KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, July 2, 2012

Wachezaji wasiolipa faini kutocheza ligi msimu ujao

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema wachezaji wote ambao
walipigwa faini msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, wakiwemo
wachezaji wa klabu ya Yanga hawataruhusiwa kucheza mechi zijazo za
kinyang'anyiro hadi pale watakapolipa faini hizo.
Akingumza Dar es Salaam leo, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface
Wambura alisema hatua hiyo imefikiwa na TFF ili kuwakumbusha viongozi na
wachezaji husika kwa nia ya kupunguza usumbufu mara itakapoanza
michuano hiyo Septemba Mosi, mwaka huu.
Aliwataja baadhi ya wachezaji wa wakongwe hao wa Yanga ambao
waliadhibiwa baada ya kubainika kufanya fujo kwenye mechi ya mzunguko
wa pili wa ligi kuu dhidi ya timu ya Azam FC iliyochezwa Uwanja wa Taifa Dar
es Salaam ni Stephano Mwasika na mshambuliaji mahiri wa kikosi hicho,
Jerson Tegete.
Wachezaji wengine ni Omega Seme na Nurdin Bakari ambao kila mmoja
aliadhibiwa kutocheza mechi tatu na kutakiwa kulipa ada ya kila mmoja sh,
milioni Moja, naye Nadir Haroub 'Cannavaro' alipewa faini ya sh. 1,000,000.
Wakati Mwasika na Tegete kila mmoja alipigwa adhabu ya faini ya sh. milioni
2, ilhali klabu ya Yanga ilipigwa faini jumla ya sh.1, kutokana na vurugu za
mashabiki zake uwanjani.
Wachezaji hao walitiwa hatiani baada ya Kamati ya Ligi ya TFF kuwabainika
kumtwanga mwamuzi wa kati aliyechezesha mechi hiyo, Israeli Nkongo
kutoka mkoani Dar es Salaam wakidai kuwa alikuwa akipendelea timu pinzani
na kwenye pambano hilo Yanga iliambulia kipigo. "Nimejaribu kupitapita kwa Mhasibu wetu na nimebaini kuwa wachezaji wengi
hawajalipa faini walizopigwa baada ya kufanya vitendo vya utovu nidhamu
kwenye msimu uliopita wa ligi kuu, lakini nachowaasa wanapaswa kulipa faini
hizo ili kujiepusha na usumbufu mara itakapoanza ligi. Kwani kulingana na
kanuni zetu mchezaji asiyelipa faini hatoruhusiwa kucheza mechi yoyote ya
ligi," alisema.
Kauli hiyo ya Wambura imekuja siku chache baada ya mlinzi kushoto Yanga,
Stephano Mwasika kukataliwa kwa dakika chache na refa, Oden Mbaga wa Dar
es Salaam kucheza mechi ya kimataifa ya kujipima nguvu dhidi ya mabingwa
wa soka nchini Uganda, timu ya The Express.
Katika mechi hiyo ambayo Yanga ilitambulisha wachezaji wake wapya
iliyowasajili ilichezwa Jumamosi iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salam na
vijana hao wenye maskani kwenye makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani,
Kariakoo waliibuka na ushindi wa mabao 2 - 1.
Mbaga alimzuia kwa muda Mwasika asiingie kucheza mechi hiyo akitokea
kwenye benchi akidai mchezaji huyo alikuwa amefungiwa mechi kwenye
msimu wa ligi iliyomalizika, lakini hata hivyo dakika chache baada ya sakata
hilo mwamuzi hodari na mwenye beji inayotambuliwa na Shirikisho la Soka la
Kimataifa (FIFA), Mbaga alijilidhisha na kumruhusu Mwasika aingie uwanjani.
Wambura alisema adhabu hizo za wachezaji zilikuwa zikihusu mechi za ligi
msimu uliomalizika, hivyo alichokifanya mwamuzi Mbaga siku hiyo ni kutaka
kujilidhisha ili kuepuka kuingia kwenye matatizo na TFF endapo kama
mchezaji huyo angelibainika kukiuka masharti ya adhabu.
"Kwa mashabiki walifika uwanja siku ile nadhani waliona Mwasika alizuiwa kwa
muda na mwamuzi wa kati, Mbaga ila baada ya kujilidhisha akamruhusu
mchezaji huyo aiingie uwanjani. Hivyo ifahamike kuwa adhabu za kutocheza
mechi ilihusu msimu ulipita na zimemalizika msimu huo huo na tena
haikuhusu mechi za kimataifa," alisema.

No comments:

Post a Comment