'
Wednesday, November 21, 2012
KOMBE LA CHALENZI KUANZA KESHOKUTWA UGANDA
MICHUANO ya soka ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama CECAFA Challenge Cup, inatarajiwa kuanza keshokutwa mjini Kampala, Uganda.
Nchi kumi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na nchi moja mwalikwa, zinatarajiwa kushiriki katika michuano hiyo itakayofikia tamati Desemba 8 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na CECAFA kwa vyombo vya habari wiki hii ilieleza kuwa, michuano hiyo itafunguliwa na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Hayatou atakwenda Uganda akiwa amefuatana na Katibu Mkuu wake, Hicham El-Amrani na baadhi ya wajumbe,Mohamed Raouraoua, Cosntant Omari na Bngangue Appolinaire.
Lengo la CECAFA kumwalika Hayatou kufungua michuano hiyo ni sehemu ya mkakati wake wa kuendeleza soka katika ukanda huu wa Afrika. Hayatou amealikwa na Rais wa CECAFA, Leodegar Tenga.
Akiwa Kampala, Hayatou atahudhuria mkutano mkuu wa baraza hilo uliopangwa kufanyika Novemba 23 mwaka huu kwenye hoteli ya Serena. Pia ameandaliwa hafla maalumu kutokana na kukubali kwake kushuhudia michuano hiyo.
Ratiba ya michuano hiyo inaonyesha kuwa, wenyeji Uganda wamepangwa kufungua dimba keshokutwa kwa kumenyana na jirani zao wa Kenya. Mechi hiyo itapigwa kwenye uwanja wa Namboole kuanzia saa 12 jioni.
Michuano ya mwaka huu imedhaminiwa na Kampuni ya Bia Afrika Mashariki (EABL), kupitia bia yake ya Tusker Lager, kwa dola za Kimarekani 450,000.
Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alisema wiki hii kuwa, lengo la michuano hiyo ni kuzisaidia maandalizi timu za Afrika Mashariki na Kati katika kuwania tiketi za kucheza Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 zitakazofanyika nchini Brazil.
Udhamini wa mwaka huu huo ni ongezeko la aslimia tano, kutoka michuano ya mwaka jana iliyofanyika mjini Dar es Salaam, ambapo Uganda iliibuka bingwa.
Udhamini huo utahusisha usafiri, malazi na huduma nyingine wakati jumla ya dola za Kimarekani 60,000 zitakuwa ni kwa ajili ya zawadi, ambapo bingwa atapata dola 30,000, mshindi wa pili dola 20,000 na wa tatu dola 10,000.
Mechi zote za michuano hiyo zitaonyeshwa na kituo cha televisheni cha Super Sport cha Afrika Kusini.
Nchi zinazotarajiwa kushiriki katika michuano hiyo ni Uganda, Kenya, Ethiopia, Sudan Kusini,Tanzania Bara, Sudan, Burundi, Somalia, Malawi, Eritrea, Rwanda na Zanzibar.
Nchi hizo zimepangwa katika makundi matatu. Kundi A litakuwa na timu za Uganda, Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini, Kundi B litakuwa na timu za Tanzania Bara, Sudan, Burundi na Somalia wakati kundi C litakuwa na timu za Malawi, Eritrea, Rwanda na Zanzibar.
Licha ya nchi za ukanda wa CECAFA kutofanya vizuri katika michuano ya Afrika, ndio unaoongoza kwa kuwa na mashindano makongwe kuliko kanda zote za bara hili. Ilianza kuandaa mashindano hayo kuanzia miaka ya 1920 wakati huo ikijulikana kwa jina la Gossage.
Mwaka 2005, michuano hiyo ilifanyika chini ya udhamini wa bilionea wa Ethiopia mwenye asili ya Saudi Arabia, Sheikh Mohammed Al Amoudi na kupewa jina la Al Amoudi Senior Challenge Cup, lakini baadaye aliondoa udhamini wake na kuchukuliwa na Tusker.
MABINGWA KOMBE LA CHALENJI
Mwaka Bingwa
1973 Uganda
1974 Tanzania
1975 Kenya
1976 Uganda
1977 Uganda
1978 Malawi
1979 Malawi
1980 Sudan
1981 Kenya
1982 Kenya
1983 Kenya
1984 Zambia
1985 Zimbabwe
1986 Haikufanyika
1987 Ethiopia
1988 Malawi
1989 Uganda
1990 Uganda
1991 Zambia
1992 Uganda
1993 Haikufanyika
1994 Tanzania
1995 Zanzibar
1996 Uganda
1997 Haikufanyika
1998 Haikufanyika
1999 Rwanda B
2000 Uganda
2001 Ethiopia
2002 Kenya
2003 Uganda
2004 Ethiopia
2005 Ethiopia
2006 Zambia
2007 Sudan
2008 Uganda
2009 Uganda
2010 Tanzania Bara
2011 Uganda
KUNDI A: Uganda, Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini
KUNDI B: Tanzania, Sudan, Burundi na Somalia
KUNDI C: Malawi, Eritrea, Rwanda na Zanzibar
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment