KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, June 29, 2012

Simba, Azam uso kwa uso Kombe la Urafiki

TIMU za soka za Simba na Azam zinatarajiwa kukutana katika michuano ya Kombe la Urafiki inayotarajiwa kuanza Jumatatu kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Simba na Azam ni miongoni mwa timu nane zilizoalikwa kushiriki kwenye michuano hiyo iliyolenga kuimarisha ujirani mwema katika michezo.

Wakati Simba na Azam zimethibitisha kushiriki kwenye michuano hiyo, Yanga imetangaza kujitoa kwa madai ya kutokuwa na maandalizi mazuri.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uamuzi wa kushiriki kwenye michuano hiyo umefikiwa kati ya benchi la ufundi na kamati ya ufundi.

“Tumeamua kushiriki kwa sababu tumeona haitakuwa vema kufanya hivyo wakati watu wa Zanzibar wametupa heshima kubwa ya kutualika kwenye michuano hii. Kombe la Urafiki lina maana kubwa kwa sasa kutokana na hali halisi ya kisiasa na kijamii iliyopo visiwani humo,"alisema.

Kaburu alisema pia kuwa, Simba itatumia fursa hiyo kuweka kambi maalumu kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Kagame iliyopangwa kufanyika kuanzia Julai 14 mwaka huu. Kwa mujibu wa Kaburu, Simba pia itatumia ziara hiyo ya Zanzibar kutembeza kombe la ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwa mashabiki wao wa huko, ambao alisema walichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa ubingwa huo.
“Tusisahau pia kwamba kabla ya kucheza mechi yetu ya mwisho dhidi ya watani wetu wa jadi Yanga, ambayo tulishinda kwa idadi ya mabao 5-0, Simba ilikwenda kuweka kambi Zanzibar,” alisema Kaburu.
Simba itaanza michuano hiyo siku ya Jumatatu usiku kwa kucheza na Mafunzo.

Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Jumatatu jioni, lakini imesogezwa mbele hadi Jumatatu usiku.
Jumla ya timu nane zinashiriki katika michuano hiyo, ambapo Waekundu wa Msimbazi wapo katika kundi A lenye timu za Azam, Mafunzo na timu ya soka ya taifa ya vijana ya Zanzibar wenye umri wa chini ya miaka 23 (Karume Boys).
Wakati huo huo, Simba inatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Express ya Uganda, itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Awali, Simba ilicheza na Express wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, ambapo zilitoka sare ya bao 1-1.

No comments:

Post a Comment