KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 14, 2012

Omotola ampiku Ini Edo kwa utajiri Nollywood

LAGOS, Nigeria
MIAKA michache iliyopita, thamani ya mwigizaji nyota wa Nigeria, Omotola Jalade-Ekeinde kwa malipo ya ndani ilikuwa ikikadiriwa kufika Naira milioni 1.7.
Kiwango hicho kilizua maswali mengi miongoni mwa mashabiki wa fani hiyo, ambao wengi walianza kuamini kuwa, kumbe fani ya uigizaji wa filamu inalipa.
Sasa ni miaka kadhaa imepita. Thamani ya Omotola siyo hiyo tena. Mwanadada huyo kwa sasa analipwa Naira milioni tano kwa kucheza filamu moja. Ni kiwango kikubwa.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka kwa watu wa karibu na mwanadada huyo, Omotola amekuwa akikataa ofa kadhaa za kucheza filamu kwa malipo ya Naira milioni tatu.
Na hivi karibuni alikataa kucheza filamu kwa malipo ya Naira milioni 2.5 na nafasi yake ilichukuliwa na mwigizaji Ireti Doyle.
”Omotola alitaka alipwe Naira milioni tano kwa kucheza filamu ya Amina, iliyoandaliwa na Tarila Thompson, lakini baada ya majadiliano, alikubali kulipwa Naira milioni 4.5,” kimesema chanzo cha habari. Kwa maana hiyo, iwapo Omotola atacheza filamu nne katika kipindi cha miezi miwili, atalipwa Naira milioni 20. Shabash! Ana kila sababu ya kustahili kuwa mwigizaji tajiri wa kike kwa sasa nchini Nigeria.
Kabla ya Omotola kupanda chati, Ini Edo ndiye aliyekuwa akishika namba moja kwa utajiri miongoni mwa waigizaji wa kike nchini Nigeria.
Katika hatua nyingine, Omotola amedhihirisha kuwa bado ni mwigizaji mwenye sura na umbo lenye mvuto nchini Nigeria kutokana na mwonekano wake kuwavutia watu wengi.
Wiki iliyopita, Omotola aliwachengua mashabiki wa fani hiyo nchini Uingereza, ambako alikwenda kwa ajili ya hafla ya uzinduzi wa filamu yake mpya ya Last Flight To Abuja.
Akiwa amevalia suruali ya jeans na blauzi ya rangi ya hudhurungi, mwanadada huyo alionekana akiwa na umbo lenye mvuto na haikuwa rahisi kuamini kuwa ni mke wa mtu na mama mwenye watoto wanne.
Omotola, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Omo Sexy ni mcheshi na anaonekana kama vile umri wake ni miaka 18. Ni mwanamke anayetajwa kuwa na mvuto zaidi nchini Nigeria.
Mara baada ya kuwasili mjini London, Omotola alifanya mkutano na waandishi wa habari akiwa na mtayarishaji wa filamu yake, Obo Emelonye.

No comments:

Post a Comment