KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 27, 2012

Ommy Dimpoz aibuka na ngoma mpya

BAADA ya kutamba vilivyo kwa kibao chake cha Nai Nai kilichomwezesha kushinda tuzo mbili za muziki za Kilimanjaro, msanii Ommy Dimpoz ameibuka na kibao kingine kipya.
Msanii huyo wa zamani wa bendi ya Top, inayoongozwa na Khaleed Mohamed (TID) ameshusha wimbo mpya unaokwenda kwa jina la Baadaye.
Dimpoz, ambaye pia hupenda kujiita kwa jina la Super Handsome alisema wiki hii mjini Dar es Salaam kuwa, anaamini kibao hicho kitawashika vilivyo mashabiki wake.
Msanii huyo alisema lengo la kurekodi kibao hicho ni kuwadhihirishia mashabiki wake kwamba hakubahatisha aliporekodi wimbo wake wa Nai Nai, akiwa amemshirikisha Ali Kiba.
Wakati kibao chake hicho kikiwa kimeshaanza kupigwa kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini, Dimpoz pia anasubiri ujio wa wimbo wake mwingine unaojulikana kwa jina la Tonight.
Dimpoz alirekodi wimbo huo kwa kushirikiana na msanii DJ Cleo wa Afrika Kusini wakati msanii huyo alipokuwepo nchini kwa ziara ya kimuziki mapema mwaka huu. Wimbo huo ulirekodiwa kwenye studio za B Hits za Dar es Salaam.
DJ Cleo aliondoka na demo ya wimbo huo kwa ajili ya kwenda kumalizia kazi ya kuurekodi nchini kwao na kazi hiyo imeshakamilika.
Kwa mujibu wa Dimpoz, wimbo huo unatarajiwa kuanza kusikika hivi karibuni baada ya CD yake kuwasili nchini.
“Nashukuru na nimefurahi sana kwamba nimepata bahati ya kurekodi wimbo na mmoja wa wasanii nyota wa muziki wa hip hop barani Afrika,”alisema Dimpoz. “Nilichokifanya ni kumpatia demo yenye wimbo huo ili akamalizie kwao kazi ya kuingiza sauti na kuchanganya mipigo ili kuiongezea ubora na akishairejesha, wimbo utakuwa umekamilika,”aliongeza msanii huyo. Dimpoz alisema amerekodi wimbo huo katika miondoko ya soul. Kwa sasa Dj Cleo anatamba na songi lake la 'Facebook'.

No comments:

Post a Comment