KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 27, 2012

Yanga sasa wajifua mchana

BENCHI la ufundi la klabu ya Yanga limeamua kubadilisha programu ya mazoezi kwa wachezaji wake kutoka asubuhi hadi mchana.
Yanga pia imeamua kuhamisha uwanja wake wa mazoezi kutoka Kaunda uliopo Jangwani kwenda shule ya sekondari ya Loyola iliyopo Mabibo, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, timu hiyo ilifanya mazoezi yake kwa muda asubuhi kwenye uwanja wa Kijitonyama.
Sendeu alisema walilazimika kufanya mazoezi kwa muda kwenye uwanja huo ili kukamilisha mipango ya kuhamia Loyola.
Awali, Yanga ilikuwa ikifanya mazoezi nyakati za asubuhi, lakini Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fred Felix Minziro na msaidizi wake, Mfaume Athumani wameamua mazoezi hayo yawe yakifanyika mchana.
Hata hivyo, Sendeu hakuweka wazi kuhusu uamuzi wa makocha hao kubadili muda wa mazoezi.
Yanga inajiandaa kwa michuano ya Kombe la Kagame, iliyopangwa kuanza Julai 14 hadi 29 mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Michuano hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, pia itazishirikisha timu za Azam na mabingwa wa Tanzania Bara, Simba. Yanga ni bingwa mtetezi.
Kwa sasa, Yanga bado ipo kwenye mchakato wa kusaka kocha mkuu mpya baada ya kocha wa zamani, Kostadin Papic kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu uliopita.
Ilielezwa kuwa, uongozi wa klabu hiyo upo kwenye mazungumzo na kocha wa zamani wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo, lakini imeamua kufuta mpango huo.
Kikosi cha sasa cha Yanga kinaundwa na wachezaji wengi wapya, wakiwemo kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na beki Kelvin Yondan waliosajiliwa kutoka Simba, Ladislaus Mbogo kutoka Toto African, viungo Frank Damayo kutoka JKT Ruvu, Nizar Khalfan aliyekuwa anakipiga Marekani na mshambuliaji Simon Msuva kutoka Moro United.

No comments:

Post a Comment