KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 14, 2012

UKWA: SICHUKII WATU WANAPONIITA MTOTO AU SHOTII

Osita Iheme, maarufu kwa jina la Ukwa akiwa amepozi

Osita Iheme (kushoto) akiwa na swahiba wake, Chinedu (Aki) katika moja ya filamu walizocheza pamoja.


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Osita Iheme amesema ukimya wake katika fani hiyo katika siku za hivi karibuni hauna maana kwamba amekwisha kiusanii.
Osita, ambaye ni maarufu zaidi kwa majina ya Ukwa na Pawpaw amesema ukimya wake umetokana na kutovutiwa na hadithi ya filamu anazoombwa kucheza.
Aliitaja sababu nyingine, iliyomfanya awe kimya kwa muda mrefu kuwa ni hali ya soko la filamu kuwa mbaya na hivyo kuwaathiri wasanii wa fani hiyo.
Osita alisema havutiwa na utaratibu unaotumika sasa wa filamu moja kuwa na sehemu zaidi ya tatu. Alisema huko ni kufilisika kisanii.
Hata hivyo, msanii huyo mfupi na mwenye mvuto katika tasnia ya filamu nchini Nigeria alikiri kuwa, ni kweli ameamua kuongeza ada yake ya malipo kwa kila filamu atakayocheza.
Alikataa kutaja kiasi hicho cha malipo kwa madai kuwa, kinategemea makubaliano atakayoingia na mtayarishaji wa filamu pamoja na maelezo ya filamu.
Alipoulizwa kuhusu mipango yake ya baadaye katika tasnia hiyo, Osita alisema ameandaa programu maalumu kwa ajili ya kuibua vipaji vya vijana na kuwaendeleza.
Osita alisema kwa sasa anajitahidi kukusanya pesa kwa ajili ya vijana wasio na kazi, lakini wenye vipaji vya kuigiza ili awasaidie kimaisha.
Akizungumzia suala la kufunga ndoa, Osita alisema hana haraka ya kufanya hivyo kwa sababu kila kitu kinakwenda kwa mipango ya Mungu.
“Mungu ni mkubwa, kila kitu kitakwenda kinavyopaswa kuwa na kwa wakati utakaopangwa,”alisema. “Wakati wowote Mungu atakaposema ndio, hata kama itachukua miaka 20, ataniongoza njia ipi ya kwenda.”
Osita, ambaye hivi karibuni alikamilisha kazi ya kutengeneza filamu ya Kihausa, inayojulikana kwa jina la Karangiya alisema, katika maisha yake, hachukii anapokutana na watu na kumuita mtoto kutokana na umbile lake.
Msanii huyo alisema anaamini Mungu alimpa umbile alilonalo ili kumtofautisha na watu wengine na kufanya iwe rahisi kwake kujulikana popote atakapokwenda. Alisema umbo hilo limemfanya awe kivutio kwa watu wengine.
“Sichukii watu wanaponiita mtoto ama mfupi. Nikifanya hivyo ni sawa na kumuhoji Mungu. Najivunia kuwa nilivyo,”alisema.
Alisema aliamua kujitosa kwenye fani hiyo kwa sababu anaipenda na aliamini angeweza kufanya vizuri. Alisema anashukuru kwamba familia yake imekuwa ikimuunga mkono na kumuongezea ari na ndio sababu iliyomfanya aendelee nayo hadi sasa.
Hata hivyo, Osita alishindwa kueleza iwapo isingekuwa uigizaji, angejihusisha na kazi ipi. Alisema ni Mungu pekee, ambaye angeweza kumuongoza lipi la kufanya katika maisha yake.
Osita alisema amekuwa akizungumza vizuri lugha ya Kiingereza kutokana na mafunzo mazuri aliyoyapata tangu akiwa shule ya sekondari na pia kujiendeleza zaidi kimasomo.
Hadi sasa, Osita ameshacheza filamu zaidi ya 80 na zimemwezesha kuishi maisha mazuri ikiwa ni pamoja na kupata vitu vyote muhimu anavyovihitaji katika maisha yake.
“Siwezi kusema kama ni milionea au bilionea, lakini cha msingi ni kwamba, ninaridhika na maisha ninayoishi,”alisema.
Osita alisema hatarajii kustaafu fani hiyo hivi karibuni na kusisitiza kuwa, ataendelea na uigizaji maisha yake yote kwa sababu fani hiyo haina umri wa mwisho.
“Hata kama nitafanya vitu vingine, nitaendelea kuwa mwigizaji. Naweza kuwa mwigizaji hata nitakapofikisha umri wa miaka 100,”alisema.

No comments:

Post a Comment