KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 20, 2012

MANJI AFUNGAKAZI YANGA

WAGOMBEA wa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti katika uchaguzi mkuu wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji (kushoto) na Clement Sanga wakisalimiana walipokutana jana kwenye hoteli ya Protea mjini Dar es Salaam. Manji na Sanga walikuwa wamewekewa pingamizi na baadhi ya wanachama ili wasigombee katika uchaguzi huo. (Picha na Emmanuel Ndege).



Mgombea wa nafasi ya mwenyekiti katika uchaguzi wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji akiwa amezungukwa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo alipofika kwenye hoteli ya Protea mjini Dar es Salaam jana kwa ajili ya kusikiliza pingamizi alilowekewa kugombea wadhifa huo.


PINGAMIZI lililowekwa na wanachama Ishashabaki Ruta, Amadhi Mohamed na Alfons John wa Yanga kwa mgombea wa nafasi ya mwenyekiti, Yussuf Manji limetupwa baada ya wanachama hao kuingia mitini.
Ishashabaki, Amadhi na Alfons walitakiwa kufika kwenye hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay mjini Dar es Salaam jana kwa ajili ya kutoa vielelezo zaidi kuhusu pingamizi hizo, lakini hawakutokea.
Kamati ya uchaguzi ya Yanga chini ya mwenyekiti wake, Jaji mstaafu John Mkwawa iliitisha kikao hotelini hapo jana kwa ajili ya kusikiliza pingamizi hizo na ile aliyowekewa mgombea wa nafasi ya makamu mwenyekiti, Clement Sanga.
Manji alifika kwenye ukumbi wa hoteli hiyo mapema kwa ajili ya kusikiliza pingamizi hilo na kupokewa kwa shangwe na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo.
Hata hivyo, hadi ilipofika saa saba mchana, Ishashabaki na wenzake hawakutokea ukumbini na kusababisha pingamizi zao zishindwe kusikilizwa na Manji kuruhusiwa kuondoka.
Katika pingamizi zao, Ishashabaki na wenzake walidai kuwa Manji hastahili kuwania wadhifa wa uenyekiti kwa sababu tayari ni mfadhili na mdhamini wa Yanga hivyo hawezi kutenda haki kwa wanachama.
Pingamizi zingine zilizowekwa na wanachama hao zilidai kwamba, Manji ana maadui wengi ndani ya Yanga na pia amesababisha migogoro mingi na pia kuwahonga baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji katika uongozi wa mwenyekiti wa zamani, Lloyd Nchunga wajiuzulu.
Licha ya pingamizi hizo kutupwa, habari zilizopatikana baadaye zilieleza kuwa, kamati ya uchaguzi ya Yanga ilibaini kwamba, hakukuwa na jina wala namba ya mwanachama aliyejitambulisha kwa jina la Ishashabaki kwenye rejesta ya wanachama ya klabu hiyo.
“Upo uwezekano mkubwa mtu aliyeweka pingamizi hilo alitumia jina na namba bandia ya uanachama kwa sababu kwenye rejesta ya wanachama wa Yanga, hakuna jina hilo,”kilisema chanzo cha habari.
Kamati hiyo pia haikuweza kusikiliza pingamizi alilowekewa Sanga baada ya wanachama waliomwekea pingamizi hilo, Abdalla Mohamed na Kibedi Mwambebule nao kuingia mitini.
Katika pingamizi zao, Abdalla na Kibedi walidai kuwa, Sanga alikuwepo kwenye uongozi wa zamani wa mwenyekiti, Iman Madega, ambao uliondolewa madarakani baada ya kutokea hali ya kutokuelewana kati yao na wanachama.
Hata hivyo, kamati ilibaini kuwa, licha ya Sanga kuteuliwa kwenye uongozi huo, hakuweza kufanyanao kazi kwa vile alikuwa nje ya nchi kikazi na aliporudi, alikuta uongozi huo umeshaondoka madarakani.
Akizungumza na Burudani wakati akiondoka kwenye hoteli hiyo, Manji alisema pingamizi alilowekewa halikuwa na msingi kwa sababu anayo haki kikatiba kuwania nafasi yoyote ya uongozi.
Manji alisema kuwa mfadhili wa klabu hiyo, hakumzuii kugongea nafasi nyingine ya uongozi na kuongeza kuwa, lengo lake ni kuiletea klabu hiyo mafanikio makubwa zaidi.
Katika hatua nyingine, timu ya Yanga imeendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa kwa michuano ya Kombe la Kagame huku idadi ya wachezaji wapya waliosajiliwa hivi karibuni ikiongezeka.
Katika mazoezi yaliyofanyika jana jioni kwenye uwanja wa Kaunda mjini Dar es Salaam, wachezaji wapya waliohudhuria ni pamoja na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, Nizar Khalfan, Saidi Bahanuzi na Juma Abdul.
Mazoezi hayo yaliyohudhuriwa na mashabiki lukuki, yalikuwa chini ya Kocha Msaidizi, Fred Felix Minziro na kocha wa makipa, Mfaume Athumani.

No comments:

Post a Comment