'
Thursday, November 22, 2012
HANSPOPE KUONGOZA TENA KAMATI YA USAJILI SIMBA, MAJI MAREFU, AZIM DEWJI NAO WAMO
KLABU ya Simba imeiunda upya kamati yake ya usajili na kumrejesha mfanyabiashara, Zacharia Hanspope kuwa mwenyekiti.
Kamati hiyo ilitangazwa jana na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam.
Rage alitangaza kuzivunja kamati zote ndogo za Simba wiki iliyopita kwa madai ya kutokuwa na mchango wowote kwa klabu.
Kuvunjwa kwa kamati hizo kulikwenda sambamba na kufutwa kwa tawi la Mpira Pesa lenye maskani yake Magomeni, Dar es Salaam kwa madai ya kuchochea vurugu klabuni.
Rage alisema ameamua kumrejesha Hanspope katika wadhifa wake huo kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika kusajili wachezaji wapya msimu huu kwa kutumia fedha zake.
Aliwataja wajumbe wengine watakaokuwa wakiunda kamati hiyo kuwa ni mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, Azim Dewji, mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani, maarufu kwa jina la Maji Marefu, Muhsin Ruhwey na Sued Nkwabi.
Rage alisema anatarajia kutangaza majina ya wajumbe wengine wa kamati hiyo hapo baadaye.
Kamati zingine ndogo za Simba zilizovunjwa ni ya ufundi, iliyokuwa ikiongozwa na Ibrahim Masoud 'Maestro', kamati ya nidhamu iliyokuwa chini ya Jamal Rwambow, kamati ya mashindano iliyokuwa chini ya Joseph Itangare 'Mzee Kinesi' na kamati ya fedha iliyokuwa chini ya makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu'.
Kwa mujibu wa Rage, atatangaza wajumbe wapya wa kamati hizo hivi karibuni baada ya mchakato wa kuwateua kumalizika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment