KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 27, 2012

Mwogeleaji aongezeka kambi ya Olimpiki

MWOGELEAJI Magdalena Moshi wa Tanzania anatarajiwa kujiunga na wachezaji wenzake watakaoshiriki katika Michezo ya Olimpiki mwishoni mwa wiki hii.
Magdalena ndiye mwogeleaji pekee wa Tanzania aliyefuzu kucheza katika michezo hiyo inayotarajiwa kuanza mwezi ujao katika Jiji la London nchini Uingereza.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Noel Kiunsi amesema Magdalena alitarajiwa kutua nchini jana akitokea Australia ambako anasoma.
"Ni kweli tumepata nafasi ya kupeleka mchezaji mmoja kwenye michezo hiyo mikubwa duniani, na kama ujuavyo, Magdalena yuko nje ya nchi kwa ajili ya masomo, lakini kulingana na taarifa zilizopo, anatarajia kuwasili nchini leo (jana) au kesho (leo)," alisema.
Kiunsi alisema mara mchezaji huyo atakapofika nchini, watawasiliana na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), ambayo ndiyo inayosimamia kambi hiyo.
Michezo ya Olimpiki imepangwa kuanza Julai 27 hadi Agosti 12 mwaka huu na Tanzania itawakilishwa na wanamichezo sita.
Akizungumzia nafasi ya Magdalena katika michezo hiyo, Kiunsi alisema itakuwa vigumu kwake kufanya vizuri kutokana na kupata nafasi hiyo kwa upendeleo.
Kwa mujibu wa Kiunsi, Magdalena amepewa nafasi hiyo na Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Kuogelea (FINA).
“Hii itakuwa mara ya pili kwa Magdalena kushiriki kwenye michezo ya kimataifa, lakini nafasi yake kubwa ni kuongeza rekodi yake anayoishikilia sasa,”alisema.
Wanamichezo wengine wa Tanzania watakaoshiriki katika michezo hiyo ni wanariadha Samsoni Ramadhan, Msenduki Mohammed (marathoni) na Zakia Mrisho (mita 5,000) na bondia Seleman Kidunda anayecheza uzito wa kilogramu 69.

No comments:

Post a Comment