KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, November 24, 2012

MUUMIN ATIMKA TWANGA PEPETA, AANZISHA BENDI MPYA



MWIMBAJI nyota na mwenye makeke katika muziki wa dansi, Muumin Mwinjuma amejiengua katika bendi ya Twanga Pepeta International na kuanzisha bendi mpya ya Victoria Sound.

Mwinjuma alitangaza uamuzi wake huo jana alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam.

Kiongozi huyo wa zamani wa bendi ya Double M alisema amepanga kuisuka vyema bendi yake hiyo mpya ili iwe tishio hapa nchini.

Mwanamuziki huyo alisema amepanga kwenda nchini Kenya kwa ajili ya kusaka wanamuziki nyota na mahiri watakaounda bendi hiyo.

Alisema ameamua kufuata wanamuziki Kenya kwa vile anafahamu vyema kuwa, nchi hiyo imejaliwa kuwa na wanamuziki wengi wa Kitanzania wenye vipaji vya muziki, lakini hawafahamiki hapa nchini.

Alisema aliwahi kufanya hivyo miaka ya nyuma kwa kuwarejesha nchini Badi Bakule, Amina Ngaluma, Rashidi Mwezingo, Rashid Sumuni, Mohamed Mbale wakati alipounda bendi ya Tamtam.

“Hakuna mtu aliyekuwa anawajua kina Ngaluma, lakini walipotua Bongo kila mtu alikubali moto wao, nitafanya hivyo hivyo katika Victoria Sound,” alisema Muumin.

“Kama ilivyo kawaida yangu kwani muziki ni kazi yangu, hivyo nawaomba mashabiki wasubiri kuona yale waliyoyamisi kutoka kwangu nikiwa na bendi hii mpya, na wala haitachukua muda mrefu nitakuwa nimekamilisha kikosi kazi changu na kuwapa raha mashabiki wa muziki wa dansi nchini. Naamini nitafanikiwa kuipandisha chati bendi hii ya Victoria pamoja na kulinda jina na kipaji changu katika tasnia hii ya muziki,” alisema Muumin.

Mkurugenzi wa bendi hiyo, Daniel Denga alisema wanajivunia kumpata mwimbaji nyota na mwenye uwezo wa juu katika anga za muziki wa dansi hapa nchini.

“Bendi yetu ilianzishwa tangu mwaka 2007, lakini hatukuweza kufikia muafaka, hivyo naamini sasa malengo yetu yamefanikiwa na yatatimia kwa kutambua uwezo wa Muumini ni mkubwa na hana mpinzani hapa nchini,” alisema Denga.

Muumin amesema atakwenda Nairobi kwa awamu mbili, ya kwanza ni kufanya usajili na ya pili ni kwenda kuwafanyia uhamisho rasmi wanamuziki kutoka Nairobi kuja jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment