KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 15, 2012

MBINU ZA KUWANG'OA RAGE NA KABURU HIZI HAPA



WAKATI Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage ameitisha kikao cha kamati ya utendaji leo kwa ajili ya kujadili mustakabali wa klabu hiyo, viongozi wa matawi ya Jijini Dar es Salaam wamepanga kumshinikiza ajiuzulu.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza kuwa, wanachama wa Simba wamepanga kumshinikiza Rage ajiuzulu kupitia kwa viongozi wa matawi, ambao ameomba kukutana nao Jumapili.
Kwa mujibu wa habari hizo, wanachama hao wameitisha mkutano wa dharula kwa ajili ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na uongozi uliopo sasa madarakani chini ya Rage.
Wanachama hao wameshaandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na taasisi zingine zinazosimamia michezo nchini kuhusu kuitishwa kwa mkutano huo kwa lengo la kupata baraka zao.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alikiri jana kupokea barua hiyo na kuongeza kuwa, wamewapa masharti wanachama hao na kuwataka wafuate taratibu na katiba ya klabu yao.
Kwa mujibu wa katiba ya Simba, wanachama wanaweza kuitisha mkutano wa dharula iwapo watajiorodhesha majina yao na kufika 500 na kwamba wanatakiwa kuwasilisha maombi ya kuitishwa kwa mkutano huo kwa viongozi.
Rage ameamua kuitisha kikao cha kamati ya utendaji kwa lengo la kujadili vurugu zilizotokea baada ya Simba kuenguliwa kwenye uongozi wa ligi kuu ya Tanzania Bara ya kufungwa na timu za Toto African na Mtibwa Sugar katika mechi za mwisho.
Simba imemaliza mzunguko huo ikiwa nafasi ya tatu, kwa kuwa na pointi 23 baada ya kucheza mechi 13. Yanga inaongoza kwa kuwa na pointi 29, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 24.
Rage alikaririwa juzi akisema kuwa, kikao cha leo ndicho kitakachoamua mustakabali wa wachezaji Haruna Moshi 'Boban' na Juma Nyoso, ambao wamesimamishwa kwa muda usiojulikana kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Mbali na kujadili hatma ya wachezaji hao, Rage alisema kikao hicho pia ndicho kitakachoamua kuhusu wachezaji watakaoachwa kwenye usajili wa dirisha dogo mwakani na wapya watakaosajiliwa kwa ajili ya mzunguko wa pili.
Wakati Rage akipanga hayo, wanachama wa Simba wameonekana kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo katika mechi za mwisho za ligi na kuutaka uongozi wake ujiuzulu.
Rage anadaiwa kuwa yupo mbali na timu kutokana na kutingwa na majukumu mengi, ikiwa ni pamoja na ubunge. Rage ni mbunge wa Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM na pia mjumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho.
Baadhi ya wanachama wa klabu hiyo pia wamekuwa wakimshutumu Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange 'Kaburu' kwa madai kuwa, amekuwa akiingilia kazi za Kocha Milovan Cirkovic kwa kupanga wachezaji anaowataka yeye.
Kaburu pia amekuwa akishutumiwa kwa kuwagawa wachezaji wa Simba na kuiongoza klabu anavyotaka yeye bila kukubali kupokea ushauri kutoka kwa viongozi wenzake na wajumbe wa kamati ya utendaji.
Juhudi za kuwapata Rage na Kaburu jana ili kuzungumzia mikakati hiyo ya wanachama, hazikuweza kufanikiwa kwa vile simu zao za mkononi zilikuwa hazipatikani.

No comments:

Post a Comment