KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 7, 2012

Kuziona Stars, Gambia buku tatu

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio vya mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 kati ya timu ya Taifa, Taifa Stars na Gambia.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kiingilio cha chini kati mechi hiyo itakayochezwa Jumapili kitakuwa sh. 3,000.
Wambura alisema watazamaji watakaolipa kiingilio hicho ni watakaokaa kwenye viti vya rangi ya bluu na kijani, ambavyo idadi yake ni 36,693 kati ya jumla ya viti 57,558 vilivyopo katika uwanja huo wa kisasa.
Kwa mujibu wa Wambura, kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ni sh. 5,000, VIP C sh. 10,000 wakati VIP B ni sh. 20,000. Alisema kiingilio kwa jukwaa la VIP A, ambalo linachukua watazamaji 748 ni sh. 30,000.
Wambura alisema mechi hiyo imepangwa kuanza saa 10 jioni na tiketi zitaanza kuuzwa keshokutwa kuanzia saa mbili asubuhi katika vituo vya mgahawa wa Steers mtaa wa Ohio na Samora, shule ya sekondari ya Benjamin Mkapa, soko kuu la Kariakoo na Uwanja wa Taifa.
Wakati huo huo, Wambura amesema timu ya taifa ya Gambia inatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanzia leo kwa ajili ya mechi yake dhidi ya Taifa Stars.
Wambura alisema hadi jana, kamati ya Chama cha Soka cha Gambia (GFA) ilikuwa haijatuma taarifa rasmi kwa TFF kuhusu tarehe ya kuwasili nchini kwa timu hiyo.
Lakini vyombo vya habari vya Gambia vimeripoti kuwa, timu hiyo ikiwa na wachezaji 23 na viongozi tisa, ilitarajiwa kuondoka nchini humo jana kuja Dar es Salaam kwa ajili ya mechi hiyo.
Ofisa Habari wa GFA, Bakary Balder alikaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akisema kuwa, msafara wa timu hiyo utaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana na Michezo, Malang Jassey. . Mbali ya Jassey, viongozi wengine katika msafara huo ni Ofisa Utawala wa timu, Modou Sowe, Kocha Luciano Machini, makocha wasaidizi Peter Bonu Johnson na Lamin Sambou, kocha wa makipa, Alhagie Marong, mtaalamu wa tiba mbadala (physiotherapist), Pa Matarr Ndow, mtunza vifaa, Sanna Bojang na daktari wa timu, Kalifa Manneh. Wachezaji ni Musa Camara, Abdou Jammeh, Momodou Futty Danso, Lamin Basmen Samateh, Ousman Koli, Pa Saikou Kujabi, Mustapha Kebba Jarju, Yankuba Mal Ceesay, Demba Savage na Saihou Gassama.
Wengine ni Alieu Darboe, Momodou Ceesay, Pa Modou Jagne, Tijan Jaiteh, Bubacarr Sanyang, Christopher Allen, Musa Yaffa, Sulayman Marr, Mamut Saine, Hamsa Barry, Ali Sowe, Omar Colley na Saloum Faal.
Katika hatua nyingine, Tanzania imepanda kwa nafasi sita kwenye orodha ya viwango ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) iliyotolewa jana na shirikisho hilo. Kwa viwango vya Mei mwaka huu, Tanzania ambayo timu yake ya Taifa (Taifa Stars) inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, ilikuwa inashika namba 145, lakini hivi sasa imefika nafasi ya 139 ikiwa na pointi 214. Mei 26 mwaka huu Taifa Stars ilicheza mechi ya kirafiki na Malawi na kutoka suluhu. Malawi yenye pointi 324 imeporomoka kwa nafasi tano kutoka ya 102 hadi 107. Ivory Coast ambayo katika mechi yake ya mwisho Juni 2 mwaka huu iliifunga Taifa Stars mabao 2-0 imeporomoka kwa nafasi moja kutoka ya 15 hadi 16 ikiwa na pointi 943. Hata hivyo ndiyo inayoongoza kwa upande wa nchi za Afrika katika viwango hivyo.

No comments:

Post a Comment