KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 27, 2012

Wadau walalamikia uzungu kwenye filamu za kiswahili

WADAU wa sanaa nchini wamehoji uhalali wa wasanii wa filamu kutumia lugha ya kiingereza kwenye majina ya filamu zao na pia kazi hizo kubeba maudhui ya kizungu zaidi.
Wakizungumza mwanzoni mwa wiki hii kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa, wadau hao walisema hawaelewi ni kwa nini filamu nyingi zinazoandaliwa nchini zinapewa majina ya kizungu wakati zipo filamu nyingi kutoka nje zinazotumia lugha za kihindi, kichina, kifaransa na zinafanya vizuri.
“Hoja kwamba, wanatumia majina ya kiingereza ili kuteka soko la kimataifa ni ya kitoto. Mbona hapa kwetu kuna filamu nyingi za kihindi na kichina zinanunuliwa kwa wingi? Hapa kuna udhaifu katika kutengeneza filamu zenye ubora, tujikite huko,” msanii Nkwama Bhallanga.
Kwa mujibu wa wadau hao, filamu ni taaluma inayozungumza kwa kutumia picha na vitendo zaidi hivyo haihitaji mtazamaji kufahamu lugha iliyotumiwa ili afahamu maudhui na ujumbe unaowasilishwa na kazi husika ya filamu.
“Maneno kwenye filamu si muhimu sana, kinachozungumza ni matendo na picha zaidi, ndiyo maana kuna watu wanaangalia picha za kikorea na wanaburudika na kuelewa kinachoendelea,” alisema Godfrey Lebejo, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Aliongeza kuwa, kinachoitesa tasnia ya filamu kwa sasa ni kukosekana kwa weledi na uhalisia wa tamaduni za Kitanzania kunakosababishwa na wimbi kubwa la watu kujiingiza kwenye filamu ili kufanikisha mambo yao yaliyo nje ya maadili na utamaduni huo.
“Inawezekana vipi utengeneze filamu ambayo baba, mama na watoto hawawezi kukaa pamoja kuitazama? Tufike mahali tuseme mambo haya ya kipuuzi basi kwenye filamu zetu,” alionya Lebejo.
Awali, akiwasilisha mada kuhusu filamu, wasanii na haja ya kujiendeleza kielimu, msanii wa filamu, Emmanuel Myamba, maarufu kam Pastor Myamba, alisema tasnia ya filamu inakosa weledi hivyo kuhitaji mabadiliko.
“Ni wazi ukiangalia filamu zetu zinakosa weledi katika uandishi wa miswada, uongozaji, uhariri na hata uumbaji wa wahusika. Lazima tukubali udhaifu huu ili tuurekebishe,” alisema Myamba, ambaye kwa sasa amefungua kituo cha mafunzo ya filamu kiitwacho Tanzania Film Training Centre (TFTC) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment