KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 1, 2012

YANGA YAITEKA DRFA


KLABU ya Yanga imeamua kukiteka Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) baada ya wanachama wake maarufu kuchukua fomu za kuwania uongozi wa chama hicho.
Wanachama waliochukua fomu leo katika ofisi za DRFA ni Ahmed Seif 'Magari' anayewania nafasi ya mwenyekiti na Ally Mayay, anayewania nafasi ya makamu mwenyekiti.
Uamuzi wa wanachama hao kuwania uongozi wa DRFA, umekuja siku chache baada ya kubaini kuwa, watani wao wa jadi Simba, wamejaza viongozi wengi katika baadhi ya vyama vya mikoa.
Hivi karibuni, mjumbe wa kamati ya usajili ya Simba, Othman Hassan 'Hassanoo' alifanikiwa kukitetea kiti chake cha mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Pwani (COREFA) wakati makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' alichaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Simba pia imefanikiwa kuweka wanachama wake wengi katika nyadhifa mbali mbali za vyama vya mikoa, akiwemo Athumani Kambi, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Mtwara.
Wakati Simba na Yanga zikipigana vikumbo kuweka wanachama wake katika vyama vya mikoa, wagombea wa nafasi ya urais wa TFF katika uchaguzi mkuu wa chama hicho, nao wamekuwa wakipigana vikumbo kuweka watu wao.
Baadhi ya wagombea wanaotajwa kupachika watu wao mikoani ni pamoja na Jamal Malinzi na Athumani Nyamlani, ambao wametajwa kuwa wanataka kumrithi rais wa sasa wa TFF, Leodegar Tenga.
Kwa sasa, Nyamlani ni makamu wa kwanza wa rais wa TFF wakati Malinzi aligombea wadhifa wa uraia katika uchaguzi uliopita na kubwagwa na Tenga.
Uchaguzi mkuu wa DRFA umepangwa kufanyika Desemba 12 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment