KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 27, 2012

Mume wa Omotola ampa somo mume wa Ini Edo

Omotola Jalade akiwa na mumewe, kepteni Mathew Ekeinde

Ini Edo (kulia) akiwa na mumewe, Philip Ehiagwina

LAGOS, NIGERIA
MUME wa mcheza filamu nyota wa Nigeria, Omotola Jalade, Kepteni Mathew Ekeinde ametoa somo kwa mume wa mcheza sinema mwingine, Ini Edo.
Kepteni Ekeinde, ambaye ni rubani wa ndege amemweleza mume wa Ini, Philip Ehiagwina kwamba hapaswi kupandwa na hasira mkewe anapoandikwa vibaya na vyombo vya habari.
Ekeinde amemtaka Philip azipuuze habari hizo kwa sababu hiyo ndiyo gharama ya umaarufu na kuongeza kuwa, habari nyingi zinazoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari ni za kupika.
“Miaka michache iliyopita, (Philip) aliripotiwa akiwaonya waandishi wa habari wa Nigeria wasindike habari mbaya kuhusu mkewe, Ini Edo. Kwa mujibu wa habari hizo, iwapo watafanya hivyo, atawachukulia hatua za kisheria,”alisema Ekeinde.
“Swali la kujiuliza ni kwamba, kama hawezi kuwa na mke maarufu, kwa nini asingeoa mke wa kawaida ? Kama angekuwa ndiye Rais Goodluck Jonathan, angewakata waandishi wote walioandika habari mbaya kuhusu mkewe, Patience?”
“Kwa nini asijifunze kutoka kwa Kepteni Mathew Ekeinde jinsi ya kumudu kuishi na mke maarufu? Pengine ni vizuri ajifunze kutokasirika pale zinaporipotiwa habari mbaya kuhusu mkewe Ini Edo kama ambavyo Kepteni Mathew amefanya kwa Omotola,”alisema.
“Tafadhali msinielewe vibaya, simaanishi kwamba waandishi wa habari wasiandike habari za uongo kuhusu watu, lakini kama hilo litatokea, vyombo vya sheria vipo kushughulikia suala hilo,”alisisitiza.
Ekeinde ametoa ushauri huo kwa Philip kufuatia kauli aliyoitoa hivi karibuni ya kukanusha mkewe Ini Edo kuonekana kwenye ukumbi wa burudani akiwa na mwanaume mwingine.
Philip aliielezea taarifa hiyo iliyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa, haikuwa ya kweli na ililenga kumchafua mkewe.
Kepteni Ekeinde alimuoa Omotola miaka 16 iliyopita na wamefanikiwa kuzaa watoto wanne. Walisherehekea ndoa yao kufikisha idadi hiyo ya miaka Machi 23 mwaka huu.
Ndoa nyingi za wacheza filamu wa kike wa Nollywood zimekuwa hazidumu kwa miaka mingi kutokana na sababu mbalimbali, lakini ndoa ya Kepten Ekeinde na Omotola imedumu kwa miaka mingi na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kijamii wamesema wanandoa hao wanastahili tuzo.
Baadhi ya vyombo vya habari vya Nigeria vimekuwa vikiripoti habari nyingi kuhusu Omotola kuwa na uhusiano na wanaume wengine, lakini mumewe amekuwa akizipuuza na kukaa kimya.

No comments:

Post a Comment