'
Wednesday, November 28, 2012
WAGOMBEA DRFA WAONYWA
MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Juma Simba 'Ghadafi' amewaonya wagombea waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho kuepuka kutoa rushwa.
Simba alitoa onyo hilo juzi wakati alipokuwa akitangaza majina ya wagombea 23 waliopitishwa kuwania uongozi wa chama hicho katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 8 mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Alisema kamati yake itakuwa makini kufuatilia nyendo za wagombea katika uchaguzi huo na wale watakaobainika kutoa rushwa kwa wapiga kura, watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Simba amewataka wajumbe wa mkutano huo kuwatendea haki watu wa Dar es Salaam kwa kuwachagulia viongozi wenye sifa na uwezo wa kuendeleza soka katika mkoa huo.
Mwenyekiti huyo alisema yeye na kamati yake wanaamini kuwa, wawakilishi wa vyama vya soka vya wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni watafanyakazi nzuri kwa kuchagua viongozi wenye uchungu wa soka.
"Tumeshaaanza kusikia tetesi kwamba baadhi ya wagombea waliopitishwa kuwania uongozi katika uchaguzi huo wameanza kuwarubuni wapiga kura. Binafsi siamini kama wajumbe wa DRFA watakubali kurubuniwa na kuuza haki yao,"alisema.
Kwa mujibu wa Simba, wameandaa vitambulisho maalumu kwa ajili ya wapiga kura, vitakavyokuwa na picha zao ili waweze kutambulika kirahisi. Pia alisema wameandaa vitambulisho kwa ajili ya waandishi wa habari, ambao watatengewa eneo maalumu la kukaa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment