KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 27, 2012

Hussein Machozi ataka kuhamia Kenya

MSANII machachari wa muziki wa bongo fleva nchini, Hussein Machozi amesema anafikiria kuhamishia shughuli zake za muziki katika nchi jirani ya Kenya.
Hussein alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa muziki wake unakubalika na kuthaminiwa zaidi nchini humo kuliko Tanzania.
Msanii huyo, ambaye mara nyingi amekuwa akiweka kambi Kenya kila anapojiandaa kutoa wimbo mpya, ameweka wazi kuwa anataka kuhama Tanzania kwa vile kumejaa wanafiki wengi wa kimuziki.
Alipotakiwa kufafanua kuhusu madai yake ya kuwepo kwa unafiki mwingi wa kimuziki bongo, Hussein alisema waandishi wa habari wamechangia kuwepo kwa hali hiyo.
“Okay, watu wa media hawako free kabisa, yaani huwa wanafuata upepo wanapoanzisha wale wenye nguvu,”alisema msanii huyo.
“Yaani wakitaka kumtoa mtu wao na media zingine zinafuata, wala hawashtuki kuwa analazimishwa atoke wakati kuna ngoma kibao kali wanazipotezea ili mtu wao apite. Matokeo yake wanatoa ngoma moja inapata umaarufu, baada ya hapo ni pumba tupu. Huwa inaniuma sana,” aliongeza msanii huyo.
“Kwa Kenya mambo hayo hakuna kabisa. Kule kama ngoma ni kali,itatandikwa hadi noma, ila kama ni mbaya, huwezi hata kuiskia,”alisisitiza msanii huyo asiyekuwa na makeke.
”Nakubalika zaidi Kenya kwa sababu ngoma zangu ni kali na zina kichwa na miguu, namaanisha wimbo unakuwa na stori ya kufuatilia na inaskilizika na rika zote, nadhani hii ni sababu tosha sana,” alisema Machozi.
Hivi karibuni, msanii huyo alirekodi wimbo wake mpya unaojulikana kwa jina la Addicted, akiwa amemshirikisha msanii anayetamba nchini Kenya kwa sasa, Size 8.
Hussein alisema ameamua kurekodi wimbo huo kwa ajili ya mashabiki wake wa kike na kuongeza kuwa, video ya wimbo huo itatengenezwa na Kampuni ya Ogopa DJs.
Msanii huyo, ambaye amekuwepo nchini Kenya tangu wakati wa sikukuu ya Pasaka, amekuwa akifanya maonyesho mbalimbali, hasa katika mji wa Mombasa na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki.
Kabla ya kurekodi kibao hicho, Hussein aliibuka na wimbo wa Jela, ambao unazungumzia matatizo mbalimbali ya kimaisha, ambayo husababisha vijana wengi kuishia huko.
Akizungumzia changamoto, ambazo amekuwa akikabiliana nazo katika kurekodi nyimbo zake hapa nchini, Hussein alisema ni gharama kubwa za kurekodi wimbo studio.
Alisema gharama hizo na zile za kurekodi video zimekuwa kubwa kiasi cha kuwafanya wasanii wengi washindwe kuzimudu na hivyo kukaa kimya kwa muda mrefu ama kuachana na fani hiyo.
Hussein alisema chanzo kikubwa cha kupanda kwa gharama hizo ni matatizo ya umeme, ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara hapa nchini.

No comments:

Post a Comment