KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 14, 2012

NURDIN BAKARI: Hakuna mwenye namba Taifa Stars

KIUNGO Nurdin Bakari ni mchezaji pekee wa klabu ya Yanga aliyemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kinachoshiriki katika michuano ya awali ya Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na ATHANAS KAZIGE, kiungo huyo anaelezea mambo mbalimbali kuhusu maisha yake kisoka.

SWALI: Hivi karibuni uliripotiwa kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja na kukufanya ushindwe kwenda Ivory Coast na timu ya Taifa Stars. Vipi hali yako inaendelea kwa sasa?
JIBU: Namshukuru Mungu kwamba kwa sasa sijambo na ninaendelea vizuri. Pia nimeshaanza mazoezi na wachezaji wenzangu wa Taifa Stars. Nawashukuru sana madaktari na wauguzi walionihudumia.
Ninachoweza kusema ni kwamba kwa sasa nipo fiti na nimedhamiria kupigania namba kwenye kikosi cha kwanza. Kama unavyojua, kikosi chetu kwa sasa kinaundwa na wachezaji wengi vijana wenye ari na kasi kubwa uwanjani, hivyo bila kupigania namba, unaweza kujikuta ukiishia benchi.
SWALI: Haukuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza mechi ya kwanza dhidi ya Ivory Coast na pia hukupata nafasi ya kucheza mechi ya pili dhidi ya Gambia. Unajisikiaje kwa kukosa mechi hizo mbili muhimu?
JIBU:
Nilikosa mechi ya kwanza kwa sababu nilikuwa majeruhi. Katika mechi ya pili nilivaa jezi, lakini sikupata nafasi ya kucheza.Kwa kifupi, nawapongeza wachezaji wenzangu kwa kucheza kwa kujituma katika mechi zote mbili. Ni bahati mbaya tu kwamba tulipoteza mechi yetu ya kwanza dhidi ya Ivory Coast, lakini baada ya kuishinda Gambia, tumejiweka kwenye hali nzuri.
Sababu kubwa iliyotufanya tupoteze mechi ya kwanza dhidi ya Ivory Coast inaweza kuwa ni woga wa kupambana na baadhi ya wachezaji nyota duniani kama vile Didier Drogba, Salomon Kalou, Kolo Toure na wengineo.
Lakini baada ya kupewa mafunzo ya kina zaidi na Kocha, Kim Poulsen timu yetu imebadilika na sasa wachezaji wameanza kushika mafunzo yake.
Kama ulivyoona katika mechi yetu dhidi ya Gambia, timu inacheza kwa kutulia na kufanya mashambulizi kimpangilio. Kwa ujumla, wachezaji wameanza kucheza kwa kujiamini.
SWALI: Pamoja na timu kucheza vizuri, bado tatizo kubwa linaonekana katika ufungaji wa mabao. Unadhani tatizo hili linaweza kumalizika vipi?
JIBU: Tatizo la kufunga mabao lipo sehemu nyingi, si Tanzania pekee, hata kwa timu za mataifa ya nje. Tayari kocha wetu ameshaanza kulifanyiakazi na nina hakika baada ya muda si mrefu, ataweza kulipatia dawa.
Kasi ya Taifa Stars inatokana na kuwepo kwa mifumo miwili tunayoitumia kwa wakati mmoja. Huwa tunaanza kwa mfumo wa 4-4-2 na kubadili kwenda mfumo wa 4-5-1, ambao ni wa kufanya mashambulizi kwa kushtukiza.
SWALI: Unazungumziaje mechi yenu ijayo dhidi ya Morocco na za marudiano dhidi ya Ivory Coast na Gambia?
JIBU: Bado nina imani kubwa kwamba safari hii tunaweza kufanya vizuri zaidi kuliko michuano iliyopita. Morocco si timu ngeni kwetu, tumeshacheza nayo mara mbili.
Hata Msumbiji tutakayocheza nayo katika Kombe la Mataifa ya Afrika sio timu ya kutisha kwa sababu tulishacheza nayo katika mechi ya awali hapa nyumbani na kutoka nayo sare ya bao 1-1. Tunachotakiwa kufanya ni kuongeza ari zaidi.
SWALI: Mara baada ya TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kumkabidhi timu Kim Poulsen, tumeona amefanya mabadiliko makubwa ya wachezaji kwa kuwapa nafasi vijana wengi wapya. Una maoni gani kuhusu mabadiliko hayo?
JIBU: Uamuzi uliofanywa na Kim ni mzuri na unastahili kupongezwa kwa sababu timu hivi sasa inaundwa na wachezaji wachache wazoefu na wachache vijana. Hali hii imesababisha kuwepo na mchuano mkali wa kuwania namba kwenye kikosi cha kwanza.
Upo uwezekano mkubwa kwa baadhi ya wachezaji wengine wazoefu kupoteza namba kwa vijana chipukizi, ambao wana vipaji vya hali ya juu vya kucheza soka.
Hii imeleta changamoto kubwa katika timu kwa sababu kila mmoja anafanya jitihada kubwa ya kupata namba, lakini mwamuzi wa mwisho ni kocha. Na hii ndiyo siri ya mafanikio ya Taifa Stars hivi sasa.
Ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba hakuna mchezaji mwenye namba ya kudumu kwenye kikosi cha Taifa Stars na baadhi ya wachezaji wazoefu wamepatwa na woga wa kupoteza namba, hasa inapotokea wameumia.
SWALI: Hebu tuzungumzie kikosi cha Yanga, ambacho unakichezea hivi sasa. Unazungumziaje kuhusu uamuzi wa Yanga kuwasajili beki Kelvin Yondan wa Simba na Nizar Khalfan, aliyekuwa akicheza soka ya kulipwa Marekani?
JIBU: Ujio wa wachezaji hao ni muhimu katika Yanga kwa sababu wataweza kuongeza nguvu ili timu iweze kufanya vizuri katika michuano mbalimbali, ikiwemo Kombe la Kagame.
Nasema hivyo nikiwa na maana kwamba kusajiliwa kwa wachezaji hao kutaongeza changamoto ndani ya Yanga kwa vile kila mchezaji atahakikisha anajituma zaidi ili aweze kupata namba.
Lakini ukweli ni kwamba, Yanga inakabiliwa na jukumu zito la kuhakikisha inatetea vyema ubingwa wa Kombe la Kagame. Michuano hiyo ndiyo itakayotoa mwelekeo wa Yanga katika msimu ujao wa ligi.
SWALI: Kuna taarifa kwamba upo mbioni kuondoka Yanga na kujiunga na timu nyingine msimu ujao. Kuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizi?
JIBU: Mimi bado nipo Yanga kwa sababu nina mkataba hadi mwishoni mwa msimu ujao wa 2012/2013. Hata hivyo, bado naendelea na mazungumzo na baadhi ya mawakala kwa ajili ya kunitafutia timu nje ya nchi.
Awali nilipata timu mbili za nje ya nchi, lakini nilishindwa kwenda kutokana na klabu yangu ya Yanga kukabiliwa na michuano ya ligi kuu mzunguko wa pili na ile ya klabu bingwa barani Afrika kabla ya kutolewa
SWALI : Nini siri ya mafanikio yako katika soka?
JIBU:Sina lolote kubwa zaidi ya kuwashukuru makocha ambao wameninoa tangu utoto wangu, wakiwemo Raphael Mzambia, Paul Ndone na Madaraka Bendera na wengine walionifundisha nikiwa katika klabu za AFC ya Arusha, Simba na Yanga.

No comments:

Post a Comment