Chama Cha Mapinduzi kimetuma salamu za rambirambi na pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, mashabiki wa wasanii wawili wa sanaa za maigizo na vichekesho Marehemu John Maganga aliyefariki Novemba 24, 2012 jijini Dar es Salaam na Hussein Mkiety aliyejulikana sana kwa jina la usanii ( Sharo Milionea) aliyefariki Novemba 26,2012 kwa ajali ya gari mkoani Tanga.
Katika salamu za Chama, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Itikadi na Uenezi Ndugu Nape Moses Nnauye ametoa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa namna yeye binafsi na CCM kwa ujumla walivyoguswa na Msiba huo mkubwa uliohusisha wasanii wawili vijana kabisa, kwa wakati Mfupi.
Katika salamu zake, Ndugu Nape amesema: “Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa habari za kutokea kwa ajali ya barabarani katika kijiji cha Lusanga Wilayani Muheza mkoani Tanga, iliyosababisha kifo cha kijana Hussein Mkiety.”
Ameongeza Ndugu Nape "Pia nimepokea kwa masikitiko Makubwa Taarifa za kifo cha Msanii we Sanaa ya maigizo Marehemu John Maganga kilichotokea katika hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kuugua kwa muda mfupi."
Ameongeza kuwa Vifo vya vijana hao wawili vilivyotokea katika Umri mdogo Kabisa, ni pigo kwa familia, tasnia ya filamu za maigizo na tasnia ya Sanaa, pamoja na Taifa kwa ujumla, kwani kazi zao zilikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya Sanaa, na Taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment