KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 28, 2012

WILFRIED ZAHA, KINDA ANAYEVITOA UDENDA VIGOGO VYA ENGLAND



LONDON, England
KOCHA Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha nia yake ya kutaka kumsajili winga wa klabu ya Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Wilfried Zaha.
Wenger amepanga kumsajili kinda huyo anayekadiriwa kuwa na thamani ya pauni milioni 20 za Uingereza wakati wa usajili wa dirisha dogo Januari mwakani.
Kocha Msaidizi wa zamani wa Arsenal, Pat Rice, ambaye bado anafanyakazi katika klabu hiyo pamoja na mvumbuzi mkuu wa wachezaji, Steve Rowley ndiyo waliompatia Wenger taarifa kuhusu kinda huyo, ambaye walimshuhudia akicheza hivi karibuni.
Arsenal imepanga kuwasilisha ofa ya kumsajili Zaha kwa klabu ya Crystal Palace kwa malipo ya pauni milioni tisa wakati usajili wa dirisha dogo utakapoanza.
Hata hivyo, kuna habari kuwa Mwenyekiti wa Crystal Palace, Steve Parish hataweza kukubali kinda huyo aondoke ndani ya klabu yake kwa kiasi hicho cha pesa.
Alipoulizwa Jumanne iliyopita iwapo ni kweli anamuhitaji mchezaji huyo, Wenger alisema: "Tunatafuta kila mchezaji, atakayeweza kukiongezea nguvu kikosi chetu, lakini kwa sasa hayumo kwenye orodha yangu."
Mbali na Arsenal, klabu zingine zilizoonyesha nia ya kumsajili Zaha ni pamoja na Liverpool, Manchester City na Manchester United.
Zaha (20) amezikuna klabu nyingi za England baada ya kuonyesha kiwango cha juu wakati timu ya taifa ya nchi hiyo ilipomenyana na Sweden katika mechi ya kirafiki ya kimataifa mapema mwezi huu, ikiwa ni mechi yake ya kwanza.
Kinda huyo alianza kuichezea Crystal Palace akiwa na umri wa miaka 17, Mei 2012 na hadi sasa ameshaichezea timu hiyo katika mechi 112 na kuifungia mabao 14.
Wenger anaamini kuwa, Arsenal ni lazima ijenge na kukiimarisha kikosi chake kwa kuwatumia wachezaji vijana waliopo England kama ilivyo kwa Jack Wilshere.
Zaha alirejea uwanjani hivi karibuni baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu na kwa sasa yupo kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya kati yake na viongozi wa Crystal Palace.
Wenger anaamini kuwa, iwapo Zaha ataungana na nyota wengine wa England kama vile Kieran Gibbs, Wilshere na Alex Oxlade Chamberlaini, kikosi cha Arsenal kitakuwa tishio katika ligi kuu ya England na michuano ya kimataifa.
Zaha amesaliwa na miaka miwili na nusu kumaliza mkataba kati yake na Crystal Palace na Wenger amekiri kuwa ni muda mrefu, lakini hawezi kukata tamaa ya kumpata.
Wenger alisema anataka kinda huyo pamoja na wachezaji wengine wa zamani kama vile Theo Walcott na Aaron Ramsey wacheze kwenye kikosi chake kwa muda mrefu.
Msimu uliopita, nahodha wa zamani wa timu hiyo, Robin van Persie aligoma kuongeza mkataba mpya na Arsenal, badala yake aliamua kutua Manchester United kwa uhamisho uliogharimu pauni milioni 24.
Kwa sasa, Arsenal inafurahia uamuzi wake wa kutoa kipaumbele kuwasajili wachezaji chipukizi wa England, ambao wamefanikiwa kuunda kikosi imara.
Kocha huyo anaamini kuwa, kusajiliwa kwa chipukizi wa England kutawafanya wachezaji hao kuichezea timu hiyo kwa kipindi kirefu kuliko ilivyo kwa wachezaji wa kigeni.
Hata hivyo, Wenger alisisitiza kuwa, katika kutekeleza mpango wao huo, watazingatia zaidi uwezo na viwango vya wachezaji.
Zaha ameripotiwa kuwa shabiki mkubwa wa Arsenal tangu akiwa mdogo na hilo linamfanya Wenger awe na uhakika mkubwa wa kumpata wakati wa usajili wa dirisha dogo.
Kuna habari kuwa, tayari Manchester City imeshaanza kufanya mipango ya awali ya kumsajili kinda huyo huku Liverpool na Tottenham nazo zikionyesha nia ya kufanya hivyo.
Zaha alizaliwa Novemba 10, 1992 katika mji wa Abidjan nchini Ivory Coast. Majina yake kamili ni Dazet Wilfried Armel Zaha. Anatumia jezi yenye namba 16. Alijiunga na Crystal Palace kuanzia 2002 hadi 2009 akiwa katika timu ya vijana kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza mwaka 2010.
Amewahi kuzichezea timu za taifa za vijana wa chini ya miaka 19 na 21 za England kabla ya kuvaa uzi wa timu ya taifa ya wakubwa kwa mara ya kwanza katika mechi dhidi ya Sweden iliyochezwa mapema mwezi huu.
Zaha alihamia England akiwa na familia yake wakati akiwa na umri wa miaka minne. Alisoma katika shule ya Whitehorse Manor Junior, Thornton Heath na Selsdon.

No comments:

Post a Comment