bongo kwa sababu hana kazi kwa sasa na yeye ni mgeni, hivyo akilipwa chake arudi Ubelgiji kuendelea na maisha ya Ulaya.
Kwake maisha ya Masaki ni 'bye bye' na aliyapa kisogo baada ya kumalizika kwa kikao cha kumjadili na kuambiwa kuwa kibarua chake kimeota nyasi kuanzia muda huo.
Saintfiet ni kati ya makocha walioweka rekodi ya kukaa kipindi kifupi katika klabu hiyo, baada ya kuondolewa kwenye kiti cha enzi akiwa amedumu siku zipatazo 80.
Kati ya siku hizo, tatu zilikuwa za kukamilisha mazungumzo ya kuinoa Yanga baada ya kuwasili nchini, ambapo alitia saini mkataba wa miaka miwili unaodaiwa ulikuwa na thamani ya sh milioni 600.
Lakini Saintfiet ameshindwa kufaidi mamilioni hayo baada ya kuanza kazi Julai 6, mwaka huu, na kufukuzwa Septemba 21! Hajadumu hata miezi mitatu, lakini ukweli ni kwamba huo ndio mwanzo na mwisho wake kupiga mzigo Yanga.
AMEKOSA NINI?
Kwa mujibu wa kocha huyo, ameshangazwa kuambiwa na kiongozi mmoja wa juu kuwa 'kazi basi', lakini dhahiri shairi amemwaga unga baada ya kushupalia sera zake na kukataa kupindishwa na kibosile huyo.
Inadaiwa Mtakatifu Tom hakuwa radhi kuwa kocha wa 'ndiyo mzee' na alijibu mapigo kila alipoona hajazungumzwa vizuri. Kumbe hakujua kama kauli zake zinamchefua mwajiri.
Kitendo bila ya kuchelewa, mwajiri alimwambia kuanzia Ijumaa usiku huo hana kazi na baada ya hapo kikao kikafungwa kwa kila mtu kupitia mlango wake kwenda kulala.
Mzizi wa kikao hicho ulitokana na matokeo mabaya kufuatia Yanga kulazimishwa suluhu na Tanzania Prisons ya Mbeya katika Uwanja wa Sokoine na mchezo uliofuata wiki iliyopita timu hiyo ilifungwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro.
Viongozi wa Yanga wanasema kosa la kocha huyo kuwaruhusu wachezaji kwenda kucheza muziki usiku mjini Mbeya baada ya kushindwa kuifunga Prisons, ambapo kitendo hicho wanasema sawa na utovu wa nidhamu.
Clement Sanga, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, anasema kuwa jambo la pili kocha huyo ni mkaidi na haambiliki, anataka anachosema kikubaliwe.
Kwa mfano, alikuwa hataki wachezaji wakae kambini, hasa baada ya kutoka Mbeya, ambapo aliamua timu irudi Dar es Salaam na kwenda Morogoro siku mbili baadaye wakati wangeweza kufika mji kasoro bahari na kubaki kambini kuwasubiri Mtibwa.
Ingawa hayo yanaochukuliwa kama makosa yaliyochangia kocha huyo kufukuzwa, ikiwemo kuzungumza 'kwa sana' na vyombo vya habari, kutoboa siri ya kudai mshahara, hana gari, nyumba ya kuishi na wachezaji kulazwa 'mzungu wa wanne', ukweli unabaki pale pale kuwa alitimuliwa kwa sababu ya kutoleana lugha kali na mwajiri wake.
"Tulikuwa tunajadiliana (na bodi ya klabu), waliniuliza maoni yangu kuhusu kinachoendelea, nilitoa mawazo yangu kwa uwazi kabisa, lakini watu wengine walikuwa na mawazo yao juu ya klabu inavyopaswa kuendeshwa, .... akasema kuanzia sasa huna kazi," alisema kocha huyo.
KUVUNJWA MKATABA/KIJEMBE
Hakuna anayejua vipengele vilivyomo katika mkataba wa miaka miwili aliosaini kocha huyo na Yanga, lakini hakuna njia ya kukwepa kumlipa fidia ya kiasi ambacho kitategemeana na vipengele vya mkataba vinasemaje.
Kisheria mlipa fidia ni Yanga kwani ndiye anayetambulika katika mikataba hata kama alishawishiwa na watu binafsi kuja kufanya kazi hiyo.
Kocha huyo juzi kupitia BBC alidai licha ya Yanga kumtupia virago, haijakabidhi barua ya kueleza uamuzi huo na kushangazwa kupoteza ulaji kutokana na mechi mbili.
"Baada ya mechi mbili huwezi kusema tumeanza vibaya, Mourinho (Jose) ana wachezaji bora Hispania, lakini hawezi kushinda kila mechi," anasema Saintfiet.
Amerusha kombora kuwa kufanya vibaya kwa Yanga kulichangiwa na kuongezwa wachezaji wapya ambao hakuwataka isipokuwa aliwatumia kutokana na maslahi ya watu binafsi ambao hakuwataja.
"Nilikuwa na orodha yangu, lakini wao walinunua wachezaji wasiohitajika."
Tangu alipofukuzwa Ijumaa iliyopita, anasema uongozi wa klabu hiyo haujawasiliana naye kujadiliana naye jinsi ya kumlipa fedha zake.
AMETOKA NIGERIA NA MKOSI
Nuksi kwa Saintfiet ilianza wakati alipokuwa Nigeria, ambako mkataba wake wa miaka minne wa Mkurugenzi wa Ufundi ulikatishwa na waziri wa michezo wa nchi hiyo.
Mkataba huo ulipigwa chini ndani ya miezi mitatu akiwa bado hajaanza kazi katika Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF).
Wiki kadhaa baada ya kuteuliwa, Mbelgiji huyo hakuripoti kazini kutokana na kuwepo mvutano juu ya uamuzi huo, ambao ulifutwa Agosti, mwaka huu, na waziri mpya wa michezo, Bolaji Abdullahi.
Uamuzi wa Abdullahi kumtimua kocha huyo ulipokewa kwa hisia tofauti na Wanaigeria kwa baadhi kushangazwa na wengine kumpongeza waziri huyo wa michezo.
Miongoni mwa waliomfagilia waziri huyo ni makocha wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, Adegboye Onigbinde na Joe Erico.
Walisema wazo la kuajiri bosi wa kigeni wa ufundi halikuwa sahihi kwa kutambua kuna makocha wengi Nigeria wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo.
“Waanzilishi wa wazo hili ni wabinafsi kwa sababu wanatambua makocha kadhaa wa Nigeria wanao uwezo wa kufanya kazi hiyo vizuri," anasema Onigbinde.
“Uzoefu gani ambao anao mkurugenzi wa kigeni, makocha wa Nigeria hawana?” alihoji.
“Ni usaliti mpaka wakati huu nchi yetu kuamini itaimarishwa na watu kutoka nje kuliko wazawa.
Erico alisema kama NFF inataka kuajiri mkurugenzi wa ufundi wa kigeni, haina budi kumwajiri mtu anayefahamu kwa kina mazingira ya soka na historia ya Nigeria.
Kocha wa zamani wa Super Eagles, Paul Hamilton, ametofautiana na Wanigeria hao juu ya kuamini kuna mzawa mwenye ubavu wa kuwa mkurugenzi wa ufundi.
'Filamu' ya Saintfiet iliishia hivyo Nigeria na hatimaye alikuja Yanga Julai mwaka huu kukamilisha mazungumzo ya ajira nyingine iliyovunjika ndani ya siku 77, wakati Nigeria kibarua chake kilidumu siku 90.
Kwaheri Mtakatifu Tom kwani ulipokewa na mashabiki 300 kwa ngoma na vifijo, lakini mnaondoka watatu; wewe, mchumba wako na dereva teksi kwenda uwanja wa ndege wa JNIA tayari kwa safari ya kurudi Ubelgiji.
Kama hana kosa, Yanga watamkumbuka na kama alikosea, hatakumbukwa na yeyote.
Kufukuzwa kocha huyo ni mwendelezo wa kimbunga kilichotua Yanga mapema Ijumaa mchana na kusambaratisha sekretarieti yote chini ya Katibu Mkuu, Mwesigwa Celestine, Masoud Saad-Mtawala, Luis Sendeu,Ofisa Habari na Hafidh Mohamed aliyechomolewa katika umeneja wa timu na kuhamishiwa katika mipango.
REKODI YA SAINTFIET YANGA
1. Yanga v JKT Ruvu (kirafiki) 2-0
2. Yanga v Atletico (Burundi, Kagame) 0-2
3. Yanga v Waw Salam (Sudan, Kagame) 7-1
4. Yanga v APR (Rwanda, Kagame) 2-0
5. Yanga v Mafunzo (Z’bar, Kagame) 1-1 (5-3 penati)
6. Yanga v APR (Rwanda, Kagame) 1-0
7. Yanga v Azam (Kagame) 2-0
8. Yanga v African Lyon (kirafiki) 4-0
9. Rayon v Yanga (kirafiki, Rwanda) 0-2
10. Polisi v Yanga (kirafiki, Rwanda) 1-2
11. Yanga v Coastal Union (kirafiki) 2-1
12. Yanga v Moro United (kirafiki) 4-0
13. Prisons v Yanga (Ligi Kuu) 0-0
14. Mtibwa v Yanga (Ligi Kuu) 0-3

VODACOM WAPASUA JIPU


KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imesema suala la kuwepo kwa kipengele cha upekee 'Exlusivity' katika mkataba wa udhamini wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara kati yake na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni la muhimu katika kuepuka migongano ya kimaslahi.
Mkuu wa Udhamini na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Vodacom inajali na kuthamini maendeleo ya klabu za soka nchini na kwamba itaendelea kufanya hivyo kwa kutoa fursa zaidi zinazolenga kukuza kiwango cha uwekezaji katika soka kwa masilahi ya klabu na taifa kwa jumla.
Twissa alisema katika kutambua umuhimu wa kupanua wigo wa uwekezazi katika ligi kuu ya Vodacom na maendeleo ya klabu, Vodacom Tanzania ilikubali kwa moyo mkunjufu kuruhusu klabu kutafuta wadhamini wengine, ambao siyo kampuni zinazofanya baishara sawa na Vodacom.
Ofisa huyo alisema hayo wakati wa kikao cha pamoja kilichowakutanisha viongozi wa TFF, kamati ya ligi kuu na Vodacom Tanzania kilichofanyika mjini Dar es Salaam jana.
“Tunatambua na kuheshimu utayari wa kampuni zingine, ambazo zipo tayari kushirikiana na sisi katika kudhamini ligi kuu ya Vodacom, nasi tupo tayari kushirikiana nao na hivyo kuleta maendeleo ya mpira wa miguu nchini,”alisema Twissa.
“Vodacom Tanzania inajivunia kuwa wadhamini wakuu wa ligi hii, tumeamua kuboresha udhamini wetu kwa sababu tunatambua umuhimu wa michezo kwa taifa letu, sasa michezo si kwa ajili ya burudani tu bali imekuwa chanzo cha ajira na kuboresha maisha ya wanaojihusisha nayo,” aliongeza.
“Tunaziomba klabu zinazoshiriki ligi kuu, vyombo vya habari na umma kwa ujumla kutambua kuwa azma ya Vodacom ni kuona mpira wa miguu unasonga mbele zaidi na ndio maana tumekuwa katika udhamni huu kwa zaidi ya miaka saba tukipitia vipindi tofauti, lakini hatukuwahi kukata tamaa. Hivyo si vyema wakati huu soka yetu inapokua, tukaruhusu hali inayoweza kusababisha changamoto katika uwekezaji wa soka,”alisema
Twisa.
Aliongeza kuwa, Vodacom itaendelea kushirikiana na TFF, kamati ya ligi na wadau wengine wote wa mpira wa miguu nchini katika kukuza uwekezaji kwa kuzisaidia klabu kupata wadhamini watakaosaidia maendeleo yao.

WAREMBO MISS TANZANIA KAMBINI OKT 2


WAREMBO 30 watakaoshiriki katika shindano la mwaka huu la kuwania taji la Miss Tanzania, wanatarajiwa kuingia kambini Oktoba 2 mwaka huu kwenye hoteli ya Giraffe mjini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga alisema jana kuwa, shindano la mwaka huu limepangwa kufanyika Novemba 3 mwaka huu kwenye hoteli ya Blue Pearl mjini Dar es Salaam.
Lundenga alisema washiriki wa shindano hilo wamepatikana baada ya kukamilika kwa mashindano ya awali ya ngazi ya mkoa na kanda.
Mwenyekiti huyo wa Miss Tanzania alisema mashindano ya mwaka huu yalikuwa na msisimko mkubwa kutokana na kuwashirikisha wasichama wengi wasomi wa elimu ya juu.
"Tunaamini mashindano ya mwaka huu ya Miss Tanzania yatakuwa na ushindani mkali kutokana na asilimia 90 ya washiriki kuwa wasomi wa vyuo vya elimu ya juu,"alisema.
Meneja wa kinywaji cha Redd's, ambao ni wadhamini wakuu wa shindano hilo, Victoria Kimaro alisema wamejipanga vyema kuhakikisha shindano la mwaka huu linakuwa na mvuto wa aina yake.
Alisema lengo la wadhamini ni kuona kuwa, mashabiki wa fani hiyo wanapata burudani ya aina yake na mshindi mwenye sifa na vigezo vya kuiwakilisha vyema Tanzania katika shindano la dunia.
Victoria alisema wakati watakapokuwa kambini, washiriki watajifunza mambo mbali mbali kwa kuzingatia mabadiliko ya kalenda ya mashindano ya urembo ya dunia.
Kutokana na mabadiliko hayo, alisema mrembo wa Tanzania atakuwa na muda mrefu wa maandalizi na atatakiwa kuripoti katika fainali za mashindano ya urembo ya dunia mwakani.

MGUNDA AWALIZA COASTAL UNION


UONGOZI wa klabu ya Coastal Union ya Tanga umeeleza kusikitishwa kwake na uamuzi wa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda na msaidizi wake, Habibu Kondo kutangaza kujiuzulu.
Akizungumza na Burudani kwa njia ya simu kutoka Tanga juzi, Mwenyekiti wa Coastal Union, Ahmed Aurola alisema wamezipokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa.
Aurola alisema kujiuzulu ghafla kwa makocha hao kumeuweka uongozi kwenye njia panda kwa vile bado timu hiyo inakabiliwa na mechi ngumu za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Alisema ameshangazwa na uamuzi huo wa Mgunda na mwenzake kwa vile hakukuwa na uhusiano wowote mbaya kati yao zaidi ya shinikizo kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo kutokana na Coastal Union kutofanya vizuri katika ligi hiyo.
Coastal Union ilianza ligi hiyo kwa kuichapa Mgambo JKT bao 1-0 mjini Tanga kabla ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Prisons mjini Mbeya na kutoka suluhu na Toto Africans mjini Tanga.
Matokeo hayo yaliifanya Coastal Union ishike nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi tano baada ya kucheza mechi tatu, sawa na Prisons na JKT Oljoro zinazoshika nafasi ya tatu na ya nne. Simba inaongoza kwa kuwa na pointi tisa ikifuatiwa na Azam yenye pointi saba.
"Siyo tu uongozi, ambao umeshtushwa na kusikitishwa na kuondoka ghafla kwa Mgunda, bali hata wachezaji nao wamepatwa na mshtuko mkubwa," alisema Aurola.
Kwa mujibu wa Aurola, tayari wameshaanza kufanya mazungumzo na kocha Hemed Morocco wa Mafunzo ya Zanzibar ili aweze kuchukua nafasi ya Mgunda.
Mbali na kufanya mazungumzo na Morocco, alisema uongozi umekutana na wachezaji na kuwataka wasahau yaliyopita, badala yake waweke mbele majukumu waliyonayo katika ligi.
"Uongozi unamshukuru Mgunda kwa mchango mkubwa alioutoa kwa Coastal Union, lakini kwa vile ameamua kujiweka pembeni, hatuna kinyongo naye, tunamtakia kila la kheri,"alisema.
Mwenyekiti huyo wa Coastal Union amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo na kuwataka wawe na subira kwa vile bado timu yao inao uwezo wa kufanya vizuri katika ligi hiyo.

KAMATI YA UCHAGUZI TFF YACHARUKA


KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imewaonya wagombea wa nafasi mbali mbali za uongozi katika vyama vya mikoa na vilivyo wanachama wa shirikisho hilo kuepuka kutoa lugha na matamshi yanayokiuka kanuni za uchaguzi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deogratias Lyatto alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, baadhi ya wagombea uongozi katika vyama hivyo wamekuwa wakikiuka kanuni za uchaguzi kwa kutoa matamshi mabaya dhidi ya wapinzani wao kupitia kwenye vyombo vya habari.
Lyatto alisema kufanya hivyo ni makosa kwa vile baadhi ya matamshi yanayotolewa na wagombea hao ama wapambe wao yanaingilia na kukiuka taratibu za uchaguzi.
"Kamati inawataka wagombea wote waheshimu na kuzingatia kikamilifu kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF, vinginevyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha wagombea wote wanapata fursa sawa,"alisema.
Lyatto alisema ni makosa kisheria kwa wagombea na wapambe wao kutoa matamshi yanayolenga kuzishawishi kamati za uchaguzi kutoa maamuzi yenye mwelekeo wa kuwanufaisha dhidi ya wapinzani wao.
Alisema kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, ibara ya 9, wagombea wa nafasi za uongozi katika vyama vya michezo vilivyo wanachama wa TFF wanapaswa kuzingatia misingi ya uadilifu wakati wote wa uchaguzi.
Tahadhari hiyo ya kamati ya uchaguzi ya TFF imekuja huku kukiwa na msuguano mkali kati ya wagombea waliokatwa kwenye uchaguzi wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kamati ya uchaguzi ya chama hicho.
Baadhi ya wagombea waliokatwa wameilalamikia kamati hiyo kwa kuwapitisha wagombea wasiokuwa na sifa na kuwaacha wale wanaoonekana kuwa tishio dhidi ya wagombea wanaobebwa.

YANGA ISIKURUPUKE KUAJIRI KOCHA MWINGINE WA KIGENI


KLABU ya Yanga wiki iliyopita ilitangaza kumtimua kocha mkuu wa timu hiyo, Tom Saintfiet kutoka Ubelgiji kwa madai ya tuhuma za utovu wa nidhamu uliokithiri.
Akitangaza uamuzi huo kwa waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alizitaja sababu za kutimuliwa kwa kocha huyo kuwa ni pamoja na kuwa mkaidi wa kutii maelekezo ya uongozi na kushindwa kuthibiti nidhamu kwa wachezaji.
Alizitaja sababu zingine kuwa ni kocha huyo, aliyekuwa na mkataba wa kuinoa Yanga kwa miaka miwili, kukataa kambi, kukiuka maadili, kujibizana na viongozi na kuzungumza hovyo na vyombo vya habari.
Licha ya kutolewa kwa sababu hizo, kuna habari kuwa, sababu kubwa iliyomfanya kocha huyo atimuliwe ni kitendo chake cha kumfokea kiongozi mmoja wa juu wa Yanga baada ya kocha huyo kumtukana mbele ya wachezaji.
Kufuatia kukatishwa kwa mkataba wa Saintfiet, uongozi wa Yanga umemteua msaidizi wake, Fred Felix Minziro kuwa kocha mkuu wa muda hadi atakapoajiriwa kocha mwingine mpya kutoka nje ya nchi.
Mbali na kukatisha mkataba wa Saintfiet, uongozi wa Yanga pia umewafungashia virago aliyekuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa, Ofisa Habari, Louis Sendeu pamoja na meneja wa timu, Hafidh Saleh.
Nafasi ya Mwesigwa imechukuliwa kwa muda na katibu mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako wakati nafasi ya meneja wa timu huenda ikachukuliwa na mchezaji wa timu hiyo, Sekilojo Chambua. Nafasi ya ofisa habari bado ipo wazi.
Kutimuliwa kwa Saintfiet kulipokelewa kwa mshtuko mkubwa na wadau wa michezo nchini, hasa ikizingatiwa kuwa, hana muda mrefu tangu alipoanza kuinoa timu hiyo, akirithi mikoba ya kocha wa zamani, Kostadin Papic.
Mbali na kutokuwa na muda mrefu Yanga, kocha huyo pia alishajiwekea rekodi nzuri, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo. Pia aliweka rekodi ya kuiongoza Yanga kushinda mechi zaidi ya nane, kutoka sare mbili na kufungwa mbili.
Lengo la safu hii si kuunga mkono ama kuulalamikia uamuzi wa Yanga kumtimua kocha huyo. Lengo ni kujadili ni athari zipi, ambazo timu hiyo inaweza kuzipata kutokana na kumtimua kocha huyo wakati ambapo ndio kwanza ligi kuu ya Tanzania Bara imeanza.
Ikumbukwe kuwa, tangu Saintfiet alipoanza kuinoa Yanga, amekuja na mfumo mpya na ambao tayari wachezaji wameshaanza kuuzoea na kuutumia katika mechi kadhaa walizocheza. Sasa iwapo atakuja kocha mwingine mpya katika kipindi hiki, ni wazi kuwa atakuja na mfumo wake mpya na itachukua muda mrefu kwa wachezaji kuuzoea na kuanza kuutumia.
Kutokana na ukweli huu, ni vyema uongozi wa Yanga usitishe mpango wa kuajiri kocha mwingine kutoka nje kwa sasa, badala yake imwache Minziro aendelee kukaimu nafasi hiyo hadi baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu.
Hii ni kwa sababu Minziro ni kocha mzoefu na ameshawahi kufanyakazi chini ya makocha wengi wa kigeni, anaufahamu vyema mfumo uliokuwa ukifundishwa na Saintfiet na ana uwezo wa kuendelea nao hadi mzunguko wa kwanza utakapomalizika.
Kama uongozi wa Yanga unayo nia ya dhati ya kuajiri kocha mwingine wa kigeni, ni vyema ufanye hivyo baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, ili hata kama atakuja na mfumo mpya, aweze kuwa na muda wa kutosha wa kuufundisha kwa wachezaji na kuutumia katika mzunguko wa pili.
Uzoefu unaonyesha kuwa, Yanga imeshawahi kufanya mabadiliko ya makocha katikati ya ligi mara kadhaa na mara zote yamekuwa yakiwaathiri wachezaji kutokana na kufundishwa mifumo tofauti katika ligi ya msimu mmoja.
Mabadiliko pekee, ambayo hayakuiathiri timu ni pale alipotimuliwa Kondic na kulewa Sam Timbe kutoka Uganda na hii ni kwa sababu kikosi cha Yanga kilikuwa kinaundwa na wachezaji wengi wazuri ndio sababu kiliweza kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya bara na Kombe la Kagame.
Hivyo ni vyema viongozi wa Yanga wasifanye papara ya kuajiri kocha wa kigeni kwa sasa, badala yake wampe nafasi Minziro ya kuonyesha uwezo wake na pia yale aliyojifunza kutoka kwa makocha waliotangulia kama vile Papic, Dusan Kondic, Timbe na Saintfiet.

