KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 20, 2012

Imetosha kwa Mkwasa kuifundisha Twiga Stars, atafutwe kocha mwingine

Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Boniface ambaye ametangaza kujiuzulu

Kikosi cha Twiga Stars


TIMU ya soka ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars mwishoni mwa wiki iliyopita ilishindwa kufuzu kucheza fainali za Afrika baada ya kuchapwa bao 1-0 na Ethiopia.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Twiga Stars ilikuwa ikihitaji ushindi wa bao 1-0 ili ifuzu kucheza fainali hizo zitakazofanyika Septemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Kipigo hicho kiliifanya Twiga Stars itolewe kwa jumla ya mabao 3-1, kufuatia kuchapwa mabao 2-1 na Ethiopia katika mechi ya awali iliyochezwa wiki tatu zilizopita mjini Addis Ababa.
Kipigo ilichokipata Twiga Stars kilipokelewa kwa huzuni kubwa na mamia ya mashabiki waliofurika kwenye uwanja huo, ambao wengi walitarajia kuwa wangerejea nyumbani wakiwa na furaha kubwa.
Walikuwa na matumaini hayo kutokana na mafanikio iliyoyapata timu hiyo katika michuano ya hivi karibuni, ambapo ilifuzu kucheza fainali za Afrika mwaka 2010, fainali za All Africa Games zilizofanyika mwaka jana nchini Msumbiji na pia kualikwa kwenye mashindano ya (COSAFA) yaliyofanyika mwaka huo huo nchini Afrika Kusini.
Licha ya kutofika mbali katika michuano hiyo mitatu mikubwa, kiwango kilichoonyeshwa na Twiga Stars na upinzani ilioutoa kwa vigogo kama vile Zimbabwe, Afrika Kusini, Ghana na Nigeria ni miongoni mwa mambo yaliyowafanya watanzania wengi waanze kuvutiwa na timu hiyo.
Hata hivyo, mambo yamekwenda kinyume na matarajio ya Watanzania wengi. Twiga Stars ilianza vyema michuano hiyo kwa kuitoa Namibia katika raundi ya kwanza, lakini safari yake imeishia mikononi mwa Waethiopia.
Kutokana na kipigo hicho, Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo kwa kile alichodai timu hiyo kutothaminiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mbali na kutothaminiwa na TFF, Mkwasa amedai pia kuwa, timu hiyo haikuwa na maandalizi mazuri na shirikisho hilo lilionekana dhahiri kutoijali kama ilivyo kwa timu ya taifa ya wanaume, Taifa Stars.
Uamuzi uliochukuliwa na Mkwasa ni wa kijasiri na unastahili kupongezwa kwa sababu unaonyesha wazi jinsi alivyo tayari kuwajibika kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo bila kujali kiini cha tatizo kipo wapi.
Ukweli ni kwamba, Mkwasa atakumbukwa kwa kuifikisha juu timu hiyo, akiiwezesha kushiriki fainali za Afrika miaka miwili iliyopita nchini Afrika Kusini, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo.
Safari ya Twiga Stars kisoka ilianza mbali, miaka ya mwishoni mwa miaka ya 1990, wakati huo ikiwa inaundwa na wachezaji wengi kutoka timu ya Sayari, iliyokuwa na maskani yake Magomeni, Dar es Salaam.
Twiga Stars pia imepitia mikononi kwa makocha wengi. Alikuwepo marehemu Suleiman Gwaje, akaja marehemu Iddi Machuppa na baadaye ikawa chini ya Mkwasa na Mohammed Rishard Adolph. Kabla ya Mkwasa kujiuzulu, alikuwa akiinoa timu hiyo kwa kushirikiana na Nasra Juma kutoka Zanzibar.
Mafanikio ya Twiga Stars kimataifa yalianza kuonekana chini ya Mkwasa, ambaye ndiye aliyeiongoza katika fainali za Afrika, fainali za All Africa Games na fainali za COSAFA. Kwa jumla, kocha huyo ndiye aliyeiingiza Twiga Stars kwenye ramani ya kimataifa kisoka.
Hata hivyo, kushindwa kwa Twiga Stars kufanya vizuri katika michuano ya mwaka huu kumeacha maswali mengi, hasa kutokana na kiwango cha chini ilichoonyesha katika mechi za kirafiki dhidi ya Zimbabwe, Afrika Kusini na Ethiopia.
Katika mechi hizo tatu, wachezaji wa Twiga Stars walishindwa kucheza kwa uelewano na ilikuwa haieleweki aina ya mfumo wanaocheza. Pia hawakuwa na stamina ya kutosha. Ilikuwa kama vile ni timu iliyofanya mazoezi kwa kipindi kifupi.
Akizungumza baada ya mechi dhidi ya Ethiopia, Boniface alikiri kuwa, kipigo walichokipata kilitokana na wachezaji wake kuwadharau wapinzani wao na pia kujiamini kupita kiasi. Hakuzungumza chochote kuhusu wachezaji wake kushindwa kufuata maelekezo yake ama timu kutothaminiwa na TFF.
Ni dhahiri kwamba uwezo wa Mkwasa kuinoa timu hiyo sasa umeanza kupungua na anahitajika mtu mwingine kuchukua nafasi yake. Hii ni kwa sababu amekaa na wachezaji wa timu hiyo kwa miaka mingi hivyo inawezekana wamemzoea kupita kiasi na pengine heshima yao kwake kuanza kupungua.
Ieleweke kuwa, kocha anapozoeana na kuwa karibu na wachezaji kwa miaka mingi, ni rahisi heshima na nidhamu kuanza kushuka kwa vile watamuona na kumchukuluia kama mwenzao.
Binafsi nampongeza sana Mkwasa kwa hatua aliyoweza kuifikisha timu hiyo katika michuano ya kimataifa, ambayo ni ya kujivunia kwa timu zetu za taifa za soka. Lakini ni wazi kwamba, kwa sasa timu hiyo inahitaji changamoto nyingine mpya.
Wapo makocha wengi wanaofaa kuinoa timu hiyo. Nakumbuka kuna wakati Mkwasa na Adolph walipokwenda masomoni nje ya nchi, timu hiyo ilikuwa chini ya Kocha Rogasiun Kaijage na ilionyesha maajabu makubwa uwanja wa Uhuru baada ya kuitandika Eritrea mabao 6-1.
Katika mechi hiyo, wachezaji wa Twiga Stars walionyesha soka ya kufundishwa. Kila aliyeshuhudia mechi hiyo, alirejea nyumbani moyo wake ukiwa umeridhika si tu kutokana na ushindi huo mkubwa, bali pia kiwango kilichoonyeshwa na timu hiyo.
Pengine wakati sasa umefika kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumpatia nafasi hiyo Kaijage, ambaye pia ni mtaalamu wa kufundisha soka ya vijana. Ni wazi kuwa, Twiga Stars inahitaji changamoto mpya, ari mpya na mbinu mpya hivyo mabadiliko ni muhimu kwa wakati huu.

No comments:

Post a Comment