KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 28, 2012

MR IBU: FAMILIA YANGU ILIKUWA MASIKINI KULIKO ZOTE KIJIJINI



LAGOS, Nigeria
BAADHI ya watu huzaliwa katika familia tajiri, lakini wengine huzaliwa katika familia za kimaskini. Kwa mcheza filamu wa Kinigeria, John Okafor, maarufu kwa jina la Mr. Ibu, anakumbuka wakati wa ujana wake, hakuwahi hata kumiliki kijiko cha kulia chakula.
Akihojiwa na mtandao wa naijerules wiki hii, Mr. Ibu alisema kabla ya kuwa maarufu, aliishi maisha ya dhiki na mateso makubwa.
Mr. Ibu alisema familia yake ilikuwa maskini kuliko zote katika kijiji alichokuwa akiishi cha Umunekwu kilichoko Ezeokwe katika Jimbo la Enugu.
"Baada ya baba yangu kufariki, katapila lilibomoa nyumba yetu, tukawa sawa na wakimbizi katika kijiji chetu,"alisema Mr. Ibu.
"Tulizaliwa wanane, wanaume watano na wanawake watatu.Tulipewa chumba kimoja, ambamo tulilala sote usiku kama vile tupo selo. Mguu mmoja hapa mwingine kule," alisema mcheza filamu huyo huku akiangua kicheko.
"Ukiwa masikini, ni masikini tu. Utalazimika kutazama vitu vingi kutoka upande mwingine. Baba yangu aliacha kunisomesha wakati nilipokuwa bado mdogo. Alifariki mwaka 1975,"alisema.
Mr. Ibu alisema kifo cha baba yake kilisababisha watoto wote wafanyekazi ya kujilisha na pia kumlisha mama yao. Pia alisema alilazimika kufanyakazi za aina mbalimbali ili aweze kupata fedha za kujikimu.
Alizitaja baadhi ya kazi hizo kuwa ni pamoja na kuuza kuni, kunyoa watu nywele, kutengeneza kreti za vinywaji kwa kutumia mbao na pia kupiga picha za mitaani. Alisema pesa alizopata alizitumia kujisomesha elimu ya sekondari.
Mr. Ibu alisema pia kuwa, kuna wakati alilazimika kufanyakazi ya kuuza bucha. Kwamba yeyote aliyekuwa akihitaji kuchinjiwa mbuzi, ng'ombe na nguruwe, alikuwa tayari kwa kazi hiyo.
"Hivyo ndivyo nilivyoweza kuendesha maisha yangu. Ni kupitia katika kazi hizo, niliweza kupata pesa za kujisomesha. Baadaye niliongezewa pesa za shule na kaka yangu,"alisema Mr. Ibu.
Kwa mujibu wa Mr. Ibu, baada ya kuteuliwa kujiunga na Taasisi ya Teknolojia na Utawala ya Enugu, kaka yake alimshauri asome kwa muda mfupi kwa vile isingekuwa rahisi kupata fedha za kulipa mihula yote ya masomo.
"Hakukuwa na muda wa kupumzika kwa sababu yalikuwa ni mapambano wakati wote. Mapambano ya kwenda shule na mapambano ya kuilisha familia yetu na mama yetu,"alisema
Mr. Ibu alisema wakati wa mapambano hayo, waliwapoteza ndugu wawili katika familia yao na kwamba umaskini waliokuwa nao ulimwezesha kujifunza mambo mengi.
"Hivi sasa namshukuru Mungu kwa miujiza yake," alisema Mr. Ibu ambaye ni miongoni mwa wacheza filamu wenye uwezo mkubwa kipesa, akiwa na mke na watoto wawili.

No comments:

Post a Comment