KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 21, 2012

MBRAZIL WA COASTAL UNION APATA KIBALI


Na Sophia Wakati, Tanga
KLABU ya Coastal Union ya Tanga imesema, mshambuliaji wake mpya, Gabriel Barbosa kutoka Brazil ameshapata kibali cha kumwezesha kufanyakazi nchini.
Mwenyekiti wa Coastal Union, Hemed Aurora alisema juzi mjini hapa kuwa, kibali hicho kimetolewa na Idara ya Uhamiaji nchini.
Aurora alisema Barbosa ni miongoni mwa wachezaji, ambao Coastal Union inatarajia kuwasajili wakati wa usajili wa dirisha dogo Januari mwakani.
Alisema wamepanga kufanya usajili huo kwa umakini mkubwa ili kukiongezea nguvu kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mechi za mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Barbosa aliwasili nchini mwanzoni mwa mwezi huu akiwa na mkewe na mtoto wao mmoja wa kiume na ametia saini mkataba wa kuichezea Coastal Union kwa mwaka mmoja.
Coastal Union ilimaliza mechi za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, ikiwa nafasi ya tano kutokana na kuwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi 13, sawa na Mtibwa Sugar, inayoshika nafasi ya nne, lakini zikiwa zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Yanga ilimaliza mzunguko huo ikiwa vinara kutokana na kuwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 13, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 24 na Azam yenye pointi 23.
Aurora alisema kwa sasa, Coastal Union inasubiri ripoti ya Kocha Hemed Morocco ili waweze kuijadili na kuyafanyia kazi mapendekezo yake kuhusu usajili wa nyongeza wa dirisha dogo.
Wakati huo huo, mshambuliaji Njsa Job wa Coastal Union amefanyiwa upasuaji wa goti katika hospitali moja nchini India.
Aurora alisema juzi kuwa, Nsa alifanyiwa upasuaji huo juzi na anatarajiwa kurejea nchini kati ya leo na kesho.
Alisema baada ya kurejea nchini, Nsa atapewa mapumziko ya mwezi mmoja kabla ya kuanza mazoezi mepesi na wachezaji wenzake.
Nsa alivunjika goti wakati wa mechi ya ligi kuu kati ya Coastal Union na JKT Ruvu iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi uliopo Mbagala, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment