KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, June 25, 2012

Milovan atua Dar, timu kurejea leo usiku kutoka Mwanza

KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amerejea nchini kwa ajili ya kuendelea kuinoa timu hiyo kwa michuano ya Kombe la Kagame na msimu ujao wa ligi.Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga ameieleza blogu ya liwazozito leo kuwa, Milovan aliwasili nchini usiku wa kuamkia leo akitokea kwao Serbia alikokwenda kwa mapumziko.

Kwa mujibu wa Kamwaga, kocha huyo alitua kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki na kupokewa na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo.

Milovan alikwenda kwao kwa mapumziko mara baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, ambapo aliiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa.

Kurejea kwa kocha huyo kumemaliza uvumi uliokuwa umezagaa kwamba, huenda asingerudi baada ya kutofautiana na viongozi wa Simba kuhusu mkataba mpya.

Wakati Milovan akiwa amerejea nchini, kikosi cha Simba kilichokwenda Mwanza na Shinyanga kwa ajili ya ziara ya mechi za kirafiki, kinatarajiwa kurejea Dar es Salaam usiku huu kwa ndege kikitokea Mwanza.

Simba ilicheza mechi yake ya kwanza Jumamosi kwa kumenyana na Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara walicheza mechi ya pili jana dhidi ya Express ya Uganda kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na kutoka nayo sare ya bao 1-1.

Katika mechi hizo mbili, Simba iliwatumia wachezaji wake kadhaa wapya, akiwemo kiungo Kigi Makasi aliyesajiliwa kutoka Yanga.

No comments:

Post a Comment