KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 15, 2012

NTOTA WAWILI WA YANGA WAPELEKWA TOTO AFRICAN


KLABU ya Yanga imepanga kuwapeleka wachezaji wake wawili kwa mkopo kwa klabu ya Toto African kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Ahadi hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Seif Ahmed 'Magari' alipokutana na viongozi wa Toto African mjini Dar es Salaam hivi karibuni.
Seif alitoa ahadi hiyo kutokana na kufurahishwa na kipigo cha bao 1-0, ambacho Toto African ilikitoa kwa Simba katika moja ya mechi za mwisho za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zilizochezwa wiki iliyopita.
Hata hivyo, Seif hakuwa tayari kutaja majina ya wachezaji hao, lakini kuna habari kuwa, huenda wakawa Idrisa Rashid na Ibrahim Job.
Kocha Msaidizi wa Toto African, Athumani Bilal alikaririwa juzi akisema kuwa, anatarajia kukutana na uongozi hivi karibuni kwa ajili ya kupanga mikakati ya mzunguko wa pili.
Bilal alisema ana hakika viongozi wa Toto watakutana na uongozi wa Yanga kwa ajili ya kupanga mipango ya kuwasajili wachezaji watakaopewa kwa mkopo ili kukiongezea nguvu kikosi chao.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga umekiri kudaiwa zaidi ya sh. milioni 175 na watu mbalimbali.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, baadhi ya madeni waliyakuta kutoka katika uongozi uliopita.
Sanga alisema kwa sasa wanaendelea kuhakiki madeni hayo kabla ya kuanza kuwalipa wahusika.
Akizungumzia usajili, Sanga alisema uongozi umeshakutana na Kocha Ernie Brandts kwa ajili ya kujadili ripoti yake yenye mapendekezo ya wachezaji watakaoachwa.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema, ripoti hiyo pia imeorodhesha majina ya baadhi ya wachezaji, ambao kocha huyo amependekeza wasajiliwe wakati wa dirisha dogo. Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja majina ya wachezaji hao.
Kuna habari kuwa, baadhi ya wachezaji, ambao kocha huyo anawataka ni pamoja na mshambuliaji Felix Themi kutoka Kagera Sugar na Issa Kanduru kutoka Mgambo JKT ya Tanga.

No comments:

Post a Comment