KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, June 15, 2012

Kazi za wasanii sasa kutozwa ushuru

WAZIRI wa Fedha, Dk. William Mgimwa amesema serikali itatoza ushuru wa bidhaa za muziki na filamu kupitia DVD,VCD na mikanda ya video.
Akiwasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2012 Bungeni jana, Dk. Mgimwa alisema hatua hiyo inalenga katika kurasimisha biashara ya bidhaa hizo na kuhakikisha uasili wake unatambulika na hivyo kuzuia kudurufu kazi za sanaa.
Dk. Mgimwa alisema vitendo vya kudurufu bidhaa hizo vinadumaza ukuaji wa sanaa na vipaji kwa wasanii wa Tanzania.
Alisema ili kutekeleza hatua hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaweka stampu kwenye bidhaa hizo ili kurahisisha utozwaji wa ushuru kwenye bidhaa hizo.
Dk. Mgimwa alisema kwa kuwa kunahitajika maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kurekebisha sheria na kanuni mbalimbali, utekelezaji wa hatua hiyo utaanza Januari Mosi 2013.
Hatua hiyo ya serikali kuanza kutoza ushuru kwa bidhaa za muziki na filamu, itakuwa mkombozi mkubwa kwa wasanii wa Tanzania, ambao kwa miaka mingi sasa wamekuwa wakilalalamikia wizi wa kazi zao.
Wizi huo umekuwa ukifanywa na wafanyabiashara wanaomiliki vifaa vya kurekodia nyimbo na filamu, ambapo wamekuwa wakidurufu kanda zao na kuziuza kwa bei ya chini.
Licha ya jitihada za polisi na wasanii kuwakamata watu hao mara kwa mara, kazi hiyo imeonekana kuwa ngumu kutokana na mtandao wa wafanyabiashara hao kuwa mkubwa na kutapakaa nchi nzima.

No comments:

Post a Comment