'
Wednesday, November 21, 2012
KAVUMBAGU: SITAKI KWENDA QATAR
MSHAMBULIAJI Didier Kavumbagu amesema hana mpango wa kuihama Yanga na kujiunga na klabu nyingine yoyote barani Afrika.
Akizungumza na LIWAZOZITO muda mfupi kabla ya kuondoka nchini juzi kwenda Burundi, Kavumbavu alisema taarifa za kutakiwa kwake na klabu moja ya Qatar amekuwa akizisikia kupitia kwenye vyombo vya habari.
"Mimi sijui lolote kuhusu kutakiwa Qatar kwa sababu hata viongozi wangu wa Yanga hawajanieleza lolote kuhusu jambo hilo,"alisema mshambuliaji huyo aliyesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Atletico ya Burundi.
Kavumbagu alisema anachotambua ni kwamba yeye bado ni mchezaji wa Yanga na kama kuna timu inayomuhitaji, inapaswa kufuata taratibu katika kumsajili.
Mwanasoka huyo wa kimataifa wa Burundi ameelezea msimamo wake huo baada ya kuwepo na taarifa kwamba, yeye na Haruna Niyonzima wanatakiwa na klabu za Sudan na Qatar.
Kwa mujibu wa taarifa, Niyonzima anatakiwa na klabu ya El-Merreikh ya Sudan, ambayo imeshawasilisha ofa ya kutaka kumsajili kwa klabu ya Yanga wakati Kavumbagu anatakiwa na klabu moja ya Qatar, ambayo haikutajwa jina lake.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema jana kuwa, bado hawajafikia uamuzi wa kuwauza wachezaji hao kwa vile kilichowasilishwa kwao ni maombi ya awali.
"Kuna taratibu, ambazo zinapaswa kufuatwa katika kuwasajili wachezaji hawa. Kwanza ni lazima kamati ya utendaji ya Yanga ikutane kujadili mambo haya kisha ndipo itoe uamuzi kama tuwauze au la,"alisema Mwalusako, ambaye alikuwa safarini kwenda Mbeya.
Klabu ya Qatar imetoa ofa ya kumsajili Kavumbagu kwa dola 100,000 za Marekani (zaidi ya sh. milioni 150) wakati El-Merreikh imeomba itajiwe bei ya Niyonzima ili iweze kumnunua.
Kwa mujibu wa Mwalusako, Yanga ipo tayari kumuuza Kavumbagu kwa dola 300,000 (zaidi ya sh. milioni 450) kama ilivyo kwa Niyonzima kwa vile wachezaji hao ni lulu kwao.
Niyonzima alisajiliwa na Yanga msimu uliopita akitokea APR ya Rwanda, ambapo usajili wake ulifanikishwa na mjumbe wa kamati ya usajili ya klabu hiyo, Abdalla Bin Kleb.
Kavumbagu kwa sasa ndiye anayeongoza kwa ufungaji mabao katika ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuzifumania nyavu mara nane, akiwa amefungana na Kipre Tchetche wa Azam.
Hata hivyo, kuna habari kuwa umezuka mvutano miongoni mwa viongozi wa Yanga kuhusu kuuzwa kwa Kavumbagu na Niyonzima. Baadhi ya viongozi wanapinga wachezaji hao kuuzwa kwa madai kuwa, kutaidhoofisha timu katika mzunguko wa pili wa ligi.
Lakini viongozi wengine wanaunga mkono wachezaji hao kuuzwa kwa madai kuwa, fedha zitakazolipwa ni zaidi ya zile zilizotumika kuwasajili, hivyo kwao ni faida.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya usajili wa Yanga wameripotiwa kufanya mipango ya kwenda Kampala, Uganda kushuhudia mashindano ya Kombe la Chalenji, yanayotarajiwa kuanza keshokutwa kwa ajili ya kusaka nyota wengine wapya.
Kuwepo kwa mipango hiyo kumeelezwa kuwa ni ishara kwamba, viongozi wa Yanga wameridhia wachezaji hao wawili kuuzwa na kutafutwa wengine wa kuziba mapengo yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment