'
Wednesday, November 28, 2012
KILIMANJARO STARS YACHEMSHA KWA BURUNDI
TIMU ya soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars jana ilijiweka katika mazingira magumu ya kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji baada ya kuchapwa bao 1-0 na Burundi.
Katika mechi hiyo ya kundi B iliyochezwa kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala, Uganda, Burundi ilijipatia bao la pekee dakika ya 52 lililofungwa kwa njia ya penalti na mshambuliaji Selemani Ndikumana.
Penalti hiyo ilitokana na kosa lililofanywa na beki Shomari Kapombe kumkwatua Ndikumana ndani ya eneo la hatari. Kapombe alionyeshwa kadi ya njano na alishindwa kuendelea na mchezo kutokana na kuumia.
Kutokana na kipigo hicho, Kilimanjaro Stars sasa italazimika iishinde Somalia katika mechi yake ya mwisho ya kundi hilo itakayochezwa keshokutwa. Iwapo itashinda mechi hiyo, inaweza kushika nafasi ya pili ama kuwa 'best looser'.
Kwa ushindi huo, Burundi imefuzu kucheza robo fainali kutokana na kuwa na pointi sita baada ya kushinda mechi mbili. Itahitimisha mechi za kundi hilo kwa kumenyana na Sudan.
Kilimanjaro Stars ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya nane wakati Mrisho Ngasa alipotoa pasi ndefu kwa Salum Abubakar, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango la Burundi.
Ngasa angeweza kufunga bao dakika ya 30 baada ya gonga safi kati ya Frank Domayo, Simon Msuva na John Boco, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya lango.
Burundi ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya 39 wakati Hamisi Tambwe alipopiga mpira wa adhabu, kipa Juma Kaseja akautema, lakini mabeki wake walitokea na kuondosha hatari.
Amri Kiemba aliyeingia kipindi cha kwanza badala ya Msuva alichangamsha mashambulizi kwa Kilimanjaro Stars na nusura afunge bao dakika ya 41 baada ya kufumua shuti kali, ambalo kipa wa Burundi alilitema na kuudaka tena mpira. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Kilimanjaro Stars ilikianza kipindi cha pili kwa kasi na kupata nafasi mbili nzuri za kufunga mabao dakika ya 47 na 49 na 88 lakini zilipotezwa na Ngasa, Mwinyi Kazimoto na Boco.
Kilimanjaro Stars iliwakilishwa na Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomari Kapombe/Idrisa Rashid, Kevin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar, Mwinyi Kazimoto/Shaaban Nditi, John Boco, Simon Msuva/Amri Kiemba.
Katika mechi ya kwanza ya kundi hilo iliyochezwa kuanzia saa 10 jioni, Sudan ilifufua matumaini ya kusonga mbele baada ya kuichapa Somalia bao 1-0.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment