'
Tuesday, November 6, 2012
MGOMO WA WACHEZAJI WAIPONZA SIMBA
MGOMO baridi unaofanywa na wachezaji wazalendo umeelezwa kuwa ndio chanzo cha timu hiyo kuvurunda katika mechi zake za hivi karibuni za ligi kuu ya Tanzania Bara.
Uchunguzi uliofanywa na Liwazozito umebaini kuwa, baadhi ya wanasoka wazalendo hawaafiki wenzao wa kigeni kulipwa mishahara mikubwa wakati mchango wao ni mdogo katika timu.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, hali hiyo imewafanya wachezaji hao wazalendo wacheze chini ya kiwango kwa lengo la kuushinikiza uongozi uwepo uwiano mzuri wa malipo ya mishahara.
Mmoja wa wachezaji waandamizi wa timu hiyo, aliieleza Liwazozito kwamba, wachezaji kama Komabil Keita na Paschal Ochieng wanalipwa mshahara wa sh. milioni 1.5 kwa mwezi, lakini wamecheza idadi ndogo ya mechi hadi sasa.
Mchezaji huyo alidokeza kuwa, viwango vya mishahara kwa wachezaji wazalendo ni kati ya sh. 500,000 na milioni moja wakati kiwango cha juu cha wanasoka wageni ni sh. milioni tatu.
Felix Sunzu ndiye mchezaji ghali kuliko wote Simba akiwa analipwa mshahara wa sh. milioni tatu wakati Emmanuel Okwi naye amekuwa akishinikiza kuongezwa mshahara katika mkataba wake mpya. Kwa sasa, Okwi analipwa sh. milioni 1.5.
Wachezaji, ambao wamekuwa wakitajwa kulipwa kiwango kidogo cha mshahara wakati mchango wao ni mkubwa katika timu ni pamoja na Shomari Kapombe, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Masoud Nassoro 'Cholo'.
Mrisho Ngasa, ambaye amesajiliwa na Simba akitokea Azam, analipwa mshahara wa sh. milioni mbili wakati Kapombe analipwa sh. 700,000 baada ya kupandishiwa hivi karibuni kutoka sh. 500,000.
Kwa mujibu wa mchezaji huyo, mgomo huo ndio uliosababisha Simba ilazimishwe kutoka sare ya bao 1-1 na Polisi Morogoro kabla ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Mmoja wa viongozi wa Simba amekiri kutambua kuwepo kwa mgomo huo na kuongeza kuwa, wanatarajia kukutana hivi karibuni kujadili hatua za kuwachukulia wachezaji wanaowashawishi wenzao kucheza chini ya kiwango.
Katika mechi ya jana, Mtibwa Sugar ilijipatia mabao yake kupitia kwa Mohamed Mkopi na Hussein Javu, kufuatia uzembe wa kipa Juma Kaseja wa Simba, ambaye mashabiki wameanza kumshutumu kwamba kiwango chake kimeporomoka na anahitaji kupumzika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment