'
Tuesday, November 27, 2012
SHARO MILIONEA ALIPORWA SH. MILIONI SITA KATIKA ENEO LA AJALI
SWAHIBA wa aliyekuwa msanii nyota wa vichekesho na muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Ramadhani, maarufu kwa jina la Sharo Milionea, amesema marehemu alikuwa na sh. milioni sita kabla ya ajali.
Akihojiwa na kituo cha redio cha Clouds FM leo usiku, swahia huyo wa Sharo Milionea, Mussa Yussuf maarufu kwa jina la Kitale amesema alizungumza kwa simu na rafiki yake huyo na kumueleza kwamba alikuwa safari kwenda Tanga kumpelekea mama yake sh. milioni sita.
Kwa mujibu wa Kitale, alipata nafasi ya kuzungumza na Sharo Milionea muda mfupi kabla ya ajali hiyo na kupanga kwenda naye katika mazishi ya msanii mwenzao wa filamu, marehemu John Maganga aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita na kuzikwa jana.
Kitale alisema alifanya mazungumzo hayo na Sharo Milionea wakati alipokuwa safarini akirejea Dar es Salaam kutoka Iringa, ambako alikwenda kushiriki kwenye tamasha la Asante Tanzania, lililoandaliwa na msanii Sajuki na mkewe Stara.
Lakini wakati akikaribia kufika Dar es Salaam, Kitale alisema alishangaa alipompigia simu Sharo Milionea na kumueleza kwamba alikuwa safarini kwenda Tanga kumtembelea mama yake.
"Aliniambia hataweza kwenda kwenye mazishi ya Maganga kwa sababu alikuwa na mzigo muhimu aliokuwa akimpelekea mama yake Tanga. Aliniambia alikuwa akimpelekea mama yake shilingi milioni sita kwa ajili ya kazi muhimu,"alisema.
Kabla ya tukio hilo, Kitale alisema marehemu Sharo Milionea alimkaribisha katika nyumba mpya aliyopanga katika maeneo ya Magomeni, Dar es Salaam, ambapo alikuwa akilipa kodi ya shilingi laki mbili kwa mwezi.
Kitale alisema Sharo aliamua kuhamia kwenye nyumba hiyo mpya kwa lengo la kubadili hali ya maisha kwa vile mambo yalishaanza kumuendea vizuri, tofauti na alivyokuwa akiishi miaka ya nyuma.
Swahiba huyo wa Sharo Milionea alieleza kusikitishwa kwake na kitendo cha watu wa kwanza waliofika katika eneo la ajali kumvua marehemu nguo zote alizokuwa amezivaa na kumuacha akiwa na nguo ya ndani.
"Kwa kweli hawa watu wamefanya kitendi kibaya sana," alisema Kitale kwa sauti iliyojaa majonzi makubwa kutokana na msiba huo mzito wa swahiba wake.
Akizungumzia jinsi alivyopata taarifa hizo, Kitale alisema alipigiwa simu na mmoja wa rafiki zake na alishindwa kuziamini hadi alipowasiliana na King Majuto, hali iliyosababisha aishiwe nguvu.
Kitale alisema amempoteza mtu muhimu katika maisha yake na hajui ataendeleaje kushiriki katika fani ya vichekesho na muziki wa kizazi kipya bila ya Kitale.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment