'
Wednesday, November 28, 2012
SAFARI YA MWISHO YA SHARO MILIONEA
Na Sophia Wakati, Muheza
MAMIA ya watu wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa na wasanii wa fani mbalimbali jana walishiriki katika mazishi ya msanii nyota wa maigizo na muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Ramadhani, maarufu kwa jina la Sharo Milionea.
Marehemu Sharo Milionea, ambaye alifariki dunia Jumatatu iliyopita kwa ajali ya gari katika eneo la Makuzoni, alizikwa jana saa saba mchana katika kijiji cha Lusanga, Muheza mkoani Tanga.
Miongoni mwa wanasiasa waliohudhuria mazishi ya msanii huyo nyota ni Katibu wa NEC-CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Mkuu wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi
Mbali na viongozi hao wa siasa, mazishi hayo pia yalihudhuriwa na wasanii zaidi ya 450 wa fani za filamu, vichekesho na muziki wa kizazi kipya, wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba, Jacob Steven 'JB' na Vicent Kigosi 'Ray'.
Msiba huo uligubikwa na simanzi zito kutoka kwa waombolezaji, ambao walishindwa kujizuia kuangua kilio, hasa baada ya mwili wa marehemu kuwasili nyumbani kwao kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali teule ya Muheza.
Wasanii waliokuwa karibu na msanii huyo kama vile Mussa Yussuf 'Kitale' pamoja na Amri Athumani 'King Majuto' waliishiwa nguvu kutokana na majonzi waliyokuwa nayo na ilibidi wapate msaada kutoka kwa watu wengine.
Waombolezaji walianza kumiminika kijijini Lusanga tangu juzi
jioni na idadi iliongezeka na kuwa kubwa kuanzia jana asubuhi. Kamati ya mazishi iliongozwa na mkuu wa wilaya ya Muheza,Subira.
Sala ya jeneza iliongozwa na Sheikh Twaha Juma na baada ya sala hiyo, waombolezaji walijipanga mistari miwili kwa ajili ya kubeba jeneza hadi makaburini, umbali wa mita 100.
Akitoa salamu kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi, Nape alisema, Mwenyekiti wa Chama, Rais Jakaya Kikwete amestushwa na kifo cha msanii huyo, na kwamba anatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wapenzi wote wa tasnia ya filamu na muziki wa bongo fleva.
"Napenda kuwapeni pole wote kutokana na msiba huu wa kipenzi chetu Sharo Milionea. Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amenituma nifkishe salam hizi za pole kwenu na amesema amestushwa sana na kifo cha msanii huyu," alisema Nape.
"Tunashukuru Mungu kwamba muda mfupi tuliyeishi naye, Sharo Milionea amefanya mambo yatakayotufanya tumkumbuke daima," alisema Nape na kuongeza:
"Licha ya umri wake mdogo, wingi huu wa watu waliohudhuria hapa kumzika, ni uthibitisho kwamba Sharo Milionea ameacha alama nzuri, hivyo ni vizuri tuliobaki kuiga mfano wake na kuyaenzi aliyofanya," alisema.
Nnauye alisema umefika wakati sasa kwa wasanii kuungana na kuhakikisha jasho lao halipotei wala kunyonywa na wajanja wengine, ambao wamekuwa wakinufaika huku wasanii wakiendelea kubaki masikini.
Nape amevitaka vyombo vinavyohusika kusimamia kazi litaka ihakikishwe kwamba haki za kazi za kisanii za Sharo Milionea alizoacha zisitapanywe, badala yake zilindwe kwa mujibu wa sheria ili ziinufaishe familia ya marehemu.
Katibu huyo wa NEC Itikadi na Uenezi pia alilaani kidendo cha watu waliovamia eneo la ajali na kupora vitu mbalimbali vya marehemu Sharo Milionea ikiwa ni pamoja na kumvua nguo zake. Aliitaka serikali kuhakikisha inawasaka wahusika na kuwatia mbaroni.
Akizungumzia uporaji huo, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, alisema, serikali wilayani humo itahakikisha inawasaka popote walipo, waliohusika na unyama huo wa kumpora marehemu Sharo Milionea wakati wa ajali hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment