KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 15, 2012

DIAMOND AMFAGILIA WALTER WA EBSS


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' amemfagilia mshindi wa shindano la Epiq Bongo Star Search (EBSS), Walter Chilambo kwamba alikuwa na kila sababu ya kushinda taji hilo.
Diamond amesema Walter ni msanii mwenye kipaji na uwezo mkubwa wa kufika mbali kimuziki iwapo atapata timu nzuri ya kumsaidia na pia promota wa uhakika.
Kauli hiyo ya Diamond imekuja siku chache baada ya Walter kuibuka mshindi wa taji hilo katika fainali ya kusisimua iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Walter, ambaye amerithi taji hilo kutoka kwa Haji Ramadhan, aliibuka mshindi baada ya kuwabwaga Salma Abushiri wa Zanzibar na Wababa Mtuka wa Dar es Salaam katika hatua ya fainali.
Ushindi huo ulimwezesha Walter kuzawadiwa kitita cha sh. milioni 50 kutoka kwa wadhamini wa mashindano hayo, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zanter. Shindano hilo liliandaliwa na Kampuni ya Benchmark.
"Kiukweli muda wangu huwa ni mchache sana kukaa kwenye televisheni, lakini siku ambayo Walter aliimba wimbo wa Mawazo, nilikuwa nyumbani, nikamsikiliza kwa umakini sana,"ameeleza Diamond kupitia kwenye tovuti yake wiki hii.
"Nilichogundua ni kwamba (Walter) ana kitu ndani yake. Namaanisha kwamba ana uwezo wa ziada na nafasi nzuri katika muziki wa Tanzania,"alisema Diamond.
Aliongeza: "Suala la kufika kwenye ngazi ya kimataifa hilo ni letu sisi Watanzania kumwezesha pamoja na yeye binafsi kuwa chini ya utawala makini, hasa kipindi hiki anachoanza kuingia katika fani hii ya muziki."
Diamond alifichua kuwa, binafsi alimpigia kura Walter akiwa na imani kubwa kwamba ndiye mshindi wake na kweli hakumuangusha.
"Nimefurahi sana. Namtakia kila la heri,"ameeleza Diamond kupitia tovuti yake, ambayo ni miongoni mwa mitandao yenye wasomaji wengi ndani na nje ya nchi.
Dalili za ushindi kwa Walter zilianza kuonekana mapema kutokana na kuimba nyimbo zenye mvuto na alizozimudu vyema.
Katika hatua ya fainali, washiriki walitakiwa kuchagua wasanii maarufu kwa ajili ya kuimba nao wimbo mmoja. Walter alimchagua Ditto. Katika hatua hiyo, Walter aliimba kibao cha One Love cha Steve na Nikikupata cha Ben Pol.
Akizungumza baada ya kutwaa taji hilo, Walter alisema anamshukuru Mungu kwa sababu hakuamini iwapo angeweza kuibuka mshindi.
Walter alisema kulikuwepo na changamoto nyingi wakati wote wa shindano hilo na kwamba ushindani ulikuwa mkali kwa vile kila mshiriki alipania kuibuka mshindi.
Alisema hakuna mshiriki aliyekuwa akimuhofia kwa sababu alijiamini na kufuata vyema mafunzo ya walimu wake ndio sababu ilikuwa rahisi kwake kuibuka mshindi.
Walter alisema wakati alipoingia kwenye shindano hilo, hakuwa akiufahamu vyema muziki zaidi ya kuwa na uwezo wa kuimba na kuiga nyimbo za wasanii mbalimbali maarufu, lakini kwa sasa amekomaa.
Mshindi huyo wa EBSS 2012 hakuwa tayari kueleza atazitumiaje fedha alizopata kwa kushinda taji hilo. Alisema atajiepusha na matumizi yasiyo na lazima na kuhakikisha kuwa, fedha hizo zinazalisha fedha zingine zaidi.

No comments:

Post a Comment