KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, November 26, 2012

YANGA KUWEKA KAMBI UTURUKI




UONGOZI wa klabu ya Yanga umepanga kuipeleka timu hiyo kambini nchini Uturuki kwa wiki mbili na kwamba ziara hiyo itafanyika mapema mwakani.

Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Yanga, Abdalla Bin Kleb amesema leo kuwa, timu hiyo itakwenda huko kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Bin Kleb alisema ziara hiyo imepangwa kufanyika kati ya Desemba mwaka huu na Februari mwakani.

Alisema kocha mkuu wa timu hiyo, Ernie Brandts ndiye aliyewasilisha pendekezo la timu hiyo kwenda kuweka kambi katika nchi hiyo kutokana na uzoefu wake.

Kwa mujibu wa Bin Kleb, ikiwa Uturuki, timu hiyo inatarajiwa kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya timu za nchi hiyo.

Katika hatua nyingine, Brandts ameamua kuwapandisha daraja wachezaji watatu kutoka katika kikosi cha pili cha timu hiyo, kinachoundwa na wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 20.

Aliwataja wachezaji hao kuwa ni kipa Yussuf Abdalla, George Banda na Rehan Kibinga.

No comments:

Post a Comment