KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 15, 2012

UKWA: BADO NIPO NIPO KWANZA



LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI machachari wa Nigeria, Osita Iheme amesema bado hajajua ni lini atafunga ndoa na atamuoa nani.
Osita ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Ukwa au Pawpaw alisema juzi mjini hapa kuwa, atafunga ndoa wakati utakapofika.
Ukwa (32) ameelezea msimamo wake huo, kufutia ndugu, jamaa na marafiki kumuhoji mara kwa mara wakitaka kujua ni lini atafunga ndoa.
Licha ya umaarufu alionao katika fani ya uigizaji filamu na pia kuwa mmoja wa waigizaji wanaolipwa vizuri nchini Nigeria, Ukwa hajaoa.
Kaka na swahiba mkubwa wa mwigizaji huyo, Chinedu Ikedieze, maarufu kwa jina la Aki alifunga ndoa mwaka jana na imeripotiwa kuwa, tayari mkewe ni mja mzito.
Ukwa alikiri kuwa anajisikia vibaya kuona kuwa, swahiba wake huyo amefunga ndoa huku yeye akiwa bado anamsaka mchumba wa kumuoa.
"Sielewi lini nitafunga ndoa, lakini naelewa kwamba wakati utakapofika, kila mmoja atafahamu. Siwezi kueleza ni lini nitafanya hivyo," alisema Ukwa.
Aliongeza: "Mungu ananitayarishia njia kwa ajili yangu nami naelekea katika njia hiyo. Nitakapofika, kila mmoja atafahamu."
"Siwezi kusema kama tayari ninaye mchumba ninayetarajia kufunga naye ndoa. Wapo wanawake wengi sehemu mbali mbali duniani. Ni jukumu langu kumsikiliza Mungu atakapozungumza nami na kunionyesha mwanamke sahihi. Wakati utakapofika, nitachagua mwanamke huyo,"alisema Ukwa.
Katika hatua nyingine, Aki na Ukwa wameamua kuanzisha kampuni yao ya kutengeneza filamu, inayojulikana kwa jina la Aki and Pawpaw Entertainment Nigeria (APEN).
Maswahiba hao wamefikia uamuzi huo kwa lengo la kuanza kutengeneza filamu zao wenyewe na kuacha kucheza filamu za watu wengine.

No comments:

Post a Comment