KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 28, 2012

TAIFA STARS KAMBINI BAADA YA CHALENJI


TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars inatarajiwa kuingia kambini baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Chalenjji, inayoendelea nchini Uganda.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kambi hiyo itakuwa kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia.
Michuano ya Kombe la Chalenji, iliyoanza kutimua vumbi Novemba 24 kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala, Uganda, inatarajiwa kufikia tamati Desemba 8 mwaka huu.
Taifa Stars inatarajiwa kumenyana na Zambia katika mechi ya kirafiki itakayopigwa Desemba 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kim alisema baada ya pambano hilo dhidi ya Zambia, wachezaji wa Taifa Stars watapewa mapumziko ya wiki mbili kabla ya kuingia tena kambini Januari 6 hadi 20 mwakani kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi nyingine ya kirafiki.
Kwa mujibu wa Kim, mechi hizo mbili zimelenga kuiandaa Taifa Stars kwa pambano lake la michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 dhidi ya Morocco.
Kocha huyo alisema amepanga kuongeza kipa mmoja kwenye kikosi chake ili kuwasaidia makipa wa sasa, Juma Kaseja na Deogratius Munish pamoja na chipukizi kadhaa kutoka timu za vijana wa chini ya miaka 17 na 20 kwa lengo la kuwapa uzoefu.
Kim alisema kwa sasa anafuatilia vipaji vya wachezaji wa Zanzibar, Zanzibar Heroes wanaoshiriki katika michuano ya Kombe la Chalenji nchini Uganda. Zanzibar imepangwa kundi moja na timu za Eritrea, Malawi na Rwanda.

No comments:

Post a Comment