OMOTOLA: SIJAKUZA MAKALIO YANGU


LAGOS, Nigeria
MWANAMUZIKI na mcheza filamu mwenye mvuto nchini Nigeria, Omotola Jalade amekanusha madai kuwa, amefanyiwa operesheni maalumu kwa ajili ya kukuza makalio yake.
Omotola amekaririwa na mtandao mmoja wa Nigeria wiki hii akisema kuwa, taarifa hizo ni za uzushi na hazina ukweli wowote.
Baadhi ya mitandao ya Nigeria iliripoti hivi karibuni kuwa, Omotola amekuza makalio yake baada ya kuchapishwa kwa picha zake akiwa mjini Lagos hivi karibuni akionekana amejazia.
Mitandao hiyo ilidai kuwa, mwanamama huyo ameamua kufanya operesheni hiyo kwa lengo la kuongeza mvuto wa mwili wake.
Hata hivyo, Omotola ameziita taarifa hizo kuwa ni za uzushi kwa vile kuongezeka kwa makalio yake ni matokeo ya kunenepa kwa mwili wake.
"Kamwe siwezi kufanya kitu kama hicho. Hili ni umbile langu halisi. Ndivyo mwili wangu ulivyo. Ninaonekana tofauti kwa sababu nimeongezeka uzito,"alisema.
Amewataka mashabiki wake waache kuziamini taarifa hizo kwa sababu anafurahia uumbaji wa Mungu kwake na hawezi kufanya kitu kingine tofauti kwa lengo la kuongeza mvuto.

DESMOND ELLIOT AZUSHIWA KIFO



LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Desmond Elliot amejikuta akiwa kwenye wakati mgumu baada ya kuzushiwa mara kwa mara kwamba ameuawa.
Uvumi wa kifo cha Elliot umekuwa ukienezwa kupitia kwenye mitandao mbali mbali ya kijamii na baadhi ya mashabiki wameonekana kukerwa na uzushi huo.
Septemba 14 mwaka huu, mtu mmoja aliandika kupitia kwenye facebook kwamba Elliot ameuawa na kuweka picha inayofanana na ya Elliot.
Lakini mwisho wa maelezo hayo, mtu huyo aliandika: "Tafadhali msishtke kwa sababu picha hii ni sehemu ya filamu mpya (ya Elliot), ambayo bado haijatoka."
Elliot ameungana na watu wengine maarufu nchini Nigeria, Morgan Freeman na Bill Nye ambao mapema mwezi huu nao walizushiwa vifo, lakini ikaja kubainika baadaye kwamba taarifa hizo hazikuwa za kweli.
Mapema wiki hii, mtu mwingine aliweka kwenye mtandao wa facebook picha ya mtu akiwa amelala kwenye dimbwi la damu na kuandika: "Habari zilizotufikia hivi punde: Mwigizaji wa Nigeria,Desmond Elliot amekutwa akiwa hajiwezi kwenye dimbwi la damu kwenye hoteli moja mjini Lagos."
Taarifa hiyo feki iliendelea kudai kuwa, Elliot alikuwa ameuawa kwenye chumba cha hoteli hiyo na kwamba uchunguzi juu ya mtu aliyemuua ulikuwa ukiendelea kufanywa na polisi.
Mwisho wa taarifa hiyo, mtu huyo aliandika: "Tafadhali msishtuke kwa sababu hii ni sehemu ya filamu mpya, ambayo bado haijatoka."
Mitandao mingine iliendelea kusambaza taarifa hizo feki na kuwapa usumbufu mkubwa mashabiki wa filamu, wakiwa wameondoa maneno ya mwisho yanayosema: "Tafadhali msishtuke."

RITA: SINA MATATIZO NA INI EDO


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nollywood, Rita Dominic amesema hana matatizo na msanii mwenzake wa fani hiyo, Ini Edo.
Rita alisema wiki hii kupitia mtandao wa facebook kuwa, tuhuma zinazoenezwa kuwa haelewani na Ini Edo hazina ukweli wowote.
"Sina tatizo lolote na Ini Edo linalohitaji kupatanishwa. Msiamini kila mnachokisoma kwenye vyombo vya habari,"ameeleza Rita kupitia mtandao huo.
Rita ametoa ufafanuzi huo baada ya shabiki wake mmoja kumuuliza kupitia mtandao huo ni lini atamaliza tofauti kati yake na Ini.
Ini na Rita wamekuwa wakiripotiwa kuwa na tofauti tangu mwaka 2011, lakini mara zote wamekuwa wakikanusha madai hayo.
Tuhuma hizo ziliibuka kwa mara ya kwanza baada ya nyota hao wawili kuteuliwa kuwania tuzo za waigizaji bora wa AFRIFF za mwaka 2011.
Rita na Ini walikuwa wakiwania tuzo ya mwigizaji bora wa kike na mshindi alitakiwa kusafiri kwenda London mwaka unaofuata. Tuzo hizo zilidhaminiwa na Arik Airline.
Kabla ya kutolewa kwa tuzo hizo, Rita alilalamikia kitendo cha Ini kuingilia kati mchakato wa uteuzi wa washindi kwa kuandika kwenye mtandao wa twitter kwamba aliibuka mshindi kwa kupata kura 200.
Kuanzia wakati huo, wacheza filamu hao walikuwa wakitoa lugha za kukashifiana kupitia kwenye mitandao mbali mbali, hali iliyosababisha waonekane kuwa hawaelewani.
Baadhi ya wacheza filamu nyota wa Nollywood wamekuwa wakilalamikiwa kwa kukanusha taarifa zinazoripotiwa na vyombo vya habari juu yao, wakidai kuwa hazina ukweli, lakini baadaye hubainika kuwa ni za kweli.
Miezi kadhaa iliyopita, Ini aliripotiwa kuwa mja mzito, lakini alikanusha taarifa hizo kabla ya kukiri kwamba ni za kweli.
Mcheza filamu mwingine nyota, Uche Jombo naye aliripotiwa kufunga ndoa kwa siri Mei mwaka huu, lakini alikanusha taarifa hizo kabla ya kubainika baadaye kwamba zilikuwa za kweli.

HAFSA KAZINJA: TANZANIA HAINA MWANAMUZIKI WA KIMATAIFA


MWANAMUZIKI nyota wa miondoko ya zouk nchini, Hafsa Kazinja amesema licha ya kuwepo kwa wanamuziki wengi nyota na wenye vipaji, bado Tanzania haijaweza kutoa mwanamuziki mwenye hadhi ya kimataifa.
Hafsa alisema hayo wiki hii wakati akihojiwa na mtandao wa Vijimambo akiwa katika ziara yake ya maonyesho kadhaa ya muziki nchini Marekani.
Mwanadada huyo alisema ni vigumu kwa Tanzania kumpata mwanamuziki mwenye hadhi hiyo kutokana na matatizo yaliyopo kwenye vyombo vya habari nchini.
"Vyombo vyetu vya habari ni tofauti na vilivyopo Kenya na Uganda. Havitazami aina bora ya muziki na mwanamuziki,"alisema Hafsa, ambaye alianza kung'ara kimuziki baada ya kurekodi kibao chake cha Presha, alichomshirikisha Banana Zorro.
Kwa mujibu wa Hafsa, mwanamuziki anapokuwa hasikiki kwa muda mrefu, haina maana kwamba ameishiwa,lakini huo ndio mtazamo wa baadhi ya vyombo vya habari vya Tanzania.
"Mara nyingi wanamuziki wanaotamba, baada ya muda fulani huwa wanawekwa pembeni. Kuna niliowakuta kwenye gemu, wakapotea, waliwekwa pembeni, lakini bado wana wapenzi wao,"alisema.
Hafsa alisema ni vigumu kwa mwanamuziki kuishiwa kwa vile bado ana kipaji na hiyo ni kazi yake, hivyo anapaswa kuendelea kuungwa mkono badala ya vyombo vya habari kumwonyesha kwamba ameishiwa.
"Nasikia hasira sana kulizungumzia jambo hili. Kuna wakati Juma Nature alionekana ameishiwa na hana jipya, lakini siku alipopanda stejini kwenye tamasha la fiesta, mashabiki walilipuka mayowe ya kumshangilia, hii inamaanisha kwamba bado anakubalika,"alisema Hafsa,
"Wanaosababisha hali hii ni watu wa vyombo vya habari. Sipaswi kuvilalamikia sana kwa sababu mimi binafsi nimejulikana kwa sababu ya vyombo vya habari,"alisema.
Katika mazingira haya, Hafsa alisema itakuwa vigumu kwa Tanzania kuwa na mwanamuziki mwenye hadhi ya kimataifa iwapo vyombo vya habari nchini havitasimama kidete kuwatangaza badala ya kuwabomoa.
Hata hivyo, Hafsa alikiri kuwa, kuibuka na kuzama kwa wanamuziki huenda kunatokana na kujisahau kwao na kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu, hivyo wanapaswa kubadilika.
Mwanamama huyo aliipongeza serikali kwa kuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya wasanii nchini kwa kuanza kutoza kodi kazi zote za sanaa ili waweze kufaidi matunda ya jasho lao.
"Kusema ule ukweli, serikali inatupenda sana, kuna vitu ambavyo imeshaanza kuvifanya, tusubiri tuone,"alisema.
Hafsa alikuwa miongoni mwa wanamuziki waliopewa nafasi ya kutumbuiza wakati wa sherehe za siku ya Mtanzania zilizofanyika hivi karibuni kwenye ubalozi wa Tanzania nchini Marekani. Katika sherehe hizo, alipata nafasi ya kuimba baadhi ya nyimbo zake zinazotamba kama vile Presha na Mashallah.
Alisema alijisikia furaha kupata nafasi hiyo kwa vile ilikuwa heshima kubwa kwake kutumbuiza mbele ya mabalozi wa nchi mbali mbali na pia baada ya kubaini kuwa nyimbo zake zinajulikana na kupendwa hata na watu wa nje.
Licha ya wasanii wengi wa Tanzania kujulikana katika baadhi ya nchi za Ulaya, Hafsa alisema hadi sasa hakuna cha maana wanachokipata kutokana na kazi yao.
"Wasanii wa Tanzania bado tunakabiliwa na matatizo mengi. Tunafanyakazi nzuri na kubwa, lakini hakuna tunachokipata,"alisema.
Kwa mujibu wa Hafsa, soko la muziki wa Kitanzania kimataifa bado siyo zuri na kwamba kujulikana kwa baadhi ya wasanii katika nchi za Ulaya kumetokana na wizi wa kazi zao za sanaa na si kununuliwa kwa wingi na mashabiki.
"Siwezi kulizungumza hili kwa sababu lina vipengele vingi. Inawezekana mashabiki wanakujua, lakini kwa sababu ya kupeana CD zenye nyimbo zako, hawanunui,"alisema.
Hafsa ameufananisha wimbo wake wa Presha kuwa ni sawa na Georgina wa Safari Trippers ama Kitambaa Cheupe wa King Kikii kwa vile hauwezi kuchujuka haraka. Alisema wimbo huo utaendelea kutamba kwa karne kadhaa zinazokuja.
Mwanamama huyo anavutiwa sana na uimbaji wa wanamuziki wakongwe wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Mbilia Bel na Tshala Muana pamoja na mtanzania, Stara Thomas, ambao amewaelezea kuwa ndio waliochangia kumfanya ajitose kwenye fani hiyo.
Kipaji cha Hafsa kilivumbuliwa na mmiliki wa Nyumba ya Vipaji (THT), Ruge Mutahaba baada ya kuvutiwa na kibao chake cha Mashallah, ambacho ndicho kilichobeba jina la albamu yake ya kwanza. Hata hivyo, kibao kilichotamba kwenye albamu hiyo ni Presha.
"Ni kweli wimbo ulionipa sifa ni Presha, lakini kwangu wimbo wa Mashallah ndio kila kitu kwa sababu ndio ulionifungulia njia,"alisema.
Hafsa alisema moja ya sababu zilizoufanya wimbo wa Presha kupata umaarufu ni kukiimba kwa kumshirikisha Banana. Alisema umaarufu wa kibao hicho ulitokana na ukongwe wa Banana katika fani ya muziki.
"Wimbo wa Presha ulipata umaarufu kwa sababu ya Banana. Alianza muziki kabla yangu. Unapomshirikisha mwanamuziki maarufu, siku zote yeye ndiye anayepata sifa. Lakini mwisho wa siku ikajulikana kwamba mimi ndiye niliyemshirikisha,"alisema.
"Kwa sasa nikishirikishwa na msanii ambaye si maarufu, watu wanaweza kudhani wimbo ni wa kwangu. Ndivyo muziki ulivyo,"aliongeza.
Hafsa alisema anapendelea sana kupiga muziki wa zouk kutokana na umri wake na pia kwa sababu ya kuvutiwa zaidi na Mbilia Bel na Tshala Muana.
"Kwa umri wangu, zouk ndio aina ya muziki unaonifaa na kunipendeza,"alisema.

SIMBA WAENDA KAMBINI ZANZIBAR

Baadhi ya wachezaji wa klabu ya Simba wakiwa bandarini mjini Dar es Salaam juzi kabla ya kupanda boti kwenda Zanzibar kwa ajili ya kujiaandaa kwa mechi yao ya ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Yanga.

Baadhi ya wachezaji wa Simba wakielekea kupanda boti kwa ajili ya safari yao ya kwenda Zanzibar juzi.

MANJI ATETA NA WAZEE NA VIJANA WA YANGA

Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji akisalimiana na wazee wa klabu ya Yanga kabla ya kuzungumza nao juzi makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji akiteta na wazee wa klabu hiyo juzi. (Picha zote na Emmanuel Ndege).
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji akinong'onezana jambo na mmoja wa vijana wa klabu hiyo baada ya kukutana na kuzungumza nao.

Monday, September 24, 2012

YANGA YAIPIKU SIMBA KWA MAPATO




Mechi za Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara za Simba na Yanga zilizochezwa wikiendi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zimeshuhudiwa na washabiki 65,458.
Yanga ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya JKT Ruvu, Jumamosi (Septemba 22 mwaka huu) mechi yao ilishuhudiwa na washabiki 15,770 wakati ile ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa jana (Septemba 23 mwaka huu) ilikuwa na washabiki 9,688. Simba ilishinda mabao 2-1.
Wakati mechi ya Yanga iliingiza sh. 88,251,000 ile ya Simba dhidi ya Ruvu Shooting Stars mapato yalikuwa sh. 55,454,000. Mechi ya Yanga kila timu ilipata sh. 19,846,194.92 huku ile ya Simba kila timu ilipata sh.11,350,774.58.
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Azam na Mtibwa Sugar iliyochezwa juzi (Septemba 22 mwaka huu) Uwanja wa Chamazi imeingiza sh. 2,509,000 ambapo kila timu imepata mgawo wa sh. 301,661.
Washabiki 827 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyomalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Nayo mechi ya ligi hiyo kati ya African Lyon na Tanzania Prisons iliyochezwa jana (Septemba 23 mwaka huu) kwenye uwanja huo imeingiza sh. 245,000 huku kila timu ikipata sh. 32,286. Prisons ilishinda mechi hiyo kwa mabao 2-1.

TFF YAZIPONGEZA KRFA NA MARFA




Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa vyama vya mpira wa miguu mikoa ya Kilimanjaro (KRFA) na Manyara (MARFA) katika uchaguzi uliofanyika juzi (Septemba 22 mwaka huu).
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza vyama hivyo unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KRFA na ule wa MARFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo katika mikoa hiyo.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa kamati za utendaji za MARFA na KRFA zinazoongozwa na Elley Mbise na Goodluck Moshi, kwani viongozi hao wapya wana changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha wanaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba zao na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.
Pia tunatoa pongezi kwa kamati za uchaguzi za IRFA na MARFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa kuongoza MARFA ni Elley Mbise (Mwenyekiti), Wilson Ihucha (Makamu Mwenyekiti), Apollinary Kayungi (Katibu), Peter Abong’o (Mhazini), Khalid Mwinyi (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Phortinatus Kalewa (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Peter Yaghambe (Mjumbe).
Kwa upande wa KRFA waliochanguliwa ni Goodluck Moshi (Mwenyekiti), Mohamed Musa (Katibu), Kenneth Mwenda (Mwakilishi wa Klabu TFF), Kusiaga Kiyata (Mhazini) na Denis Msemo (Mjumbe). Nafasi zilizowazi baada ya kukosa wagombea wenye sifa kwenye vyama hivyo zitajazwa baadaye.

Sunday, September 23, 2012

SIMBA YAZIDI KUCHANUA, YAICHAPA RUVU SHOOTING 2-1


BAO lililofungwa na mshambuliaji chipukizi, Christopher Edward leo limeiwezesha Simba kuichapa Ruvu Shooting mabao 2-1 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Edward aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ramadhani Chombo, alifunga bao hilo dakika 10 kabla ya mchezo kumalizika, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Mrisho Ngasa.
Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Felix Sunzi, aliyeunganisha wavuni kwa kichwa krosi maridhawa iliyochongwa na Nassoro Masoud Chollo aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi.
Ruvu Shooting ilisawazisha bao hilo dakika ya 78 kwa bao lililofungwa na Seif Rashid baada ya kumpokonya mpira beki Juma Nyoso ndani ya eneo la hatari na kuukwamisha mpira wavuni.
Simba ilifanikiwa kupata penalti kipindi cha kwanza baada ya beki mmoja wa Ruvu Shooting kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari, lakini shuti la Daniel Akuffour lilipanguliwa na kipa Benjamin Haule na kuwa kona, ambayo haikuzaa matunda.

EDDA ATWAA TAJI LA MISS TEMEKE 2012

Malkia wa Redd's Miss Tameke 2012, Edda Sylvester (katikati), akiwa na mshindi wa pili Flavian Maeda (kushoto) na Catherine Masumbigana aliyeshika nafasi ya tatu katika kilele cha mashindano hayo, Ukumbi wa PTA Sabasaba, Dar es Salaam jana usiku.

MINZIRO AMFUNIKA SAINTFIET


Hamisi Kiiza (kushoto) wa Yanga akigombea mpira na beki Ally Khan wa JKT Ruvu timu hizo zilipomenyana jana katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga ilishinda 4-1. (Picha kwa hisani ya blogu ya kamanda wa matukio)

KAIMU kocha mkuu wa Yanga, Fred Felix Minziro jana alikianza vyema kibarua chake baada ya kuiongoza timu hiyo kuichapa JKT Ruvu mabao 4-1 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Yanga tangu ligi hiyo ilipoanza wiki mbili zilizopita. Katika mechi ya ufunguzi, Yanga ililazimishwa kutoka suluhu na Prisons mjini Mbeya kabla ya kupigwa mweleka wa mabao 3-0 na Mtibwa mjini Morogoro.
Yanga ililazimika kucheza mechi ya jana ikiwa chini ya Minziro baada ya uongozi kuamua kusitisha mkataba wa kocha Tom Saintfiet kutoka Ubelgiji kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Didier Kavumbagu, aliyefunga mawili, Nadir Haroub 'Cannavaro' na Simon Msuva. JKT ilipata bao lake la kufutia machozi kupitia kwa mkongwe Credo Mwaipopo.
Katika mechi zingine zilizochezwa jana, Azam iliichapa Mtibwa bao 1-0, Oljoro JKT iliichapa Polisi Morogoro bao 1-0 wakati Coastal Union ilitoka suluhu na Toto Africans.

Saturday, September 22, 2012

YANGA YATANGAZA RASMI KUMTIMUA SAINTFIET


HATIMAYE klabu ya Yanga imetangaza rasmi kumtimua kocha mkuu wa timu hiyo, Tom Saintfiet kutoka Ubelgiji.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clament Sanga ametangaza maamuzi hayo leo asubuhi alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Sanga alisema nafasi ya Saintfiet itashikiliwa kwa muda na kocha msaidizi, Fred Felix Minziro hadi atakapotafutwa kocha mwingine.
Kwa mujibu wa Sanga, kocha huyo ametimuliwa kutokana na matokeo mabaya ya Yanga katika mechi za ligi kuu ilizocheza hivi karibuni, ambapo ililazimishwa kutoka suluhu na Prisons kabla ya kunyukwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar.

Sanga alisema si kweli kwamba wamemtimua Saintfiet kutokana na kutokuelewana na mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji.
Makamu mwenyekiti huyo wa Yanga alizitaja sababu zingine zilizochangia kutimuliwa kwa kocha huyo kuwa ni pamoja na kujihusisha na vitendo vya ulevi akiwa na wachezaji wa timu hiyo.
"Yapo mapungufu mengine mengi, lakini hatuwezi kuyaweka hadharani,"alisema.
Sanga alisema pia kuwa, nafasi ya katibu mkuu wa klabu hiyo kwa sasa itashikwa kwa muda na Lawrence Mwalusako wakati Dennis Oundo ameteulia kuwa mkurugenzi wa fedha na utawala.
Mwalusako amechukua nafasi ya Celestine Mwesigwa, ambaye mkataba wake umesitishwa sambamba na aliyekuwa ofisa habari, Louis Sendeu.
Yanga pia imeteua Sekilojo Chambua kuwa meneja mpya wa timu hiyo, kuchukua nafasi ya Hafidh Saleh, ambaye  atapangiwa majukumu mengine.

SIMBA, YANGA ZAKABIDHIWA MABASI MAPYA


Mkurugenzi Mkuu wa TBL, Robin Goetzsche kulia akimkabidhi mfano wa ufunguo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga wakati wa hafla ya kukabidhi basi jipya kwa klabu hiyo. TBL ndio mdhamini Mkuu wa klabu za Simba na Yanga.


Basi jipya la klabu ya Simba
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage akipokea mfano wa ufunguo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TBL, Robin Goetzsche kama ishara ya makabidhiano ya basi jipya lililotolewa na kampuni ya Bia Tanzania (TBL) katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Basi jipya la klabu ya Yanga

Friday, September 21, 2012

SILAHA ZA YANGA KWA JKT RUVU, JE MINZIRO ATABADILI KIKOSI BAADA YA TOM KUTIMULIWA?


KOCHA Mkuu wa Yanga. Tom Saintefiet ametangaza kikosi cha wachezaji 18 watakaocheza mechi ya ligi kuu ya Tanzania bara kesho dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika kikosi hicho, Tom ameamua kumtema mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Saidi Bahanunzi na kumpa nafasi hiyo, Jerry Tegete.
Tom aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, amekuwa akikatishwa tamaa na tamaa na baadhi ya wachezaji wake kutokana na viwango vyao kushuka.
Kocha huyo kutoka Ubelgiji alisema katika mazoezi waliyofanya leo asubuhi ya upigaji wa penalti, kati ya wachezaji sita waliopiga adhabu hiyo, waliofunga ni wawili tu.
Aliwataja wachezaji aliowateua kwa ajili ya mechi ya kesho, ambayo itakuwa ya tatu tangu kuanza kwa
ligi kuu kuwa ni makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, Godfrey Taita, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasika.
Viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Rashid Gumbo, Shamte
Ally na Simon Msuva wakati washambuliaji ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza.
Wachezaji walioachwa kwenye kikosi hicho ni kipa Said Mohamed, mabeki Nsajigwa Shadrack, Job
Ibrahim, viungo Frank Domayo, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Omega Seme, Nurdin Bakari, Idrisa
Assega na Issa Ngao.

SANGA AKIRI KUTIMULIWA KWA MAOFISA YANGA


UONGOZI wa klabu ya Yanga umeisimamisha kazi sekretarieti nzima ya klabu hiyo,

akiwemo Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa na Ofisa Habari, Louis Sendeu kutokana na kilichodaiwa kuwa ni utendaji mbovu wa kazi.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam leo kuwa, uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo kilichofanyika kuanzia asubuhi hadi jioni.
Watendaji wengine wa Yanga waliokutwa na pangua pangua hiyo ni aliyekuwa ofisa wa utawala, 
Masoud Saad, aliyekuwa mhasibu, Philip Chifuka na aliyekuwa meneja wa muda wa timu, Hafidh Saleh.
“Ni kweli tumeamua kusitisha mikataba ya sekretarieti nzima, pia tumefanya marekebisho, tumewatoa baadhi ya watendaji na kuteua watendaji wapya,”alisema Sanga.

BREAKING NEWSSSSS! KOCHA MKUU YANGA, KATIBU MKUU WATIMULIWA


UONGOZI wa klabu ya Yanga umetangaza kuwatimua Kocha Mkuu wa timu hiyo, Tom Saintfiet, Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa na Ofisa Habari, Louis Sendeu.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo kilichofanyika mjini Dar es Salaam leo.
Kikao hicho kiliitishwa siku moja baada ya Yanga kuchapwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Kipigo hicho kilikuwa mwendelezo mbaya kwa Yanga katika ligi hiyo iliyoanza wiki mbili zilizopita. Katika mechi ya ufunguzi, Yanga ililazimishwa kutoka suluhu na Prisons kwenye uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Thursday, September 20, 2012

YANGA KILIO MORO


Na Abdallah Mweri, Morogoro

TIMU ya Yanga imeendelea kushindwa kuonyesha cheche zake katika ligi kuu ya Tanzania Bara, baada ya kulambishwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Mtibwa Sugar ilistahili kutoka kifua mbele kutokana na kuidhibiti Yanga katika sehemu ya kiungo na kuwatumia vizuri winga Vicent Barnabas na mshambuliaji Hussen Javu walioipeleka puta ngome ya mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati 2012.
Viungo Shaban Nditi na Shaban Kisiga 'Malone' walitawala katika dimba la kati na kuisambaratisha Yanga ambayo imefanya usajili wa 'kufa mtu' kwa lengo la kufanya vizuri msimu huu.
Wachezaji mahiri waliosajiliwa na timu ya Yanga, Said Bahanuzi, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite na Didier Kavumbagu, jana hawakufua dafu kwa Mtibwa waliocheza kwa jihadi katika dakika zote 90 za mechi hiyo.
Dalili za Mtibwa Sugar kutoka uwanjani na ushindi zilianza kuonekana mapema baada ya Barnabas na Javu kufumua mashuti ambayo yaliokolewa na kipa Ally Mustapha 'Barthez' ndani ya dakika 11 na kabla ya Dickson Mbeikya kufunga bao la kwanza kwa kichwa baada ya kujitwisha kona iliyochongwa na Malika Ndeule dakika ya 12.
Baada ya bao hilo Mtibwa walicharuka na kuwaweka roho juu mashabiki wa Yanga waliofurika Morogoro kutazama mechi hiyo ya pili kwa timu yao iliyoanza msimu kwa kupepesuka. Mechi ya kwanza ya ufunguzi wa ligi Yanga ilitoka suluhu na Prisons ya Mbeya katika Uwanja wa Sokoine.
Katika mechi ya jana ilifungwa bao la pili na Javu aliyetumia uzembe wa mabeki kujichanganya katika dakika ya 43, ambapo aliachia shuti la nguvu nje ya mita 18 kwa mguu wa kushoto na mpira kujaa wavuni ukimpita Barthez aliyeruka bila mafanikio.
Ngwe ya kwanza Yanga walionyesha uhai pekee katika dakika ya 19, 22 na 25 baada ya Hamis Kiiza, Bahanuzi na Frank Domayo kupiga mashuti ambayo yalipanguliwa na Shaban Kado, kipa ambaye Yanga imemrudisha Mtibwa Sugar kucheza kwa mkopo kutokana na kukosa namba.
Bao hilo la Mtibwa lilipatikana ikiwa dakika moja baada ya beki wake Ndeule kuondoa kwenye 'chaki' mpira wa kichwa kilichokandamizwa na Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Kipindi cha pili licha Yanga kuongeza nguvu mpya kwa kuwaingiza Didier Kavumbagu, Stephano Mwasika na Simon Msuva na kufanya mashambulizi butu kuanzia dakika ya 71, haikuweza kudhibiti kasi ya Mtibwa iliyokuwa mwiba kutokana na kuonana kwa pasi na kufika kwenye eneo la wapinzani wao kadiri walivyotaka.
Javu alihakikishia Mtibwa Sugar bao la tatu katika dakika ya 76 baada ya kufunga kwa kunyanyua mpira wa mbali wakati alipobaki ana kwa ana na Barthez.
Yanga ilicheza chini ya kiwango ikiwemo Kiiza kupaisha penalti iliyotolewa katika dakika ya 87 na mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza kutokana na beki Ndeule kuunawa mpira ndani ya kiboksi cha hatari.
MTIBWA: Shaban Kado, Malika Ndeule, Issa Issa, Dickson Mbeikya, Salvatory Ntebe, Shaban Nditi, Jamali Mnyate, Awadhi Juma, Hussein Javu, Shaban Kisiga na Vicent Barnabas/Ally Mohamed.
YANGA: Ally Mustapha 'Barthez', Juma Abdul, David Luhende/Stephano Mwasika, Kelvini Yondani, Nadir Haroub 'Cannavaro', Mbuyu Twite/Didier Kavumbagu, Athuman Idd 'Chuji', Frank Domayo/ Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi na Hamis Kiiza.

SIMBA RAHA TUPU


LICHA ya kucheza ikiwa na wachezaji pungufu, Simba jana iliendelea kuunguruma katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuitungua JKT Ruvu mabao 2-0.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, imba ilijipatia mabao yake hayo mawili kupitia kwa kiungo Amri Kiemba na mshambuliaji Haruna Moshi 'Boban'.
Kiemba alifunga bao la kwanza dakika ya 47 kufuatia mpira wa kona uliopigwa na Amir Maftah, ambao uligonga nguzo ya pembeni ya goli na kumkuta mfungaji aliyeukwamisha wavuni.
Boban aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 72 baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Ramadhani Chombo, aliyeingia badala ya Daniel Akuffour, ambaye aliwatoka mabeki wawili wa JKT Ruvu na kutoa pasi kwa mfungaji aliyeukwamisha wavuni.
Matokeo hayo yameiwezesha Simba kuendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili, ikifuatiwa na Azam yenye idadi hiyo ya pointi, lakini zikiwa zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Simba ililazimika kucheza muda mwingi wa pambano hilo ikiwa na wachezaji 10 baada ya mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani kwa kosa la kumpiga kiwiko beki Kessy Mapande wa JKT Ruvu.\
Simba ilikuwa ya kwanza kubisha hodi kwenye lango la JKT Ruvu wakati Emmanuel Okwi alipochomoka na mpira na kupiga krosi iliyomita kipa Shabani Dihile, lakini mpira ulitoka nje.
Dakika tano baadaye, Mrisho Ngasa aligongeana vizuri na Mwinyi Kazimoto, aliyekuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga, lakini shuti lake lilipaa juu.
JKT Ruvu ilijibu mapigo dakika ya 22 wakati Omary Chang'a alipopewa pasi na Hussein Bunu na kuingia na mpira ndani ya 18, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Juma Kaseja.
Mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani alilazimika kumwonyesha kadi ya njani Kazimoto wa Simba kwa kosa la kucheza rafu na kisha kutoa lugha chafu kwa mwamuzi.
Beki Amir Maftah nusura aifungie bao Simba dakika ya 30 baada ya kupewa pasi murua na Daniel Akuffour, lakini shuti lake lilimbabatiza beki Damas Makwaya na mpira kutoka nje.
Kipa Dihile wa JKT Ruvu alilazimika kufanyakazi ya ziada dakika ya 34 kuokoa shuti kali la Mrisho Ngasa, aliyekuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga bao kabla ya kuokoa shuti lingine la Nassoro Cholo dakika ya 36 baada ya kutema shuti la kwanza.
Pamoja na kucheza ikiwa pungufu, Simba ilifanya mashambulizi makali kwenye lango la JKT Ruvu dakika ya 39 na 44 wakati Haruna Moshi alipopewa pasi akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake la kwanza liligonga mwamba wa goli na la pili liliokolewa na mabeki. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Daniel Akuffour nusura aiongezee Simba bao la pili dakika ya 49 baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa krosi kutoka kwa Kiemba, lakini kipa Dihile aliuwahi na kuokoa.
JKT Ruvu ilipata nafasi mbili nzuri za kufunga mabao dakika ya 51 na 56 wakati Mapande na Jimmy Shoji walipoingia na mpira ndani ya 18, lakini shuti la kwanza liliokolewa na kipa Kaseja wakati shuti la pili liligonga mwamba na mpira kutoka nje.
Simba: Juma Kaseja, Nassoro Cholo, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Juma Nyoso, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi, Daniel Akuffour/ Ramadhani Chombo, Mrisho Ngasa, Emmanuel Okwi.
JKT Ruvu: Shabani Dihile, Kessy Mapande, Stanley Nkomola, Damas Makwaya, George Minja, Ally Khan, Saidi Otega/Amos Kagisa, Jimmy Shoji, Omar Chang'a, Hussein Bunu na Credo Mwaipopo.
Solomon Mwansele ameripoti kutoka Mbeya kuwa, wenyeji Prisons na Coastal Union zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Coastal Union ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 30 kupitia kwa Jerry Santo kabla ya Prisons kusawazisha dakika ya 52 kwa bao lililofungwa na Freddy Chudu baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Coastal Union.

WAMENIDHALILISHA, LAKINI HAWANIWEZI-TID




BAADA ya kuwa kimya kwa muda kuhusu tuhuma za kutaka kumuua msanii mwenzake Ali Kiba, msanii machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Khaleed Mohamed 'TID' amesema tuhuma hizo hazikuwa na ukweli wowote.
TID amesema anashindwa kuelewa kwa nini alizushiwa tuhuma hizo kwa vile hana matatizo yoyote na Kiba, hajawahi kugombana naye na ni mtu wake wa karibu.
Kiongozi huyo wa Top Band aliwahi kushikiliwa na kuhojiwa na polisi kwa siku kadhaa kutokana na kuwepo kwa tuhuma hizo kabla ya kuachiwa huru.
"Hii kesi nashindwa kuielewa. Mimi ni mtu mzima sana, halafu ukiniambia nina matatizo na Ali Kiba wakati hata sijagombana naye, sielewi,"alisema TID wiki hii alipokuwa akihojiwa na kituo cha redio cha Clouds FM.
"Hivi mtu unakwenda kwa mganga, unataka kujibasti, halafu mganga anakwambia TID katoa ngoma kali, anataka kukuua, wewe unachukulia siriasi, hivi vitu ni vya kijinga sana, unatakiwa kufikiria kwa makini,"aliongeza msanii huyo, aliyewahi kutesa kwa kibao cha Zeze.
Kwa mujibu wa TID, baada ya kukamatwa na kuhojiwa, polisi walichukua namba yake ya simu kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kimawasiliano kuhusu tuhuma hizo, lakini hawakuweza kupata lolote la maana.
Alisema uchunguzi huo wa polisi ulibaini kwamba, hakuwahi kuzungumza lolote na Kiba ama mtu mwingine yoyote aliyetaka kumuua msanii huyo, hali iliyothibitisha kwamba tuhuma hizo zilikuwa za uongo.
TID alisema kwa fikra zake, anahisi mganga aliyemweleza Kiba maneno hayo, alifanya makosa makubwa kwa sababu katika maisha yake, hajawahi kuwaza kutenda dhambi kama hiyo kwa vile anajiamini kutokana na kipaji chake.
“Yeye kama anataka kuwa mkali kunizidi mimi, ajifue, atoe ngoma kali, lakini hakuna mtu anayemchukia, mimi nampenda sana na kama yeye anakataa mimi simpendi, kwa nini ameingia kwenye remix yangu na nimemuweka pale?" Alihoji TID.
Msanii huyo mwenye makeke alisema anahisi kuna baadhi ya watu wanaomchukia katika gemu, lakini alisisitiza kuwa hawamuwezi.
“Wanataka kuniweka ndani, wanataka kunifunga jela, lakini hawaniwezi," alisisitiza msanii huyo.
Akizungumzia kesi aliyofungiwa, TID alisema ni lazima ifike kwa mwanasheria mkuu ili aweze kuangalia iwapo ni halali au ya kubambikiwa.
"Nimepata taarifa kwamba imerudishwa baada ya kubainika kwamba haiwezi kuwa kesi kwa vile haina ushahidi wowote. Imeonekana kuwa ni vitu vya kufikirika, ambavyo mtu alipanga vifanyike. Kwa sababu wao walitaka iwe kesi, na mimi nitawafungulia kesi kwa kunidhalilisha,"alisema.