KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, June 11, 2012

Korti Kuu kutatua utata umri wa Lulu

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeamua kusikiliza maombi ya msanii wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba, kuhusu umri wake.
Akitoa uamuzi jana, Jaji Fauz Twaib, pia amesema uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kukataa ombi la upande wa utetezi la kutaka ufanywe uchunguzi wa umri wa Lulu lilikuwa kosa kisheria na na kuwa ilikwepa jukumu lake, suala ambalo imetupilia mbali.
Jaji Twaib alisema kuwa maombi ya Lulu yalikuwa si sahihi kuwasilishwa mahakamani hapo kwa sababu yaliwasilishwa kinyume na utaratibu wa sheria.
Jaji huyo alisema upande wa waombaji haukuwasilisha ombi la kupitia shauri hilo baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa uamuzi, hivyo umekwenda katika mahakama hiyo kinyume cha utaratibu.
Hata hivyo, Jaji Twaib alisema kwa kuwa mahakama ina kumbukumbu za mwenendo wa kesi kwa kutumia uwezo wake wa kuangalia uhalali wa mashauri yanayoendeshwa na mahakama za chini, imeamua kufanya uchunguzi wa suala la umri wa Lulu.
“Kwa kutumia uwezo wa Mahakama Kuu kuangalia uhalali wa mashauri yanayoendeshwa katika mahakama za chini. Nimeamua suala la umri wa Lulu litangaliwa Mahakama Kuu na kusikilizwa,” alisema jaji huyo.
Jaji Twaib aliamuru upande wa mwombaji (Lulu) anayewakilishwa na mawakili Fulgence Masawe na Peter Kibatala kuwasilisha viapo, vielelezo vya maandishi na ushahidi kuhusu umri wa Lulu. Pia upande wa mashitaka unaowakilishwa na Elizabeth Kaganda umetakiwa kuwasilisha vielelezo.
Jaji Twaib aliuamuru upande wa waombaji kuwasilisha ushahidi wao wa viapo, vielelezo vya maandishi na vielelezo kuhusu umri wa Lulu ifikapo kesho na upande wa mashitaka uwasilishe ushahidi wao kama wanao Juni 20, mwaka huu.
Alisema iwapo upande wa waombaji utakuwa na majibu uwasilishe Juni 22, mwaka huu na maombi hayo yatasikilizwa Juni 25, mwaka huu.
Kupitia mawakili wake, Lulu aliwasilisha maombi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako ndiko iliko kesi ya msingi inayomkabili kutupilia mbali ombi lake la kutaka suala lake lisikilizwe kwa kuzingatia Sheria ya Watoto.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliamua kutupilia mbali ombi hilo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo, na kuutaka upande wa utetezi iwapo ulikuwa na hoja kuhusu suala hilo upeleke Mahakama Kuu.
Katika Mahakama Kuu, maombi ya Lulu yalipigwa na upande wa mashitaka kwa madai kuwa hakupaswa kuyawasilisha ila alitakiwa kuiomba mahakama hiyo ipitie uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Kisutu au kukata rufani kupinga uamuzi huo.

No comments:

Post a Comment