KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 21, 2012

MADUDU YA TFF YANATISHA

TFF




KAMATI ya Saidia Serengeti Boys Ishinde imelijia juu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa madai kuwa, limetumia na kugawa vibaya fedha za mapato yaliyopatikana katika mechi kati ya Serengeti Boys na Congo Brazzavile.
Katibu wa kamati hiyo, Henry Tandau aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, kutokana na mgawo huo mbovu uliofanywa na TFF, fedha nyingi ziliishia mifukoni mwa wajanja wachache huku kamati yake ikiambulia sh. milioni moja.
Mchezo huo wa michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2013 uliofanyika wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, uliingiza sh. milioni 23 kutokana na watazamaji 18, 022 waliolipa viingilio.
Katika mechi hiyo, Serengeti Boys iliishinda Congo Brazaville bao 1-0 na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga fainali hizo kwa mara ya kwanza, zitakazofanyika nchini Morocco.
Tandau alisema kamati yake yenye wajumbe 10, ndiyo iliyosimamia maandalizi ya mchezo huo, ikiwa ni pamoja na kuchangisha fedha za kugharamia mchezo baada ya TFF kukosa fedha, lakini cha ajabu haikushirikishwa kwenye mgawanyo wa mapato.
Alisema kiutaratibu, kamati yake ilipaswa kushirikishwa kwenye mgawanyo wa mapato hayo ili kiasi fulani cha fedha kiweze kutumika kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya marudiano itakayochezwa wiki mbili zijazo mjini Brazaville.
Katibu huyo wa kamati alisema walifanikiwa kupata sh. milioni 35 kwa ajili ya kuwalipia tiketi waamuzi kutoka Uganda na Kamisaa kutoka Zambia, ikiwa ni pamoja na kulipa gharama za hoteli kwa timu ya Congo Brazaville iliyokuwa na msafara wa watu 25.
Kwa mujibu wa Tandau, kamati yake ilikuwa ikihitaji sh. milioni 60 ili kufanikisha mechi hiyo, lakini baada ya kupata sh. milioni 35, imesaliwa na deni la sh. milioni 23 wanazodaiwa na uongozi wa hoteli ya JB Del Monte.
Tandau alisema pia kuwa, anashangaa kuona katika mchezo huo, TFF ilitoa sehemu ya mapato kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati timu iliyocheza ni ya vijana wa chini ya miaka 17, ambao kisheria hawatakiwi kukatwa VAT.
Mbali na fedha za VAT, Tandau alisema TFF imekata gharama za mchezo sh. 1,000,537, lakini haijulikani zimepelekwa wapi kwa vile zilipaswa kupelekwa kwenye kamati yake.
Alisema katika mgawanyo huo, TFF imelipa gharama za ulinzi mara mbili kwa kubadilisha lugha ya kujipatia fedha hizo na kuongeza kuwa, fedha hizo ni zile zilizolipwa usafi na ulinzi sh. 2,350,000 na kisha kulipwa tena ulinzi wa mechi sh. 3,500,000.
"Ukiangalia hapa kuna ujanja ujanja uliotumika kujipatia fedha hizo kwani katika fomu ya malipo, wamelipa sehemu mbili ulinzi na kumlipa msimamizi wa mchezo wakati sisi tuliotoa fedha zetu na kusimamia mchezo hatujalipwa kitu," alisema Tandau.
Alisema pia kuwa, TFF imefanya ujanja kwa kukata sh. 1,000,000 kwa ajili ya vitambulisho vya kuingia uwanjani wakati hakuna kitambulisho cha aina hiyo kilichotengenezwa. Alisema siku ya mechi hiyo, hakukuwepo vitambulisho vya aina yoyote.
Kutokana na hali hiyo, Tandau ameiomba TFF na serikali kuangalia upya makato yanayotolewa katika mechi za Serengeti Boys kwa vile hayastahili kutokana na ukweli kwamba timu hiyo haina mdhamini.

No comments:

Post a Comment