KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 15, 2012

SIJAWAHI KUPOKEA RUSHWA-DIDA



KLABU ya Azam hivi karibuni ilitangaza kuwasimamisha wachezaji wake watatu nyota, akiwemo kipa Deogratius Boniventura Mushi, maarufu kwa jina la Dida kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa timu pinzani wakati wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, Dida anazungumzia kuhusu tuhuma hizo na mikakati yake katika soka.

SWALI: Wiki iliyopita ilitolewa taarifa na klabu ya Azam ikikuhusisha wewe na wachezaji wenzako wawili, Erasto Nyoni, Said Morad na Aggrey Morris mkituhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa timu pinzani wakati wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Nini ukweli kuhusu tuhuma hizo?
JIBU:Kwa kweli nimejisikia vibaya sana kutokana na kuhusishwa na jambo hilo. Mimi ni Mkristo tena Mromani, sijawahi kufanya jambo hilo hata siku moja katika maisha yangu na kwa kweli taarifa hizi zimeniumiza sana.
Nadhani viongozi wa Azam hawakututendea haki, hasa mimi binafsi. Ni kweli kila kukicha tuhuma hizi zimekuwa zikitawala katika soka ya Tanzania, lakini si jambo zuri kumuhusisha mchezaji bila ya kuwa na ushahidi.
Kwa vile uongozi wa Azam umesema umewasilisha tuhuma hizo TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), nina hamu kubwa ya kusikia matokeo ya uchunguzi wao ili haki itendeke na kwa wale waliojihusisha kweli na vitendo hivyo, sheria ichukue mkondo wake.
Hivyo ndivyo ninavyoweza kuzungumza kwa sasa. Lakini napenda kuweka wazi kuwa, sijawahi kujihusisha na vitendo hivyo hata siku moja katika maisha yangu na kama nimefanya hivyo, Mungu atanihukumu. Namuachia yeye kwa sababu ndiye muweza wa yote.
SWALI: Familia yako ilizipokea vipi hizi taarifa?
JIBU: Naweza kusema kwa mara ya kwanza nimepata aibu kubwa katika maisha yangu. Lakini kwa sababu familia yangu, hasa wazazi, ndugu na marafiki wananifahamu vyema, wameshangazwa na tuhuma hizo na hakuna anayeamini kwamba ninaweza kufanya vitendo hivyo.
Kushangaa kwao kumetokana na ukweli kwamba, mbali na kujihusisha na soka, mimi ni mfanyabiashara hivyo ninakuwa na shughuli nyingi za kufanya na kujishughulisha nazo. Kwa kweli imeniuma sana.
Mbali na kufanya biashara, nilikuwa nikilipwa mshahara mzuri na Azam, hivyo sikuwa na sababu ya kujihusisha na vitendo vichafu kama vile kupokea rushwa. Hakuna timu inayowalipa vizuri wachezaji wake kama Azam. Sidhani kama kuna mchezaji anayeweza kukubali apewe rushwa ili aihujumu timu inayomsaidia kuendesha maisha yake.
Napenda kutumia nafasi hii kuuhakikishia uongozi wa Azam na wapenzi wa soka nchini kwamba, sijawahi kupokea rushwa ili niihujumu Azam na hizi tuhuma kwangu ni za uongo na kupandikiza kwa lengo la kuchafua jina langu.
SWALI: Unadhani tuhuma hizi zinaweza kuwa zimepandikizwa kwa lengo la kukuchafua?
JIBU: Hiyo ni kweli kabisa. Kuna baadhi ya watu, ambao wamekuwa wakipeleka taarifa potofu kwa uongozi kwa lengo la kutuchafua baadhi yetu. Na inasikitisha kuona kuwa, uongozi umekuwa ukizipokea taarifa hizi na kuchukua hatua bila ya kufanya uchunguzi.
Kwa mchezaji yeyote mwenye akili timamu hawezi kufanya kitu kama hicho kwa sababu soka ndiyo ajira yake. Akicheza vizuri, ulaji ndipo unaongezeka. Kwa mtu kama mimi, nikifanya kitu kama hicho ni sawa na kujiua kisoka.
Ukifuatilia kwa makini, katika mechi zetu dhidi ya Simba na Yanga, mimi sikukaa langoni. Mechi zote mbili alicheza Mwadin Ally, sasa iweje niambiwe kwamba nilipewa rushwa wakati sikucheza? Kama huku si kuharibiana, ni nini? Ninawezaje kuhujumu timu wakati sikucheza?
SWALI: Baada ya vipigo hivyo, bodi ya wakurugenzi ya Azam ilifanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi kwa kumuondoa Kocha Boris Bunjak wa Serbia na kumrejesha Stewart Hall, ambaye alitimuliwa mwishoni mwa msimu uliopita. Nini maoni yako kuhusu mabadiliko haya?
JIBU: Kwa hilo siwezi kusema lolote kwa sababu mimi siye mwajiri. Inawezekana uongozi ulimuona Bunjak uwezo wake ni wa chini. Kazi yangu ni kucheza soka, hivyo jukumu langu ni kufuata maelekezo ya kocha yoyote.
SWALI: Baada ya kusimamishwa na uongozi kwa tuhuma za rushwa, unafikiri wachezaji wenzenu watakuwa katika morari?
JIBU: Ni wazi kwamba uamuzi huu umewashtua sana wachezaji wenzetu na nina hakika wapo baadhi ambao wataanza kucheza kwa woga kwa vile watakuwa hawajui hatma yao. Hili ni jambo la hatari sana kwa timu kubwa kama Azam.
SWALI: Baada ya sakata hili, kumekuwepo na uvumi kwamba unataka kurejea katika klabu yako ya zamani ya Simba. Je, kuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizi?
JIBU: Taarifa hizo hazina ukweli wowote. Mimi bado ni mchezaji wa Azam kwa vile nina mkataba nayo, labda litokee jambo jingine. Lakini kwa sasa bado mimi ni mchezaji wa Azam.
SWALI: Una maoni gani kuhusu maendeleo ya soka nchini?
JIBU: Napenda kuwashauri viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), kufuatilia kwa makini mambo yanavyokwenda ndani ya klabu za ligi kuu kwa vile wachezaji wengi wanakosa haki zao za msingi.
Kwa mfano hivi karibuni, mwenzetu Nsa Job aliumia katika mechi ya ligi kuu na kibaya zaidi hakuwa na bima, ingawa sheria zinataka timu zote za ligi kuu ziwakatie bima wachezaji wake.
Sio jambo zuri kuwaacha wachezaji wanaumia na kupata ulemavu kutokana na mechi za ligi huku viongozi wakinufaika kwa mapato ya milangoni. Ni vyema viongozi wa TFF wafuatilie kwa makini suala hili.

No comments:

Post a Comment