KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 28, 2012

BURIANI SHARO MILIONEA




MSANII nyota wa vichekesho na muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Ramadhani Mkiety, maarufu kwa jina la Sharo Milionea, aliyefariki dunia Jumatatu iliyopita, alizikwa juzi kijijini kwao Lusanga wilayani Muheza mkoani Tanga.
Sharo alifariki dunia kwa ajali ya gari Jumatatu iliyopita saa mbili usiku katika barabara ya Segera-Muheza wakati alipokuwa akitoka Dar es Salaam kwenda Muheza.
Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alisema kwa njia ya simu kuwa, Sharo alipata ajali katika eneo la Maguzonizoga wilayani Muheza baada ya gari alilokuwa akiendesha kuacha barabara na kupinduka mara kadhaa.
Kwa mujibu wa Kamanda Massawe, marehemu Sharo alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 478 BVR na kwamba alikuwa peke yake kwenye gari.
Kamanda alisema hakukuwa na kona kali sana wala ubovu wa barabara kwenye sehemu aliyopata ajali Sharo Milionea.
WASEMAVYO WASANII
Kifo cha marehemu Sharo kilipokelewa kwa mshtuko mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa ndio kwanza anaanza kuchipukia katika fani ya vichekesho na muziki wa kizazi kipya.
Baadhi ya wasanii wenzake walipopata taarifa hizo, walihisi ni za uzushi tu, uliolenga kuwashtua watu na kuwafanya wataharuki. Kwa waliokuwa karibu naye, walitamani taarifa hizo ziwe za kuzusha, wakiamini kuwa, Sharo hawezi kuondoka duniani mapema kiasi hiki.
Wasanii wengine wamemwelezea Sharo kwamba ameiaga dunia akiwa bado mdogo huku akiwa na ndoto nyingi na malengo mengi. Wamekifananisha kifo cha Sharo kuwa ni sawa na kipaji kilichoyeyuka mithili ya mshumaa uliowaka na kuzimwa na upepo wa kifo!
Lakini hivyo ndivyo kifo kilivyo. Hakina taarifa. Humtokea binadamu wakati na muda wowote. Tunatembea nacho. Hakuna anayeweza kufahamu ni lini ataondoka duniani. Ni siri kubwa, ambayo Mwenyezi Mungu amewaficha viumbe wake.
Marehemu Sharo alianza kujipatia umaarufu baada ya kushiriki kwenye filamu za vichekesho zilizokuwa zikitayarishwa na msanii mkongwe wa fani hiyo, Amri Athumani maarufu kwa jina la King Majuto.
Baadaye alijitosa kwenye fani ya muziki wa kizazi kipya, ambapo alifanikiwa kuteka soko la muziki huo baada ya kuibuka na kibao cha Chuki za nini.
Hivi karibuni, Sharo alijiongezea umaarufu zaidi baada ya kushiriki kutengeneza matangazo ya Kampuni ya Simu ya Airtel akiwa na King Majuto.
MAHOJIANO YA MWISHO
Katika mahojiano na gazeti la Burudani yaliyochapishwa mapema mwaka huu, Sharo alielezea kwa kirefu kuhusu alikotoka, malengo na matarajia yake ya baadaye katika fani ya vichekesho na muziki wa kizazi kipya.
Msanii huyo aliyekuwa na mvuto wa aina yake alisema alibuni staili ya usharobaro kwa lengo la kujitofautisha na wasanii wengine. Alisema ubunifu wake huo ulimwezesha kupata mashabiki wengi katika fani zote mbili.
Sharo alisema licha ya kuwepo kwa tabia ya watu wanaojikweza kwa muda mrefu, wakiwa maarufu kwa jina la ‘mabradha meni’, staili aliyoibuni ya watu wa aina hiyo imekuwa na mvuto zaidi.
Alivitaja vitu vingine alivyovibuni kwa lengo la kuupa mvuto ‘ubradha meni’ kuwa ni pamoja na uzungumzaji wake kwa kupinda mdomo, uvaaji, utembeaji, unyoaji nywele na kubandika plasta usoni.
“Staili ya mabradha meni asili yake hasa ni Wamarekani. Kila wakisema neno, lazima wamalizie kwa kusema ‘you know man’. Nami nimeiiga, lakini nimeongezea vionjo vingine zaidi,”alisema.
Hussein alisema alianza kujihusisha na uigizaji tangu akiwa shule ya sekondari na kwamba amewahi kucheza filamu moja na baadhi ya wasanii maarufu kama vile Masanja Mkandamizaji na McReagan wa kundi la Orijino Komedi.
Aliongeza kuwa, fani ya uchekeshaji ni asili yake tangu akiwa mdogo kutokana na kuwafurahisha vijana wenzake kila walipokuwa wakikutana kwa mazungumzo vijiweni kwa kubuni maneno yenye mvuto.
“Kila nilipokuwa nikikaa na kuzungumza na wenzangu, niliposema maneno fulani, walikuwa wakivutiwa nayo sana na kuniona mtu wa ajabu, yaani mchekeshaji,”alisema.
KIPAJI CHA MUZIKI
Hussein alisema aliamua kujitosa kwenye fani ya muziki baada ya kujibaini kwamba, anacho kipaji cha fani hiyo na hadi sasa amesharekodi nyimbo nne. Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Tusigombane, Chuki bure aliomshirikisha Dully Sykes, Nawazamisha aliomshirikisha Nukta na Hawataki alioimba kwa kushirikiana na Kanali Top na Richard Mavoko.
Kwa mujibu wa Hussein, aliweza kurekodi nyimbo hizo kwa msaada mkubwa wa promota maarufu wa muziki nchini, Ustaadh Juma Namusoma, ambaye kwa sasa anamiliki kundi la Watanashati.
Hussein alisema kwa sasa ameshampata mdhamini, atakayekuwa akigharamia kurekodi nyimbo zake pamoja na kurekodi kanda za video, lakini hakuwa tayari kumtaja.
Alisema kwa kumtumia mdhamini huyo, ameanza kuandaa nyimbo zake mpya, ambazo atazirekodi kwa kushirikiana na msanii mwenzake nyota wa vichekesho, anayejulikana zaidi kwa jina la Kitale.
Alikiri kuwa, licha ya kurekodi nyimbo nne hadi sasa, bado hajaweza kupata mafanikio makubwa kimuziki kutokana na fani hiyo kukumbwa na vikwazo vingi. Alisema mafanikio pekee aliyoyapata ni kujulikana na mashabiki wengi wa muziki na pia kupata marafiki wapya kila kukicha.
“Kwa sasa nitaendelea kurekodi wimbo mmoja mmoja hadi hapo mambo yatakapokuwa mazuri ndipo nitakaporekodi albamu,”alisema msanii huyo.
Alipoulizwa madai kuwa, amekuwa akipenda kujifagilia katika vichekesho anavyocheza pamoja na nyimbo zake, Hussein alisema huo ni uigizaji, lakini sivyo alivyo.
AMTAJA KIWEWE
Hussein alikiri kuwa, miongoni mwa watu waliomwonyesha njia katika fani ya uigizaji ni msanii Kiwewe wa kundi la Ze Comedy. Lakini alikanusha madai kwamba, amewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mcheza filamu, Shilole.
“Shilole ni rafiki yangu na ni kama dada yangu. Vivyo hivyo kwa Mzee Majuto, namuheshimu, nampenda na kumuheshimu kama baba yangu," alisema.
Msanii huyo pia alikanusha madai kuwa, aliwahi kugombania jina la Sharobaro na msanii Bob Junior. Alisema jina la kiusanii analotumia ni Sharo Milionea na siyo Sharobaro.
Hussein amekiri kuwa, katika wimbo wa Ferouz wa Starehe gharama, alikubali kuvua nguo zake kwenye picha ya video baada ya kulipwa kitita cha sh. milioni moja na nusu, ambacho alikielezea kuwa kwake ni kikubwa.

No comments:

Post a Comment