'
Thursday, November 15, 2012
OMOTOLA AZIDI KUPAA
LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu mwenye mvuto nchini Nigeria, Omotola Jalade amezidi kupaa kwa umaarufu, kufuatia filamu yake mpya ya Last Flight To Abuja kufanya vizuri kimataifa.
Omotola amecheza filamu hiyo kwa kushirikiana na waigizaji wengine maarufu wa Nigeria kama vile Jim Iyke, Jide Kosoko, Hakeem Kae Kazeem na wengineo.
Kufanya vizuri kwa filamu hiyo sokoni, kumeufanya mwaka 2012 uwe wa mafanikio makubwa kwa Omotola. Nakala zaidi ya milioni nane za filamu hiyo ziliuzwa katika wiki ya kwanza.
Kwa sasa, Omotola ndiye mwigizaji tajiri wa kike nchini Nigeria na pia amekuwa bize kucheza filamu nyingi zenye bajeti kubwa ya pesa.
Imeelezwa kuwa, ratiba ya Omotola kwa mwaka huu imejaa kutokana na kutakiwa kucheza filamu nyingi. Omotola ndiye mwigizaji pekee wa kike aliyecheza filamu nyingi mwaka huu.
Hivi karibuni, Omotola alifanya uzinduzi wa filamu yake mpya, inayojulikana kwa jina la Amina, uliofanyika mjini London, Uingereza na kuhudhuriwa na watu wengi maarufu.
Filamu hiyo imeandaliwa na kuongozwa na Christian Ashaiku na ameicheza kwa kushirikiana na Wil Johnson na Vincent Regan wa Uingereza.
Omotola pia ameshiriki kucheza filamu ya 'Ties That Bind' akiwa na baadhi ya wacheza filamu maarufu wa kike duniani kama vile Kimberley Elise, Kofi Adjorlolo, Ama K na Khareemar Aguiar.
Mama huyo wa watoto wanne, ambaye pia ni mwanamuziki amecheza filamu nyingine ya bei mbaya, inayojulikana kwa jina la Up Creek, ambayo ipo katika hatua za mwisho za matayarisho kabla ya kuingia sokoni. Pia ameitwa kucheza filamu mpya ya Teco Benson, inayojulikana kwa jina la Blood on the Lagoon.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment