KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, June 15, 2012

Mzee Mwinyi amwaga maneno mazito tuzo za TASWA

RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi amewataka viongozi wa vyama vya michezo nchini kuwachukulia hatua watu watakaobainika kupanga matokeo katika mechi mbalimbali.
Mwinyi amesema upangaji wa matokeo ni hatari katika michezo kwa vile unachangia kushusha viwango vya michezo na kuzipa ushindi timu zisizostahili.
“Tuhuma za upangaji matokeo zisipuuzwe, kama kweli zipo ni mbaya, na kama ni za uongo, basi ni bora zibaki hivyo hivyo,” alisema Rais huyo mstaafu, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Mzee Ruska.
Mwinyi alisema hayo juzi wakati wa sherehe za utoaji wa tuzo za wanamichezo bora zilizoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) na kufanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Alisema kutokana na tuhuma hizo kujitokeza mara kwa mara katika michezo mbalimbali, hasa soka, ni vyema viongozi wa vyama husika wazifanyie kazi ili zisigharimu sura ya michezo nchini.
Rais huyo mstaafu alisema katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika michuano mbalimbali ya kimataifa na imeanza kuondokana na hadithi ya ‘kichwa cha mwendawazimu’, ambacho kila anayejifunza kunyoa, anakitumia.
“Huko nyuma niliwahi kuzifananisha timu zetu na kichwa cha mwendawazimu, ambacho kila anayejifunza kunyoa, anakitumia. Tuwe na subira, hadithi ya kichwa cha mwendawazimu sasa inaanza kutoweka,”alisema rais huyo mstaafu huku akishangiliwa na wanamichezo mbalimbali waliohudhuria sherehe hizo.
Aliipongeza TASWA kwa kuweka utaratibu wa kutoa tuzo kwa wanamichezo bora wa michezo mbalimbali kila mwaka na kuongeza kuwa, utaratibu huo umesaidia kuamsha ari ya vijana.
Rais huyo mstaafu alizitaka kampuni mbalimbali ziache kuelekeza udhamini wao katika mchezo wa soka pekee, badala yake zigeukie michezo mingine.
“Udhamini katika michezo using’ang’anie soka na michezo mikubwa, uende na kwenye michezo mingine,”alisema.
Alivitaka vyama vya michezo vijikite zaidi katika kuibua vipaji vya vijana na kuwaendeleza na kwamba vipaji hivyo vitafutwe mikoani na vijijini badala ya Dar es Salaam pekee.
“Wapo vijana wengi wenye vipaji vya michezo mbalimbali, lakini hatuwajui, hatuwatambi na hatuwaendei walipo,”alisema Rais Mwinyi na kusisitiza kuwa, ni vigumu kwa nchi kupata mafanikio kimichezo bila kuwekeza kwa vijana.
Akitoa mfano, alisema kutaka maendeleo ya haraka kimichezo bila kufanya jitihada za kuibua vipaji vya vijana na kuwaendeleza ni sawa na kutamani kwenda peponi kabla ya kufa.
Rais mstaafu pia amewataka waandishi wa habari za michezo nchini kuacha ushabiki wanaporipoti habari za michezo, badala yake wajikite zaidi katika kueleza ukweli na hali halisi.
Alisema inafurahisha kuona kuwa, habari za migogoro zimeanza kupungua kwenye vyombo vya habari, lakini baadhi ya waandishi wanaweka mbele zaidi ushabiki.
“Linapokuja suala la uteuzi wa timu, utaona baadhi ya waandishi wanahoji mbona fulani hayupo? Tuwaache makocha wafanyekazi yao,”alisema huku akishangiliwa.
Mapema akifungua sherehe hizo, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto alisema chama chake kimekuwa kikiziboresha tuzo hizo kila mwaka kwa lengo la kuzipa hadhi na heshima zaidi kwa wanamichezo.
Pinto aliipongeza Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa kudhamini tuzo hizo kwa mwaka wa pili mfululizo na pia kuboresha udhamini wake.

No comments:

Post a Comment