Jumla ya timu za shule za sekondari 24 kutoka mikoa sita zilishiriki michuano ya Airtel Rising Stars kwa mwaka huu huku wachezaji bora wakichanguliwa kuunda timu kombaini za mikoa kwa ajili ya fainali za taifa. Mikoa iliyoshiriki ni Lindi, Mbeya, Arusha, Ilala, Kinondoni na Temeke.
Shule hizo zilichanguliwa kutokana na kufanya vizuri kwenye michuano ya taifa ya shule za sekondari (UMISSETA) mwaka jana. Uzinduzi rasmi wa ARS 2012 ulifanyika Mei, kwenye Hoteli ya Sea Cliff jijini Dar es Salaam na mchezaji wa zamani wa Klabu ya Manchester United ya Uingereza, Quinton Fortune.
Fainali za ARS za wiki moja pia zimetumika kuchangua timu ambayo itawakilisha Tanzania kwenye michuano ya ‘inter-continental’ ambayo itashirikisha nchi 17 ambao Airtel inafanya biashara. Michuano hii itafanyika Nairobi mwezi wa Agosti.
Timu ya wavulana ya Temeke imepata nafasi ya kuwa bingwa wa Airtel Rising Stars 2012 baada ya kuifunga Mbeya 3-1 kwenye fainali kali ya kusisimua huku wasichana wa Mbeya wakiibuka bingwa baada ya kuwafunga wenzao wa Arusha 3-1.
Timu hizo mbili bingwa zilijinyakulia vitabu vya thamani ya Tshs milioni moja, medali ya dhahabu na vyeti vya kushiriki.
Michuano wa Airtel Rising Stars ni mpango kambambe kwa Afrika nzima ambao ni wa kutafuta na kukuza vipaji vya soka vinavyochipukia kwa wavulana na wasichana wenye miaka chini ya kumi na saba ambao watapata muda wa kuonyesha vipaji vyao na kukutana na wataalamu wa mpira wa miguu ambao watawapa mafunzo zaidi na kupata nafasi ya kukuza vipaji vyao.
Airtel Rising Stars ni ushirikiano kati ya Airtel na klabu ya Uingereza ya Manchester United ya kukuza vipaji vya soka barani Afrika. Huu ni mwaka wa pili kwa Airtel kudhamini michuano hii. Mwaka jana, Klabu ya Manchester United ilitoa walimu wake wa soka ya vijana kuendesha kliniki ya soka ya Kimataifa ambazo kliniki hizo zilifanyika Tanzania, Afrika Kusini na Gabon.
No comments:
Post a Comment